Muhtasari: Habari kuu leo Jumatano

Miongoni mwa habari nyingine kuu leo, mawaziri wa fedha wa EU wamekubali kuipa Ugiriki pesa zaidi na Wakurdi wameshambulia mji mkuu wa Islamic State.

1. Ugiriki kupokea fedha zaidi kutoka EU

Haki miliki ya picha AFP

Mawaziri wa fedha kutoka maeneo yanayotumia Euro wamekubaliana kutoa kiasi kingine cha fedha kinachofikia dola bilioni 11.5, kuisaidia Ugiriki. Baada ya mazungumzo yaliyoendelea hadi usiku mjini Brussels, pia walikubaliana kuipa Ugiriki nafuu ya ktolipa madeni, kwa kipindi cha miaka miwili.

2. Wakurdi washambulia mji mkuu wa IS

Haki miliki ya picha Reuters

Kundi la wapiganaji wa Islamic State linakabiliwa na vita vikali maeneo mawili wakati huu linapojaribu kuongeza maeneo linayodhibiti nchini Syria na Iraq.

Muungano wa Kikurdi, unaoongozwa na makundi yenye silaha katika maeneo ya kaskazini mashariki mwa Syria, umetangaza kuanza rasmi kwa operesheni kali karibu na mji mkuu wa IS wa Raqqa.

Nchini Iraq, majeshi, wanamgambo na makabila tiifu kwa serikali, yanaendelea na mashambulizi dhidi ya IS katika mji wanaoudhibiti wa Falluja.

3. Cuba kuruhusu biashara za kibinafsi

Haki miliki ya picha EPA

Serikali ya kikomunisti ya Cuba imetangaza kuwa itahalalisha biashara za kibinafsi ndogo ndogo na za wastani, katika juhudi zake za hivi punde za mabadiliko ya kiuchumi.

Mabadiliko hayo yalianza baada ya Rais Raul Castro kutwaa uongozi wa taifa hilo kutoka kwa kakake Fidel, mnamo mwaka wa 2008.

Hatua hiyo itapanua pakubwa sekta ya biashara ya kibinafsi katika taifa hilo la mwisho duniani kuruhusu kuwa na uchumi unaodhibitiwa na serikali.

4. Rais wa Somalia ataka mazungumzo kuhusu wakimbizi

Haki miliki ya picha Reuters

Kwa mara ya kwanza tangu Kenya ilipotangaza kufungwa kwa kambi kubwa ya wakimbizi ya Daadab kaskazini mwa nchi hiyo, Rais wa Somalia Hassan Sheikh Mohamed ametoa wito kwa serikali ya Kenya kurejea katika meza ya mazungumzo kati yake, shirika la Umoja wa Mataifa linalowashughulikia wakimbizi UNHCR, pamoja na serikali ya Somalia, ili kujadili upya suala hilo.

5. Erdogan aionya EU kuhusu mkataba wa wahamiaji

Haki miliki ya picha EPA

Na Rais wa Uturuki, Recep Tayyip Erdogan, amesema bunge la nchi yake litaweka kikwazo kwenye makubaliano yaliyoafikiwa na muungano wa mataifa ya bara Ulaya, kuzuia mtiririko wa wahamiaji katika Bahari ya Aegean.

Amesema ni lazima wananchi wa Uturuki waruhusiwe kuzuru mataifa ya bara Ulaya bila kuhitajika kuwa na viza huria.

Nao maafisa wakuu wa muungano wa EU, wamesema kuwa hawataweza kuwapa viza huria za usafiri kwa Waturuki, hadi pale Ankara, itakapokubalia kuifanyia mabadiliko sheria yake ya kukabiliana na ugaidi.

6. Marekani yataka muuaji ahukumiwe kifo

Haki miliki ya picha AP

Idara ya haki nchini Marekani inasema kuwa itatafuta hukumu ya kifo dhidi ya raia mmoja mweupe ambaye anatuhumiwa kuwauwa wafungwa tisa weusi katika kanisa moja la kihistoria katika eneo la South Carolina mwezi Juni mwaka uliopita wa 2015.

Dylann Roof, anakabiliwa na makosa 33, ikiwemo uhalifu wa chuki na matumizi mabaya ya silaha.

7. Afisa wa UN afurahia kikosi cha AU

Haki miliki ya picha AFP

Afisa anayesimamia shughuli za kulinda amani katika Umoja wa Mataifa, amesema ana furaha kubwa kwamba kikosi cha Muungano wa Afrika cha kushughulikia hali kwa dharura sasa kitaanza kazi hivi karibuni.

Herve Ladsous ameliambia baraza kuu la usalama la Umoja wa Mataifa kuwa hilo ni muhimu sana kwani tisa kati ya vikosi 16 vya Umoja wa Mataifa vya kulinda huhudumu Afrika.