Marekani yaiondolea vikwazo Vietnam

Haki miliki ya picha AFP Getty
Image caption Rais Obama nchini Vietnam

Rais Obama ametangaza kwamba serikali ya Marekani itaiondolea vikwazo vya mauzo ya silaha hatari Vietnam,hasimu wake wa zamani.

Akizungumza wakati wa ziara kwa taifa hilo la kikomyunisti ambapo alifanya mazungumzo na viongozi wake ,Obama amesema kuwa hatua hiyo itamaliza mgogoro wa vita baridi uliokuwepo na vietnam.

Marekani inajaribu kuimarisha uhusiano wake na mataifa yaliopo katika bahari ya Pacific ,huku China ikiimarisha umiliki wa baadhi ya maeneo.

Lakini bw Obama amesema vikwazo hivyo havihusiani na sera za Marekani nchini China.

''Inahusu harakati zetu za kutaka kumaliza kile kimetajwa kuwa uhasimu na kuleta ushirikiano na taifa hilo'',alisema huko Hanoi.

Vietnam ni mongoni mwa mataifa ambayo yamezozana na Uchina kuhusu umiliki wa maeneo yaliomo katika bahari hiyo.

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Rais Obama na rais Tran Dai Quang wa Vietnam

Marekani inasisitiza kuwa na uhuru wa kutembea kusini mwa bahari ya China.

Mwaka 2014,mgogoro kuhusu kifaa cha kuchimba mafuta karibu na kisiwa cha Paracel ulisababisha mgogoro kati ya vyombo vya baharini vya China na Vietnam mbali na maandamano ya kupinga China nchini Vietnam.

Mafisa wa Ikulu ya White House walisema vikwazo hivyo vya silaha vilivyowekwa tangu mwaka 1984,vitaondolewa iwapo haki za kibinaadamu nchini Vietnam zitaimarika.