Uturuki: Malkia wa urembo jela kwa kumtusi rais

Haki miliki ya picha AP
Image caption Merve Buyuksarac, mwenye umri wa miaka 27 alipatikana na hatia ya kumtukana hadharani afisa huyo mkuu wa serikali

Mahakama moja mjini Istanbul imemhukumu mshindi wa zamani wa tuzo la urembo nchini Uturuki kwa kumtusi rais wa nchi hiyo Recep Tayyip Erdogan.

Amehukumiwa kifungo kilichoahirishwa cha miezi 14 gerezani.

Merve Buyuksarac, mwenye umri wa miaka 27 alipatikana na hatia ya kumtukana hadharani afisa huyo mkuu wa serikali.

Anasemekana pia aliandika kwenye mtandao wake wa kijamii pamoja na kuwatumia watu shairi lenye matusi katika mtandao wake wa Instagram.

Wakili wake amesema kuwa amepinga hukumu hiyo katika mahakama kuu ya bara Ulaya.

Haki miliki ya picha AP
Image caption Uturuki: Malkia wa urembo jela kwa kumtusi rais

Bi Buyuksarac, amekanusha madai yote dhidi yake.

Wanaharakati wa kupigania haki za kibinadamu wanasema kuwa kesi hiyo ni mojawepo ya njia ya serikali ya rais Erdogan kukandamiza uhuru wa kujieleza.

Hadi kufikia sasa takriban watu 2,000 wengi wao wasanii nyota na hata wanafunzi wameshtakiwa kwa kumkejeli au hata kumtusi rais huyo tangu mwaka wa 2014.

Hukumu hiyo iliahirishwa ilimradi tu asirudie makosa hayo katika kipindi cha miaka mitano ijayo.