Muhtasari: Habari kuu leo Jumanne

Miongoni mwa habari kuu leo, mkanda wa video umemchongea waziri Brazil, Wachina wanatumia nguruwe kutibu upofu katika binadamu na popo wanazua balaa Australia.

1. Mkanda wa video wamponza waziri Brazil

Image caption Juca amesema ameeleweka visivyo

Waziri mmoja mashuhuri katika serikali mpya ya Brazil, amejiuzulu baada ya kunaswa katika mkanda wa video, akila njama ya kupanga namna ya kuzuia uchunguzi wa mojawapo ya kashfa kubwa mno za ufisadi nchini humo.

Katika mkanda huo, waziri huyo wa mipango, Romero Juca, anasema kuwa kufanikiwa kwa mpango wa kuidhinisha kura ya kutokuwa na imani na Rais aliyesimamishwa kazi, Dilma Rousseff, kutasimamisha uchunguzi wa ufisadi ndani ya kampuni kubwa ya taifa ya mafuta Petrobras.

Bw Juca anasema kwamba matamshi yake yameeleweka vibaya.

2. Viongozi Ulaya wafurahia matokeo Austria

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Hofer aliongoza kwa asilimia 0.6 ya kura dhidi ya mpinzani wake

Viongozi wakuu barani Ulaya wameeleza kuridhishwa kwao na matokeo ya uchaguzi wa urais nchini Austria ambapo mgombea wa chama cha mrengo wa kulia cha Freedom, Norbert Hofer, alishindwa na kura chache mno.

Waziri wa mashauri ya nchi za kigeni wa Ujerumani, amesema kuwa bara Ulaya sasa linapumua vizuri na kwa urahisi mno.

Naye waziri mkuu wa Ufaransa anasema Manuel Valls ameridhishwa pia.

3. Wanasayansi watumia nguruwe kutibu upofu

Haki miliki ya picha Getty

Wanasayansi wa Uchina wamefaulu katika tiba yao mpya ya majaribio ya kutibu upofu.

Walitumia nguruwe katika majaribio hayo ya tiba ya kuondoa upofu, ambapo walitumia konea kutoka kwa wanyama hao.

Sasa wamesema wana imani kwamba hilo litafaa sana kutokana na uhaba wa konea za binadamu.

Inakisiwa kuwa Wachina wapatao 5 milioni wanakabiliwa na matatizo ya konea, sehemu ya mbele ya jicho iliyo ngumu na inayowezesha miali ya mwanga kupenya.

Matatizo ya konea husababisha watu wengi kuwa kipofu.

4. UN yataka raia waruhusiwe kuondoka Fallujah

Haki miliki ya picha AFP
Image caption IS wamedhibiti mji wa Fallujah tangu 2014

Umoja wa Mataifa imetoa wito wa haraka wa njia itakayowaruhusu raia kuondoka mji uliozingirwa wa Fallujah, nchini Iraq.

Maelfu ya majeshi ya serikali pamoja na wapiganaji wameanza kukabiliana vikali kungangania mji huo wa Fallujah, ambao umekuwa mikononi mwa wapiganaji wa Islamic State kwa miaka miwili sasa.

5. Marekani yawataka waasi kukomesha vita Syria

Haki miliki ya picha EPA SANA

Marekani imeyaomba makundi ya waasi nchini Syria kukomesha mara moja mapigano na kukumbatia amani. Mnamo siku ya Jumapili wiki hii, zaidi ya makundi 30 hasimu ya waasi yalisema kwamba yatavunjilia mbali mwafaka wa amani na kuingia tena katika vita, iwapo serikali ya Rais Bashar al- Asaad, haitakomesha mapigano nje na ndani ya mji wa Damascus, katika kipindi cha saa 48.

6. Popo wahangaisha wakazi Bateman Bay, Australia

Haki miliki ya picha Thinkstock

Wakuu katika jimbo la New South Wales nchini Australia, wametangaza hali ya tahadhari, ili kusaidia mji mmoja ambao umezingirwa na maelfu ya popo. Wakazi wa mji wa Bateman Bay, wanasema kuwa kelele za kuudhi, harufu mbaya na kinyesi cha popo, vinawapa kero kubwa.

Mamlaka kuu ya jimbo hilo, sasa inapania kutumia dola 1.8 milioni, kuwahamisha popo hao, ambao pia wanafahamika kama mbweha wanaopaa.

7. Je, Wachina walitangulia kugema pombe?

Haki miliki ya picha Thinkstock

Na wanahistoria kaskazini mwa China, wamefukua na kutambua kile wanachoamini kuwa ni vigae vya nyungu vinavyoonyesha kuwa pombe ilianza kugemwa katika eneo hilo, yapata miaka 5000 iliyopita.