Kenya yapanga kuuteka mji wa Kismayu

Haki miliki ya picha internet
Image caption Majeshi ya Kenya nchini Somalia

Baada ya mashambulizi ya juma moja sasa wanajeshi wa Kenya wamefika kusini mwa Somalia karibu na eneo la Afmadoow , mji ulioko eneo la Juba.

Wanajeshi wa kenya kwa wakati huu wako viungani mwa mjuu wa Afmadoow wakijitayarisha kufanya mashambulizi kuuteka mji huu ambao ni muhimu sana kwa Mji wa Kismayu

Afmadoow ni maarufu sana kwa biashara ya magendo kutoka Kenya na unamilikiwa na wapiganaji wa Al Shabaab.

Kwa muujibu wa msemaji wa Jeshi la Kenya Meja Emmanuel Chirchir ,itakuwa rahisi kuuteka mji wa Kismayu baada ya kutia mkononi Afmadoow.

Wanajeshi wa Kenya wamepania kuuteka mji wa Kismayu kwa sababu hii ni ngome kuu ya wapiganaji wa Al Shabaab.

Na kama njia mojawapo ya kuwatawanya wapiganaji hao wa Al shabaab na kupunguza uwezo wao wa kivita , mwishoni mwa juma ndege za kivita zilishambulia mji huo kwa mabomu.

Hata hivyo haijabainika mashambulizi hayo ya angani yalitekelezwa na nani.

Lakini balozi wa marekani nchini Kenya Scot Gration amesema kuwa marekani inaunga mkono hatua ya Kenya kuivaimia Somalia kwa lengo la kuwafyeka Al Shabaab.

Hata hivyo taarifa ya Rais Sheikh Sharif inayoshutumu Kenya kwa kuivamia Somalia kijeshi inatarajiwa kuleta tumbo joto kati ya Nairobi na Mogadishi.

Lakini wachanganuzi wa maswala ya kidiplomasia na kivita wanasema kuwa hii huenda imetokana na pendekezo la Kenya la kuundwa kwa halmashauri ndani ya Somalia katika eneo la Juba.

Sharif huenda akiawa anahofia kuwa kuwepo kwa halmashuri hii kutampunguzia uwezo wake kiutawala.