Maelezo mafupi kuhusu Nick Clegg

Nick Clegg, kiongozi wa chama cha Liberal Democrats
Image caption Nick Clegg, kiongozi wa chama cha Liberal Democrats anachuana vikali na waliomtangulia Gordon Brown na David Cameron.

Nick Clegg hupenda kujitambulisha kama mwanasiasa wa kisasa zaidi.

Baada ya kujiuzulu kwa wanasiasa Charles Kennedy kutokana na tatizo la ulevi na Sir Menzies Cambbell kutokana na utata juu ya umri wake mwishoni mwa mwaka 2007- Chama cha Liberal Democrats kilihitaji sasa mtu tofauti wa kukiongoza.

Aliyepatikana kukamata nafasi hiyo ya uongozi ni bwana Clegg ambaye hakika hakuwa akijulikana sana nje ya Westminster.

Akiwa na umri wa miaka 43, mwenye mvuto katika runinga, na baba wa watoto watatu mwenye uwezo wa kuzungumza lugha kadhaa, ndiye kiongozi kijana kabisa na wa ‘kisasa’ katika safu ya uongozi wa juu wa Liberal Democrats.

Bw Clegg huenda akawa ndiye kiongozi wa kwanza wa juu kabisa Uingereza kukiri hadharani kuhusu mwenendo wake katika suala la ngono ambapo alikiri kuwahi kulala na wanawake wasiozidi 30.

Pia wakati wanasiasa wengi hawapendi kuweka hadharani imani zao za kiroho, Bw Clegg alisema wazi kabisa kuwa si muumini imara wa kiroho. Hakuishia hapo tu katika kuweka mambo hadharani, akasema pia wakati akiwa na umri wa miaka 16 jijini Munich Ujerumani aliwahi kupewa kifungo cha kutumikia jamiii baada ya kuchoma moto maua ya jamii ya cacti, ambayo hupatikana kwa uchache.

Bw Clegg ni mume wa mwanamama mwanasheria wa kibiashara Miriam Gonzalez Durantez. Anasema miongoni mwa rafiki zake maarufu ni pamoja na mtangazaji wa runinga, Louis Theroux, na mwongozaji filamu Sam Mendez. Mwaka jana alipozaliwa mwanae wa kiume Bw Clegg alichukua likizo ya uzazi.

Wapo watu wanaomwona Clegg kama mwanasiasa wa kisasa, lakini mwenye uzoefu mdogo wa hali halisi ya mambo duniani.

Masuala ya kifamilia

Bw Clegg baada ya kubahatika kusoma katika shule maalumu ya Westminster, chuo kikuu cha Cambridge na vyuo kadhaa Marekani na Ubelgiji, alifanya kazi kama mhadhiri na mwandishi wa habari.

Baada ya hapo alifanya kazi Tume ya Ulaya, akisimamia miradi ya misaada na mazungumzo ya kibiashara.

Akiwa ndani ya Tume ya Ulaya, aliwahi kushawishiwa na Makamu Mwenyekiti wa Tume hiyo Bw Leon Brittan, ili ajiunge na chama cha Conservative, lakini alikataa.

Badala yake Clegg, akachagua chama cha Liberal Democrats, ambapo mwaka 1999, alichaguliwa kuwa mwanachama wa Bunge la Ulaya akiwakilisha eneo la East Midlands.

Baada ya miaka mitano akaachia ngazi, akidai kazi ile ilikuwa ikiingiliana na majukumu yake ya kulea familia yake changa.

Haikuchukua muda mrefu Bw Clegg akachaguliwa kuwa mbunge wa jimbo la Sheffield Hallam mwaka 2005. Hapo akaanza kutajwa kama mtu anayefaa kukiongoza chama kwa miaka ijayo.

Mwaka 2005, Bw Clegg, akiwa msemaji wa chama wa masuala ya Ulaya, hakujitokeza kugombea wakati Charles Kennedy alipoacha uongozi wake wa chama cha Liberal Democrat.

Badala yake, akaamua kumuunga mkono wake katika ofisi ya ya mambo ya nje, Sir Menzies Campbell, kwa makubaliano ya kushirikiana pamoja katika harakati za kisiasa.

Baada ya Sir Menzies kushinda uchaguzi, akamteua Clegg kuwa msemaji wa masuala ya ndani ya nchi; hali iliyoimarisha heshima yake pale aliposhindana na mawaziri juu ya masuala ya vitambulisho na mikakati ya kukabiliana na ugaidi.

Wakati Sir Menzies alipojiuzulu nafasi yake ya uongozi wa chama mwaka 2007 kutokana na madai kuwa umri wake ulikuwa umemtupa mkono kwa nafasi hiyo, Bw Clegg akajitokeza kuwa mtu aliyepewa nafasi kubwa ya kurithi uongozi.

Katika uchaguzi uliofuata bwana Clegg akamshinda mpinzani wake bwana Chris Huhne, kwa tofauti ya kura 511 na kukamata kiti cha uongozi wa chama cha Liberal Democrats.

Baada ya hapo Clegg amekuwa akifanya jitihada za kurekebisha sera ya kushughulikia mporomoko wa kiuchumi na kukua kwa nakisi katika bajeti. Chama kimeweka vipaumbele kama vile kuongeza huduma bure kwa watoto na wazee na kuondoa ada katika elimu ya juu.

Bw Clegg mwaka jana, katika mkutano wa chama chake, aliwakasirisha baadhi ya wenzake ndani ya chama akiwemo aliyemtangulia, Bw Charles Kennedy, pale aliposema kuwa punguzo kali katika bajeti ya matumizi lingehitajika.

Mvuto wa kisiasa

Pengine mvuto wake katika duru za kisiasa ulionekana pia pale alipomuunga mkono mwigizaji Joanna Lumley katika harakati zake za kufanikisha wanajeshi kutoka Nepal wajulikanao kama Ghurka wapate haki ya kuishi Uingereza, hasa kwa kuwa waliisaidia nchi hiyo katika vita mbali mbali.

Vile vile katika mkutano wa viongozi wa chama alitoa wito kwa spika wa bunge la dogo la Uingereza, Bw Michael Martin kujiuzulu kwa madai ya kushindwa kushughulikia vyema suala la mgogoro wa gharama za matumizi ya wabunge.

Hivyo basi yote hayo ukiongezea na namna alivyojipanga katika midahalo ya wagombea wa nafasi ya Waziri Mkuu huenda ikamsaidia katika kufikisha ujumbe kwa wananchi wa Uingereza ili wamchague yeye.