Timu ya Raga ya Kenya yatemwa Paris

Image caption Kenya ilitwaa Ubingwa wa Singapore kwa kuizima Fiji kwa alama 30-7.

Mibabe wa mzunguko wa Raga wa Singapore, kwenye michuano ya wachezaji saba kila upande, Kenya, maarufu Shujaa, wamebanduliwa kutoka fainalia za mzunguko wa Raga mjini Paris, Ufaransa baada ya kupoteza dhidi ya Wenyeji hao, Ufaransa.

Kenya, iliyotwaa Ubingwa wa Singapore kwa kuizima Fiji, 30-7, ilibanduliwa na Ufaransa kwa alama 5-24 kwenye robo fainali ya kombe hilo.

Aidha vijana hao wa Benjamin Ayimba walipoteza mechi ya nusu fainali ya Sahani, dhid ya Australia. Australia iliifunga Kenya 7-26.

Image caption Licha ya kubanduliwa, Kenya imesalia katika nafasi ya Saba kwa kukusanya alama kumi na kuzidisha idadi ya alama hadi 95.

Rais Uhuru Kenyatta aliyeialika timu hiyo ikuluni wiki chache zilizopita alikuwa miongoni mwa mamilioni ya mashabiki walioipa timu hiyo motisha baada ya kupoteza.

‘Nitasalia kuwa shabiki wenu hata licha ya kupoteza, tulenge London,’’ aliandika kwenye ukurasa rasmi wa Rais wa Kenya wa Twitter.

Licha ya kubanduliwa, Kenya imesalia katika nafasi ya Saba kwa kukusanya alama kumi na kuzidisha idadi ya alama hadi 95.

Kenya inatarajiwa kujaribu bahati mjini London, Uingereza kwenye mzunguko wa mwisho utakaopepetwa kuanzia tarehe 21 mwezi huu.