EgyptAir: Mabaki ya ndege yatafutwa

Ndege Haki miliki ya picha AFP
Image caption Ndege hiyo ilikuwa imewabeba watu 66

Siku moja baada ya ndege ya shirika la Misri la EgyptAir kutoweka, vifusi vya ndege hiyo bado havijapatikana.

Maafisa wa Misri wakisaidiwa na maafisa wa Ugiriki bado wanaendelea kutafuta vifusi hivyo katika bahari ya Mediterranean.

Maafisa wa Misri awali walidhani kwamba vifusi vilivyopatikana vikielea kwenye bahari hiyo vilikuwa vimetoka kwa ndege hiyo, lakini baadaye ilibainika kwamba havikuwa vya ndege hiyo.

Ndege hiyo ya Airbus safari nambari MS804 ilitoweka kutoka kwenye mitambo ya rada muda mfupi baada ya kuingia anga ya Misri ikitoka Paris.

Jamaa na marafiki wa watu 66 waliokuwa kwenye ndege hiyo wamekusanyika katika uwanja wa ndege wa Cairo wakisubiri habari kuhusu hatima ya ndege hiyo.

Mwandishi wa BBC anasema maafisa wanakabiliwa na shinikizo za kuhakikisha wanashughulikia mkasa huo kwa utaalamu na utu.

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Jamaa na marafiki wa waliokuwa kwenye ndege hiyo wamekusanyika uwanja wa ndege Cairo

Hayo yakijiri, maafisa wa Ufaransa wanajaribu kubaini iwapo kulikuwa na utepetevu wa kiusalama katika uwanja wa ndege wa Charles de Gaulle, Paris kabla ya ndege hiyo kuondoka.

Wachanganuzi wa masuala ya kiusalama wanasema iwapo kulikuwa na bomu kwenye ndege hiyo, basi kuna njia kadha ambazo huenda zilitumiwa kuliingiza.

Kabla ya kufika Paris, ndege hiyo ilikuwa imetua Cairo, Tunis na Eritrea.