Uganda yawashtaki upya washukiwa 5 wa ugaidi

Image caption Uganda yawashtaki upya washukiwa 5 wa ugaidi

Uganda imewafungulia upya mashtaka washukiwa 5 wa mashambulizi ya kigaidi yaliyotokea nchini humo mwaka wa 2010 ambao walikuwa wameachiwa huru juma lililopita.

Msemaji wa polisi Fred Enanga katika taarifa kwa vyombo vya habari amesema kuwa watano hao wamefunguliwa mashtaka ya kughushi stakabadhi rasmi za serikali wakati wakiwa rumande kusubiri kesi dhidi yao.

Enanga anasema kuwa watano hao Omar Awadhi Omar, Mohammad Hamid Suleiman almaarufu Abu Zainab, Abubakaer Batemyeto, Dr Ismail Kalule na Yahya Suleiman Mbuthia wakiwa katika gereza la Luzira walishiriki njama zaidi ya kuishambulia Kampala na wakaghushi stakabathi za serikali mbali na kutoa msaada kwa wahusika wengine waio mbele ya mahakama hiyo jijini Jinja.

Image caption Suleiman Mbuthia akiwa kizimbani

Watano hao walikamatwa punde baada ya kuachiwa huru na mahakama ya Kampala kwa makosa ya mashambulizi ya kigaidi yaliyosababisha vifo vya watu 74 mwaka wa 2010 walipokuwa wakitizama mechi ya kombe la dunia.

Watano wengine walihukumiwa kifungo cha maisha jela kwa shambulizi hilo lililodaiwa kutekelezwa na kundi la wapiganaji wa kiislamu la Alshaabab.