Shinikizo huongeza maradhi kwa wanawake.

Moyo wa binadamu
Image caption Moyo wa binadamu

Shinikizo za kazi huongeza uwezekano wa maradhi ya moyo kwa wanawake walio chini ya umri wa miaka 50, kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na wauguzi elfu kumi na wawili.

Utafiti uliofanywa na taasisi moja ya huko Denmark kuhusu matibabu ya wafanyakazi na katika mazingira umebaini kwamba wanawake walio chini ya umri wa miaka hamsini hawapati madhara sawa na wanawake waliozidi umri huo.Utafiti huo unapendekeza kuwa kuna sababu nyingine zinazochangia maradhi ya moyo miongoni mwa wanawake wenye umri mkubwa.

Kuna ushahidi mwingi unaothibitisha kuwa shinikizo zinazotokea kazini huongezea uwezekano wa maradhi ya moyo kwa wanaume, ingawa hapakuwa na utafiti kuhusu athari zinazowapata wanawake.

Katika utafiti huu wataalamu waliwahoji zaidi ya wauguzi 12,000 walio kati ya umri wa miaka 45 na 64 kuhusu shinikizo zinazowakabili wanapokuwa kazini na kuwafuatilia kwa kipindi cha miaka 15 hadi mwaka 2008.

Kufikia mwaka huo wauguzi 580 tayari walikuwa wameshalazwa hospitalini kwa magonjwa yanayohusiana na moyo, huku 369 wakikabiliwa na mshituko wa moyo pamoja na maumivu ya viungo yanayosababishwa na mapigo ya moyo.

Wataalamu hao waligundua kuwa pamoja na kuzingatia masuala ya uvutaji sigara na kisukari, watu walioelezea shinikizo katika kazi zao kuwa juu walikuwa na uwezekano wa asilimia 35 ya kupatikana na maradhi ya moyo kuliko wale waliojihisi hawana shinikizo kazini.

Lakini walipochuja matokeo ya utafiti kulingana na umri, walipata kuwa ni wanawake wenye umri mdogo chini ya miaka 50 walioathirika kwa kiwango kikubwa.

Wataalamu hao kutoka chuo kikuu cha Glostrup nchini Denmark wanasema kuwa athari za shinikizo kazini zina athari kubwa kwa wanawake wenye umri mdogo.