Pesa za elimu ya bure zafujwa Kenya

Fred
Image caption Dkt Matiang'i amesema hakuna mifumo ya kuzuia ufujaji wa pesa

Uchunguzi uliofanywa na tume ya kupambana na ufisadi nchini Kenya umefichua kuwa walimu wakuu nchini humo walifuja pesa za elimu ya bure kwa shule za msingi katika taifa hilo.

Walimu wakuu wanadaiwa kutumia pesa zilizotengwa kununua vifaa vya shule kama vile vitabu kwa masuala tofauti.

Wakuu hao wanalaumiwa kwa kutumia pesa za vitabu kugharamia safari za nje na kujilipa marupurupu.

Hali hii inalaumiwa kusababisha uhaba wa vitabu na dawati katika maelfu ya shule za msingi nchini Kenya. Aidha baadhi ya walimu wakuu waliwakopesha wazazi pesa hizo bila ya wazazi kuzirudisha.

Image caption Waziri Matiangi akipokea ripoti

Kulingana na ripoti hiyo, shule nyinginezo zilipokea pesa hizo kupitia akaunti ya shule tofauti. Hili limetiliwa shaka kwani kila shule inastahili kupokea pesa kwa akaunti yake kwa minajili ya uwajibikaji.

Waziri wa Elimu Dkt Fred Matiangi alilaumu kutokuwepo kwa namna ya kuzuia ufujaji. '

Kwa upande wake, afisa mkuu mtendaji wa tume ya maadili na kupambana na ufisadi nchini Kenya, Halakhe Wako, amesema kuwa serikali ya Kenya inastahili kuwachukulia hatua walimu husika ili kukomesha tabia hiyo.

Mapema mwaka huu rais Uhuru Kenyatta alimuagiza waziri Matiangi kuanzisha uchunguzi juu ya jinsi fedha za elimu ya bure zinavyotumika.

Mnamo mwaka wa 2010 mataifa ya marekani na Uingereza yalisimamisha ufadhili wao kwa wizara ya elimu na kusema kuwa hatua hio ilitokana na wizi wa fedha za elimu ya buire.

Serikali ya Kenya hutumia shilingi bilioni 14 kila mwaka kufadhili elimu ya bure.