Mafuvu ya Waherero yarejea

Ramani ya Namibia
Image caption Ujerumani ilitawala 1884 -1915

Maelfu ya raia wa Namibia hususan kutoka makabila ya wa Herero na wa Nama mapema siku ya jumanne wameandamana kupokea mafuvu 20 ya wenzao yaliyokuwa yakishikiliwa nchini Ujerumani kwa zaidi ya miaka mia moja.

Takriban watu 4,000 walijitokeza kwenye uwanja wa ndege wa Windhoek ambako ndege iliyobeba mafuvu hayo ilitua alfajiri. Wengi wao walibeba mabango yende maandiko 'tunawakaribisha babu zetu, mashujaa wetu'.

Mwishoni mwa uwanja wa ndege, masanduku mawili yaliyofunikwa bendera ya Namibia yalishushwa kutoka kwenye ndege ya jeshi la Namibia, yakibebwa na wanajeshi na kutumbuizwa kwa heshima ya tarumbeta la kijeshi.

Chanzo cha vifo vya watu hawa kilitokea mnamo miongo ya 1880 Ujerumani ilipoiteka ardhi ambayo hii leo linajulikana kama Taifa la Namibia, na kulipa jina South West Africa.

Haki miliki ya picha BBC World Service
Image caption Mafuvu ya Waherero na Wanama

Mnamo mwaka 1904 kabila la wa Herero, ambalo ni kubwa miongoni mwa makabila 200, lilizusha upinzani dhidi ya utawala wa kikoloni na kuua takriban Wajerumani 120.

Wajerumani walijibu kitendo hicho kwa ukatili usio na kifani. Generali Lothar von Trotha alitia saini amri ya kuwafyeka watu wa kabila la Herero, akiwashinda katika mapigano na kuwalazimisha kukimbilia jangwani ambako wengi waliuawa kwa ukosefu wa maji ya kunywa.

Kati ya idadi ya jumla ya wa Herero 65,000 Herero, ni 15,000 walionusurika. Inasadikiwa kuwa pamoja na hao kuna takriban watu 10,000 wa kabila la Nama waliouawa.

Mnamo mwaka 1985, Ripoti ya Umoja wa Mataifa ilitaja tukio hilo kama njama ya kujaribu kuwateketeza wa Herero na wa Nama wa Namibia ya leo na kwa hiyo kuyaita mauwaji ya kimbari ya karne ya 20.

Mnamo mwaka 2004, balozi wa Ujerumani nchini Namibia akaonyesha masikitiko juu ya tukio hilo.

Mafuvu yaliyowasili Namibia ni miongoni mwa watu 300 waliohamishiwa Ujerumani baada ya mauwaji ya kimbari wakati wa utawala wa Mjerumani kati ya mwaka 1884 na 1915.

Waherero walichukizwa na wahamiaji kuiba ardhi yao, mifugo na wanawake ndio wakaona bora wakabili uchokozi huo na mnamo mwezi januari mwaka 1904 wapiganaji wao wakaua raia wajerumani 123 katika mashambulizi ya siku kadhaa. Wenzao kutoka kabila la Nama nao wakajiunga nao mnamo mwaka 1905.

Chini ya amri ya General Lothar von Trotha Waherero walizingirwa ndani ya jela pamoja na Wanama na kuachwa humo bila chakula wala maji. Wengi wao walikatwa vichwa baada ya kufariki na mafuvu yao kutumwa kwa wataalamu wa Kijerumani mjini Berlin ili vifanyiwe uchunguzi wa kisayansi''.

Mafuvu yaliyowasili Namibia leo ni ya wanawake wanne, wanaume 15 na mvulana mmoja.

'uhusiano wa utawala wa Ki-Nazi'

Msemaji wa shirika lisilo la kiserikali 'charite' Claudia Peter amesema madai ya ukaguzi wa mafuvu hayo na wataalamu wa Kijerumani yalikuwa na lengo la kuthibitisha dhana ya kikabila kwamba thamani ya watu wenye rangi nyeusi haiwezi ikalinganishwa na ya mtu mweupe na hilo lilichangia katika fikra na sera ya utawala wa Nazi.