Upinzani wasitisha maandamano Kenya

Muthama
Image caption Bw Muthama amesema maandamano yatarejelewa suluhu isipopatikana

Muungano wa upinzani nchini Kenya umeahirisha kwa muda maandamano ambayo umekuwa ukiandaa kila wiki katika miji mikuu nchini humo.

Mmoja wa viongozi wa muungano huo, Seneta wa Machakos Johnstone Muthama amesema uamuzi wa kuahirisha maandamano hayo umechukuliwa kuipa serikali muda wa kuitisha mazungumzo.

Muungano huo wa Coalition for Reforms and and Democracy (CORD) umeipa serikali makataa ya siku 10 la sivyo urejelee maandamano hayo.

Viongozi wa CORD wanataka maafisa wakuu wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (IEBC) wajiuzulu wakisema tume hiyo haiwezi kuandaa uchaguzi mkuu huru na wa haki mwaka ujao.

Walikuwa wameandaa kuandamana hadi afisi za tume hiyo miji mbalimbali nchini Kenya hadi maafisa hao wajiuzulu.

Maandamano hayo yamekuwa yakikumbwa na vurugu huku polisi wakishutumiwa na mashirika ya kutetea haki za kibinadamu kwa kutumia nguvu kupita kiasi.

Haki miliki ya picha EPA
Image caption Maandamano hayo yamekumbwa na vurugu

Jumatatu wiki hii, mmoja wa waandamanaji alifariki kwenye maandamano mjini Kisumu, magharibi mwa Kenya.

Msemaji wa serikali Eric Kiraithe Jumanne aliambia wanahabari kwamba maafisa 29 wa polisi walijeruhiwa wakati wa maandamano hayo.

Serikali hiyo imesema maandamano hayo ni haramu.