Muhtasari: Habari kuu leo Jumatatu

Miongoni mwa habari nyingine kuu leo, polisi jiji la Manchester wamesema kifaa kilichosababisha mechi kuahirishwa Jumapili kilikuwa bomu feki na Rais mpya wa Ufilipino amesema atatetea kurejeshwa kwa hukumu ya kifo.

1. Polisi wasema bomu la Manchester lilikuwa feki

Haki miliki ya picha EPAPETER POWELL

Maafisa wa polisi nchini Uingereza wamesema kuwa kifaa kilichopatikana katika uwanja wa Old Trafford, hakikuwa bomu bali lilikuwa kifaa cha mafunzo ya vilipuzi.

Kifaa hicho kiliachwa hapo na kampuni moja ya ulinzi iliyokuwa ikifanya mazoezi na mbwa wa kunusa vilipuzi. Ugunduzi huo ulisababisha mechi ya mwisho ya ligi kuu msimu huu katika uwanja huo wa Manchester United kuahirishwa na mashabiki kuamriwa kuondoka.

2. Rais wa Ufilipino ataka hukumu ya kifo irejeshwe

Haki miliki ya picha AFP

Rais mteule wa Ufilipino, Rodrigo Duterte, amekariri sera zake kali za kukabiliana na uhalifu na ulanguzi wa mihadarati nchini humo.

Amesema kuwa ataagiza maafisa wa ulinzi kuwapiga risasi washukiwa wa ugaidi watakaokaidi amri yao.

Bw Duterte amesema anashinikiza bunge la Congress kurejesha tena adhabu ya kifo.

3. Shirika la Uingereza kusaidia kuondoa mabomu

Haki miliki ya picha AFP

Shirika moja la misaada la Uingereza litafanya operesheni ya kuondoa mabomu yaliyotegwa ardhini kuzunguka makanisa saba katika Ukingo wa Magharibu mwa mto Jordan, katika eneo ambalo Wakristo wanaamini kuwa Yesu alibatiziwa.

Eneo hilo lilitekwa na wanajeshi wa Israel mwaka wa 1967, ambao walitega mabomu hayo ya ardhini.

4. Mstari wa wakoloni ulioathiri siasa Mashariki ya Kati

Haki miliki ya picha BBC World Service

Mia mia moja iliyopita, watawala wa kikoloni wa Ufaransa na Uingereza walichora mstari mmoja katika ramani ya eneo la Mashariki ya kati, ambayo inaendelea kubadili siasa za kanda hiyo hadi leo.

Mkataba wa kisiri unaojulikana kama Sykes-Picot, ulitenga eneo na ardhi inayoanzia Iran hadi bahari ya Mediterranean, kuwa himaya ya Uingereza na Ufaransa.

5. Waasi wa FARC kuwaachilia watoto

Haki miliki ya picha AFP

Serikali ya Colombia imesema imeafikiana mpango wa kuwaachilia watoto wanaotumiwa kwenye vita na kundi la waasi la FARC.

Mkataba huo ulioafikiwa kwenye mazungumzo ya amani mjini Havana, utatoa nafasi kwa wapiganaji walio na chini ya umri wa miaka kumi na mitano waliosajiliwa na kundi hilo la FARC kuachiliwa.

Mkataba huo kisha utawajumuisha wapiganaji wote walio na chini ya umri wa miaka kumi na minane.

6.Waliomuua Mfaransa wafungwa jela Misri

Haki miliki ya picha EPA

Na mahakama moja nchini Misri imewahukumu wanaume sita kifungo cha miaka saba gerezani, baada ya kuwapata na hatia ya kumpiga raia mmoja wa ufaransa hadi kufa katika kituo kimoja cha polisi.

Eric Lang, mwenye umri wa miaka 49 na ambaye ni mwalimu alikamatwa miaka mitatu iliyopita mjini Cairo. Kwa mujibu wa upande wa mashtaka, Lang alishambuliwa na wafungwa hao baada ya kuzozana wakiwa kizuizini.