Chama cha Labour

Gordon Brown, kiongozi wa chama cha Labour akiwa na mkewe Bi Sara.
Image caption Gordon Brown, kiongozi wa chama cha Labour akiwa na mkewe Bi Sara. Bw Brown anakabiliwa na upinzani mkali kutoka kwa David Cameron na Nick Clegg.

Kitovu cha chama cha Leba ni vuguvugu la vyama vya wafanyikazi mnamo mwanzo wa karne ya 20, yaani mwaka wa 1900. Lengo la Leba lilikuwa kutetea haki za wafanyikazi.

Leba kilionja madaraka wakati baadhi ya viongozi wake waliteuliwa kuwa mawaziri katika serikali ya kitaifa iliyoundwa wakati wa vita vya kwanza vya dunia. Baada ya vita hivyo, Leba kiliendelea kufanya vyema kama chama cha upinzani. Mara mbili, kiliingia madarakani lakini kwa muda mfupi. Mustakabali wa chama cha Leba ulibadilika zaidi baada ya vita vya pili vya dunia. Serikali ya mseto ilipoundwa mnamo mwaka 1940, kiongozi wa Leba, Clement Attlee aliteuliwa kuwa makamu wa Waziri Mkuu Winston Churchill. Wakati wa uchaguzi wa 1945, Leba kilinyakua ushindi mkubwa zaidi na ambao uliwashangaza wengi na hata wafuasi wake. Ulikuwa wakati huo, baada ya vita vya pili vya dunia, ambapo mfumo wa kulipa mafao kwa raia pamoja na kutaifishwa kwa viwanda kama vile vya mkaa, chuma na reli ulizinduliwa.

Upinzani

Lakini miaka sita baadaye Leba kilitimuliwa madarakani na chama cha Conservative ambacho kilitawala kwa miaka 13, yenye ufanisi. Leba kikiongozwa na Harold Wilson, kilirejea kwa kishindo mnamo miaka ya 1960. Hata hivyo utawala wa Leba ulikumbwa na matatizo mengi ya kiuchumi hali ambayo iliilazimu serikali kupunguza thamani ya sarafu ya Pauni. Mwaka 1970, mazingira yalikuwa tayari kukirejesha Conservative madarakani. Miaka minne baadaye, mambo yalibadilika na Leba kikachukua uongozi ambao ulizongwa na matatizo. Harold Wilson alijiuzulu kama kiongozi wa chama. Jim Callaghan alimrithi kama waziri mkuu lakini ulikuwa wakati wa msukosuko wa kiuchumi ambao ulihitaji kiwango kikubwa cha mkopo pamoja na kupunguzwa kwa matumizi ya fedha za kutoa huduma za umma. Mambo yaliendelea kuzorota kutokana na msururu wa migomo ya wafanyikazi. Ulikuwa msimu wa baridi wenye kisirani. Ilipofika mwaka 1979, chama cha Leba kilitupwa nje na Margaret Thatcher akaingia madarakani. Kwa miaka 18, Leba kilisalia kwenye kipindi kigumu cha upinzani. Kilibadilishabadilisha viongozi, kutoka kwa Michael Foot mwenye mrengo wa kushoto hadi kwa Neil Kinnock ambaye alikuja na ajenda ya kukibadilisha chama kuwa cha kisasa. Neil Kinnock alishindwa kukirejesha Leba madarakani. Kisha akaingia John Smith ambaye aliheshimika sana bungeni na wengi walimwona kama mtu aliyestahili kuwa waziri mkuu.

Lakini Smith aliaga dunia ghafla mnamo mwaka 1994. Kifo chake kilikuwa pigo kubwa kwa chama cha Leba.

Ushindi wa kishindo

Tony Blair alichaguliwa kukiongoza Leba na kuendeleza mabadiliko ambayo Neil Kinnock alikuwa amezindua. Huku kikipewa jina la Leba Mpya au New Labour, chama hicho kiliasi sera za zaman kama zile za utaifishaji. Wakati uchaguzi wa 1997 ulipowadia, wengi walikuwa wamechoshwa na utawala wa Conservative ambacho kilifanyiwa kejeli kama chama chenye uchafu. Leba kilipata ushindi mkubwa na Tony Blair akachaguliwa kuwa waziri mkuu. Leba kiliahidi kuibadilisha Uingereza kuwa nchi ya kisasa na kujenga jamii yenye usawa. Tony Blair alitoa msimamo mkali kuhusu ushirikiano kati ya Leba na vyama vya wafanyikazi huku akisema serikali yake haitavipendelea vyama hivyo. Chama cha Leba kilishinda uchaguzi uliofuata kwa vipindi vingine viwili. Lakini umaarufu wake ulianza kudorora kufuatia hatua ya serikali ya Leba ya kuunga mkono vita vya Iraq.

Mwanzo mpya

Mtiririko wa matatizo dhidi ya serikali ya Leba ulikuwa umeanza: Kushindwa katika uchaguzi mdogo, utoaji hongo ili kutunukiwa taji la kuwa lodi, mzozo kuhusu miradi kama vile ya kutoa vitambulisho na nyongeza ya siku za kumshikilia mshukiwa rumande kwa hadi siku 90. Kwa upande wake chama cha Conservative kilimpata kiongozi chipukizi, David Cameron. Blair aliamua kujiuzulu mwezi Juni mwaka 2007 na Gordon Brown akachukuwa wadhifa huo bila ushindani. Wengi walidhani kwamba Waziri Mkuu Brown angetumia wakati huo ambapo sifa zake zilikuwa bado zinapaa, kuandaa uchaguzi mapema. Bw Brown alikataa. Chama cha Leba kikashindwa vibaya mno katika uchaguzi wa serikali za mitaa. Baada ya miaka ya ufanisi, uchumi ulipigwa na dhoruba ya mdororo wa kiuchumi. Brown alijivunia jinsi alivyochukua hatua mwafaka na kwa dharura kuokoa uchumi wa Uingereza na pia Ulaya. Katika hatua ambayo iliwashutua wengi, Bw Brown alimwalika hasimu wake wa kisiasa katika Leba, Peter Mandelson kurejea serikalini. Huku Mandelson alibisha hodi, baadhi ya mawaziri wa Leba kama vile James purnell, Charles Clarke, Geoff Hoon na Patricia Hewitt walikuwa wanaiasi serikali huku wakimlaumu Waziri Mkuu Brown kwa kuwa mzigo kwa chama cha Leba. Kufichuliwa kwa kashfa ya wabunge kutumia vibaya mfumo wa marupurupu ulikichafulia sifa chama cha Leba. Kashfa hiyo iliviathiri vyama vyote lakini Conservatives walinyoosha kidole kwa serikali ya Leba kwa kudumisha mfumo huo. Huenda Leba kina hofu kwamba kashfa hizo zitawafanya wapigaji kura kukimbilia chama tofauti. Labda kile kitakachowapa moyo ni kujikumbusha mwaka wa 1992 wakati waliposhindwa kwenye uchaguzi na John Major licha ya uchumi kukumbwa na msukosuko.