Maelezo mafupi kuhusu David Cameron

David Cameron akiwa katika harakati za kampeni.
Image caption Kiu ya chama cha Conservative kurudi madarakani imemfanya David Cameron kuwa na matumaini katika kupambana na Gordon Brown, Waziri mkuu wa sasa kutoka chama cha Labour.

David Cameron wakati fulani alijitaja kama ‘mrithi wa Tony Blair’. Hakika kuna mfanano wa namna alivyoweza kwa kutumia kikundi kidogo cha wanasiasa wa ‘kisasa’ kulazimisha mabadiliko ndani ya chama ambacho husita kufanya mabadiliko.

Pia Bw Cameron mwenye umri wa miaka 43 anafanana na Waziri Mkuu wa zamani Bw Blair kwa umahiri wake wa kuongea mbele ya kamera za runinga.

Akiwa ni mtoto wa dalali wa hisa, Bw Cameron alikulia katika eneo la Newbury, Berkshire, pamoja na kaka yake aitwaye Alec na dada wawili Tania na Claire.

Baada ya elimu ya awali, akafuata jadi ya kifamilia na kusoma Eton na baadaye chuo kikuu cha Oxford, ambapo alipata daraja la juu kabisa (la kwanza) katika Falsafa, Siasa na Uchumi. Mhadhiri wake wa Oxford aitwaye Vernon Bogdanor anamtaja Cameron kama mmoja wa wanafunzi wenye uwezo mkubwa aliowahi kufundisha.

Chuoni Oxford, hakujishughulisha na siasa za wanafunzi, lakini alikuwa mwananchama wa klabu ya Bullingdon dining, maarufu kwa unywaji wa pombe na mienendo mibaya. Hata hivyo Bw Cameron siku zote ameepuka kuongelea suala hili la unywaji mkali wa pombe chuoni na amekanusha kujihusisha na utumiaji wa madawa ya kulevya wakati akiwa mwanafunzi.

Lakini inaweza kuwa ni makosa kufikiri kuwa Bw Cameron alikuwa tu mtu wa tabaka la aina ya viongozi wa chama cha Tory wa zama zilizopita. Hii ni kwa kuwa sehemu muhimu ya mvuto wake kisiasa imekuwa ni madai yake ya yeye kuwa sambamba na Uingereza ya leo kuliko wapinzani wake kutoka chama cha Labour.

Anakamilisha maneno yake haya pale anapokiongoza chama chake kukumbatia dhana zenye mvutano wa kisiasa leo hii kama vile mabadiliko ya hewa duniani na haki za mashoga.

Kupanda ngazi

Historia ya Bw Cameron ya kufanya kazi ndani ya makao makuu ya chama cha Conservative wakati kikiwa madarakani inachukuliwa kama nguvu iliyomwezesha kukibadilisha chama hicho.

Baada ya kuhitimu Oxford, alifanya kazi katika idara ya utafiti ya chama cha Conservative ambapo pia alihusika katika kutoa muhtasari kwa Waziri Mkuu John Major juu ya maswali mbalimbali kutoka kwa wabunge.

Pia alikuwa akiambatana na Waziri wa fedha Norman Lamont, baada ya sarafu ya pauni kupata misuko suko katika mfumo wa kubadilisha fedha.

Bada ya hapo Bw Cameron kwa miaka saba akafanya kazi kama mkuu wa mahusiano ya umma katika kampuni ya matangazo televisheni ya Carlton. Wakati wote huo, alifanya jitihada za kuwania ubunge, lengo ambalo aliweza kulifanikisha mwaka 2001, pale aliposhinda katika jimbo la Witney.

Wakati huu Bw Cameron alikuwa tayari amemwoa Bi Samantha, binti wa mmilikaji wa ardhi Sir Reginald Sheffield. Bi Samantha anamiliki kampuni yake ya vifaa vya maofisini na mashuleni. Wamebahatika kupata watoto wawili na mwezi wa tisa wanatarajia kupata mtoto mwingine baada ya uchaguzi.

Hamasa

Mtoto wao wa kwanza aliyekuwa akiitwa Ivan, alizaliwa na ulemavu mkubwa na alihitaji uangalizi wa karibu sana. Hata hivyo alifariki mwezi wa pili mwaka jana 2009.

Changamoto ya kumtunza mtoto Ivan na moyo wa kujituma wa wafanyakazi wa afya ya jamii katika kumhudumia mtoto huyo, inatajwa na marafiki wa familia hiyo kama mambo yaliyoweka alama nyingine katika maisha yao na kuleta maana mpya za maisha.

Bw Michael Howard aliyekuwa kiongozi wa chama cha Conseravative alikiona kipaji cha Cameron katika miaka ya 1990. Lakini ni watu wachache waliweza kumpa Bw Cameron nafasi ya kuweza kufanya vyema pale alipojitokeza kugombea kumrithi Bw Howard kama kiongozi wa chama mwaka 2005. Wakati huo alikuwa ni msemaji wa chama katika masuala ya elimu na mbunge.

Lakini katika mkutano wa chama, hotuba yake mahiri aliyotoa bila ya kuwa na maneno ya kujikumbusha au muhtasari, iliweza kubadilisha mawazo ya watu ndani ya chama. Aina hii ya utoaji wa hotuba imekuwa sasa ni sehemu ya utambulisho wa Bw Cameron kisiasa.

Lakini katika miezi yake ya mwanzo ya uongozi wa chama baadhi ya watu hawakuvutiwa na mtazamo wake juu ya suala la kushughulikia wakosaji wenye umri mdogo. Bw Cameron anapendelea wakosaji wachanga kupewa upendo zaidi kama njia ya kuwabadilisha tabia.

Wakati mgumu

Katika mwanzo wa uongozi wake, bwana Cameron amekuwa akifanya jitihada za kubadilidha taswira isiyopendeza ya chama na kuongelea matumaini mapya na kuleta mgawanyo wa faida za kukua kwa uchumi kwa wote.

Alisisitiza kuondokana na kushikilia sana fikra juu ya Ulaya na kutaka chama kijikite na masuala ya mazingira na huduma za afya.Vile vile kukaribisha wanawake na wagombea nafasi za uongozi kutoka katika jamii za makabila mbalimbali.

Vile vile kwa ujanja akatumia kashfa ya gharama za wabunge kujitambulisha mwenyewe kama mwana siasa aliye tayari kuleta mabadiliko.

Pia Bw Cameron amebahatika kuungwa mkono na wanasiasa wakongwe ndani ya chama.

Wakati huo huo akawa akifanya vyema katika kura za maoni- licha ya kuwa ilibidi atoe onyo kwa wapiga kura kwamba wategemee makato katika matumizi ya bajeti ya serikali..

Licha ya mtazamo huo, Bw Cameron ameendelea kufanya vyema katika kura za maoni, ukiondoa kipindi kifupi tu wakati Bw Gordon Brown alipoingia madarakani mwaka 2007. Bila shaka ni matumaini yake kuwa hali njema katika kura za maoni itaendelea na kupata kura nyingi katika siku ya uchguzi mkuu.