Aukata ulimi wa mkewe baada ya ugomvi

Image caption Wanawake wa Afghanistan huvalia Burgha

Mwanamme mmoja amewekwa kizuizini Kaskazini mwa Afghanistan kwa kukata ulimi wa mkewe kufuatia mzozo wa kinyumbani.

Mwanamme huyo kwa jina la Saleh alimshambulia mkewe huyo nyumbani kwao kijiji cha Jangory Jimbo la Balkh.

Maafisa wa polisi wamesema muathiriwa huyo wa miaka 20 alikuwa na mimba ya miezi saba iliyotoka kufuatia ukatili huo.

Madaktari wameweza kuushona na kuurudisha kama ulivyokuwa ulimwi wa mwanamke huyo, japo haijulikani ikiwa ataweza kuzungumza tena.

Kwa sasa bibi huyo anashughulikiwa katika kituo maalum cha wanawake ambapo alijitokeza mbele ya waandishi wa habari akiandamana na mamake na maafisa wa polisi.

Mwandishi wa BBC eneo la Balkh Waheed Massoud amesema mama huyo alionekana kufadhaika kiasi cha kushindwa kuongea. Mamake muathiriwa amesema mkwewe huyo kwa jina Saleh amekuwa akimdhulumu mwanawe siku zote wameishi pamoja katika ndoa ya mwaka mmoja.

"Alisha teketeza chumba chake cha kulala, na kumshambulia kila mara. Kila mara wakienda kwa wazee wanasema ni mambo ya mke na mme", Alisema mama muathirika kwa waandishi wa habari. Aliongeza baada ya mkwewe kuukata ulimi wa mwanawe hapo akaamua kuwasilisha malalamishi kwa polisi.

Shambulio hili katika kijiji cha Jangory inatoa taswira ya ukatili wa manyumbani Afghanistan. Mapema mwezi huu wakwe wa binti wa miaka 15 Sahar Gul mkoa wa Baghlan walihukumiwa jela miaka 10 kwa kumtesa mkaza mwanao alipokataa kufanya ukahaba.

Wiki mbili zilizopita wasichana wawili kati ya miaka 10 na 13 waijinyonga baada ya kupatikana wakiwa na mavazi ya kiume kuwawezesha kuzuru kijiji cha karibu.

Katika baadhi ya maeneo ya Afghanistan wanawake hawaruhusiwi kutembea peke yao au kuondoka nyumbani bila idhini. Wasichana hao wanadaiwa kusombwa na mafadhaiko baada ya jamaa zao kuwakemea kwa kuletea familia zao aibu.

Licha ya katiba ya sasa nchini Afghanistan kutoa usawa wa jinsia Umoja wa Mataifa unasema wanawake wengi wameendelea kuathirika na ukatili wa nyumbani.

Makundi ya kutetea haki za wanawake yamelalamikia hatua ya kuwajumuisha waakilishi wa Taleban katika uwongozi yakisema hali ya wanawake huenda ikazorota zaidi.

Aidha Shirika la kitaifa la Wanawake limeelezea wasi wasi kuhusu hatima ya wanawake baada ya wanajeshi wa NATO kuondoka nchini humo mwaka wa 2014.

Shirika hilo limeomba serikali kuimarisha usalama miongoni mwa wasichana wadogo baada ya kuwepo na visa vya kupatiwa sumu na watu wanaoshukiwa kuwa kundi la Taleban.