Muhtasari: Habari kuu leo Jumatano

Miongoni mwa habari kuu hivi leo, Bw Trump amesema Bw Bill Clinton alikuwa mbaya zaidi kwa wanawake na Marekani imetoa pesa za kusaidia kukabili Zika.

1. Kiongozi wa upinzani alitaka jeshi kuamua Venezuela

Haki miliki ya picha JUAN BARRETO Getty

Kiongozi wa upinzani nchini Venezuela, Henrique Capriles, ametoa wito kwa jeshi la nchi hiyo kuchagua kati ya rais Nicolas Maduro na katiba.

Amemshutumu Bw Maduro kwa kutangaza hali ya tahadhari nchini humo wiki iliyopita.

Kabla ya bunge la nchi hiyo kupinga uamuzi huo wa rais. Maduro alisema hatua hiyo ilihitajika kwa sababu uhuru wa taifa hilo ulikuwa unakabiliwa na mashambulio ambayo hayakutarajiwa.

2. Trump: Bill Clinton alikuwa hatari zaidi

Haki miliki ya picha Reuters

Mgombea anayetarajiwa kuwania kiti cha urais nchini Marekani kupitia chama cha Republican, Donald Trump, amemkejeli mgombea wa kiti cha urais wa chama cha Democratic Bi Hillary Clinton, kwa kushutumu maoni yake kuhusu wanawake.

BwTrump aliandika kwenye mtandao wake wa kijamii kuwa ameshangazwa na shutuma hizo za Bi Clinton, wakati mumewe alikuwa mtu aliyewadhulumu zaidi wanawake katika historia ya marekani.

3. Marekani kuchangia vita dhidi ya Zika

Haki miliki ya picha AP

Bunge la Seneti nchini Marekani limeidhinisha mswada utakaoidhinisha zaidi ya dola milioni moja kusaida vita dhidi ya virusi vya Zika, ambavyo vinaweza kusababisha matatizo ya uzazi.

Kiasi hicho hata hivyo ni chini ya kiwango kilichopendekezwa na Rais barrack Obama cha dola milioni moja nukta tisa kwa kampeini hiyo.

4. Mexico kuhalalisha ndoa za wapenzi wa jinsia moja

Haki miliki ya picha Reuters

Rais wa Mexico, ametangaza mipango ya kubadili katiba ya nchi hiyo ili kuruhusu ndoa za wapenzi wa jinsia moja kote nchini humo.

Hatua hiyo imejiri baada ya mahakama ya juu zaidi nchini humo kutoa uamuzi ambao unatambua ndoa za jinsia moja.

5. Waandamanaji 75 wakamatwa Ufaransa

Haki miliki ya picha AFP

Maafisa wa kupambana na ghasia nchini Ufaransa wametumia gesi ya kutoa machozi kukabiliana na waandamanaji waliokuwa wakirusha mawe, kulalamikia mpango wa serikali ya nchi hiyo wa kubadili sheria za utendaji kazi nchini humo.

Watu sabini na watano wamekamatwa na polisi.

6. Uhaba mkubwa wa chakula Yemen

Haki miliki ya picha AFP

Mratibu mkuu wa Umoja wa Mataifa anayehusika na masuala ya misaada ya kibinadamu, ameonya kuwa zaidi ya watu milioni saba na nusu katika nchi inayokumbwa na vita ya Yemen wanakabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula, na kuwa taifa hilo linakaribia kukumbwa na ukame.

John Ging amesema wameshuhudia kupungua kwa idadi ya wafadhili.

7. Bunge la Seneti laidhinisha uteuzi wa Fanning Marekani

Bunge la Senate nchini Marekani, limeidhinisha kwa kauli moja uteuzi wa rais Obama, Eric Fanning kuwa katibu wa jeshi.

Fanning atakuwa mtu wa kwanza kukiri ni mpenzi wa jinsia moja kuwahi kuongoza kitengo chochote cha jeshi la Marekani.