Chama cha Liberal Democrats

Nick Clegg, kiongozi wa chama cha Liberal Democrats.
Image caption Nick Clegg, kiongozi wa chama cha Liberal Democrats, amepata umaarufu mkubwa kutokana na kujieleza vizuri katika midahalo ya wagombea.

Chama cha Liberal Democrats kina historia ndefu katika siasa za Uingereza. Kilizinduliwa mnamo karne ya 19, wakati huo kikiitwa Liberal Party. Miaka nenda rundi kimeshuhudia mengi mazuri na mabaya huku siasa za Uingereza zikizongwa na migawanyiko ya mara kwa mara.

Chama hicho kiliongozwa na falsafa ya kudumisha haki za mtu binafsi na uhuru wake wa kuchagua. Maadili haya ndiyo msingi wa mfumo wa kisasa wa siasa ambao unatoa mwongozo katika jitihada za serikali za kutoa nafasi sawa kwa raia wake, kumaliza umaskini na ubaguzi. Baada ya chama hicho cha Liberal kuundwa na kufuatia uchaguzi wa 1868, William Gladstone aliunda serikali huku chama chake kikidhibiti bunge la Uingereza.

Mpasuko

Chama hicho kilikumbwa na mpasuko mnamo mwaka wa 1886 juu ya utawala wa ndani wa Ireland. Hata hivyo, mpasuko huo haukukizuia kwendelea kupambana na chama Conservative kung’ang’ania madaraka hadi wakati wa vita vya kwanza vya dunia. Migawanyiko katika chama cha Liberal iliendelea, hali ambayo iliikitia nguvu chama cha Leba ambacho kilikuwa chama rasmi cha upinzani. Umaarufu wa Liberal uliendelea kupwaya. Idadi ya wapigaji kura wake walididimia kiasi kwamba mnamo miaka ya hamsini chama hicho kingeweza kuvutia asilimia 2.5 peke yake ya wapigaji kura. Huku unyonge ukiwa umekibana, kulikuwa na gumzo kwamba kingeungana na chama cha wahafidhina, yaani Conservative. Lakini chini ya uongozi wa Jo Grimond, chama cha Liberal kilibadilisha mkondo wa siasa zake. Kilirejea mashinani kujijenga upya na kuyapigia debe maswala ya kijamii na kutumia mbinu zake za kuendeleza siasa za mtaani. Liberal kilianza kushinda viti vya mabaraza huku wanaharakati wake wakijenga ngome katika miji kama vile Liverpool. Umaarufu huu katika serikali za mitaani ulifufua matumaini ya Liberal kulenga uongozi wa kitaifa. Wakati wa uchaguzi mkuu wa 1974 chama cha Conservative kilikosa kupata ushindi wa moja kwa moja, hali ambayo ilikilazimisha kuomba ushirikiano wa chama cha Liberal licha ya kuwa na viti vichache mno bungeni. Kiongozi wa Liberal, Jeremy Thorpe alitupilia mbali ombi hilo. Badala yake chama cha Leba kilichukuwa mamlaka hali ambayo ilikipatia Liberal nafasi ya kushiriki katika serikali. Bw Thorpe alilazimika kujiuzulu baada ya kuhusishwa na kashfa ya kushiriki mapenzi ya jinsia moja na mwana fashoni wa kiume, Norman Scott. Isitoshe, Thorpe alishutumiwa kwa kujaribu kumuua Scott. Madai hayo ya kuhusika katika njama za kuua, yalitupiliwa mbali. Lakini, nyota ya Thorpe katika siasa ilizima daima. Itakumbukwa kwamba wakati wa uongozi wa Bwana Thorpe, idadi ya wapigaji kura wake iliongezeka kutoka milioni mbili hadi sita ambayo ilikuwa takriban asilimia 20 ya kura zote. Umaarufu huo ulimpa nguvu kiongozi mpya David Steel ambaye alidumisha ushirikiano wa chama cha Liberal na cha Leba, na kwa pamoja vyama hivyo viliunga mkono uongozi wa Waziri Mkuu Jim Callaghan wa Leba.

Mageuzi

Lakini mambo yalibadilika wakati chama cha Leba kilishindwa katika uchaguzi wa 1979. Wanasiasa wanne au ‘genge la wanne’ waliohudumu kama mawaziri katika serikali ya Leba walikiasi chama hicho na kuunda kile kilichoitwa, Social Democratic Party. Mara moja Liberal kikaungana na SDP na kwa pamoja vyama hivyo vilinyakua asilimia 25 ya kura zote zilizopigwa wakati wa uchaguzi wa 1983. Mwaka wa 1988 chama cha Liberal na cha SDP viliungana kirasmi na kubadilisha jina kuwa Liberal Democrats. Chini ya uongozi wa Paddy Ashdown, Liberal Democrats kilipania kujinadi kama chama chenye umaarufu na chenye sera zenye uwezo wa kuleta mabadiliko makubwa. Liberal Democrats kiliendelea kujenga mvuto wake mnamo miaka ya 1990 na miaka saba baadaye kikanyakua nafasi ya pili kama chama chenye umaarufu mkubwa kwenye serikali za mitaa. Kilidhibiti mabaraza 55. Kiliahidi kuongeza senti moja tu kwenye kodi ya mapato ili kugharamia elimu na pia kikatilia mkazo maswala ya mazingira. Chini ya Bwana Ashdown, Liberal Democrats waliendelea kushirikiana na serikali ya Leba katika maswala kama vile ugatuzi wa madaraka. Hata hivyo, wakati Charles Kennedy aliporithi utawala wa Liberal Democrats, ushirikiano wao na chama cha Leba ulianza kuyumbayumba. Liberal Democrats walitamaushwa na kushindwa kwa Leba wa kubadilisha mfumo wa upigaji kura, swala ambalo lilipewa uzito na chama cha Liberal Democrats.

Vita vya Iraq

Chama hicho pia kiliungama na hisia na umma dhidi ya vita vya Iraq. Wakati wa uchaguzi wa 2001, Liberal Democrats walishinda viti 52 na kuongeza 10 zaidi wakti wa uchaguzi wa 2005. Kilikipokonya chama cha Leba vita 12. Kiongozi wake, Charles Kennedy alikitaja kuwa chama cha siku za usoni. Lakini miezi michache baada ya matamshi hayo alijikuta kwenye minong’ono kutokana na uraibu wake wa kunywa pombe. Mrithi wake, Sir Menzies Campbell akiwa na umri wa miaka 66 hakutawala chama hicho kwa muda mrefu. Alikosolewa kwa kuwa mzee sana kukiongoza chama. Sir Menzies aling’atuka na kwa kipindi kifupi, msemaji wa chama hicho wa maswala ya fedha, Vince Cable alishikilia wadhifa wa uongozi. Taji hilo lilikuwa likimsubiri Nick Clegg ambaye alimshinda kwa kura chache zaidi Chris Huhne. Huku Uingereza ikielekea kwenye uchaguzi mkuu, wengi wanahisi huenda hakuna chama kati ya Leba na kile cha Conservative ambacho kitapata ushindi wa moja kwa moja. Hapo ndipo umuhimu wa Liberal Democrats utakapozingatiwa. Hali hiyo ikitokea, chama cha Liberal Democrats kitaunga nani mkono? Leba au Conservative. Ni swala au swali ambalo Nick Clegg hatothubutu kulijibu kwa sasa lau atakosolewa na wapigaji kura.