Maisha ya Aung Suu Kyi Uingereza

Suu Kyi katika jumba la shirika la BBC Haki miliki ya picha AFP

Aung San Suu Kyi anarejea tena Uingereza miaka 24 tangu kurudi Burma ambapo alianzisha harakati za kushinikiza mageuzi ya kidemokrasia. Mwandishi wa BBC wa masuala ya dunia Mike Woolridge ameandaa makala haya yakiangazia maisha ya mwanasiasa huyu nchini Uingereza ambapo alipata masomo yake na pia ndoa yake.

Aung San Suu Kyi anasema ziara yake hii ambayo ni ya kwanza kwa robo karne Uingereza ni muhimu sana akiwa na matumaini ya kukutana na marafiki wa zamani na kutembelea maeneo aliyohafahamu. Anasema angependa sana ziara hii isilete kumbukumbu ambazo huenda zikamfanya kuwa na huzuni.

Lakini haitakuwa rahisi kwa mwanaharakati huyu ambaye ni mshindi wa tuzo ya amani ya Nobel kuepuka huzuni wakati akitafakari maisha yake nchini Uingereza ambapo aliishi pamoja marehemu mumewe,Michael Aris. Bw Aris alifariki dunia mwaka 1999 baada ya kuugua maradhi ya saratani huku mkewe akiwa yuko nyumbani Burma.

Marehemu alinyimwa visa kusafiri Burma kwa miaka mingi japo watawala wa kijeshi walimuarifu Suu Kyi kwamba mumewe alikua anaugua na kumuarifu alikuwa huru kumtembelea kabla ya kifo chake. Hata hivyo alihofia kuzuiwa kurudi nyumbani na hivyo kumlazimu kuishi uhamishoni.

Kwa upande wake, Michael Aris alielewa majukumu ya mkewe katika kusaidia raia wa Burma. Suu Kyi aliwahi kumuandikia waraka kwamba endapo angetakiwa kutumikia nchi na raia wake basi angemkubalia kuwahudumia.

Uwamuzi wa kurudi Burma nwaka wa 1988 uliimaanisha kutengana na familia yake, mumewe na watoto wawili wa kiume, Alexander na Kim ambao walimtembelea mara kadhaa mjini Rangoon.

Sababu kubwa ya mwanaharakati huyo kurejea nyumbani ni kumhudumia mamake aliyekuwa anaugua lakini akiwa nyumbani akajipata katika harakati za kushinikiza mageuzi ya kidemokrasia na vuguvugu la mageuzi lilimuomba awe kiongozi wake.

Bi Suu Kyi alipata masomo yake ya sekondari nchini India mwaka baada ya mamake kuteuliwa kama balozi wa Burma nchini humo. Baada ya kukamilisha masomo yake mjini Delhi aliekea Uingereza kusomea shahada ya Uchumi, Filosofia, na Siasa katika chuo cha St Hugh's ,Oxford.

Bi Suu Kyi alikutana na Michael Aris msomi wa utamaduni wa Tibetan kupitia rafiki na kisha uhusiano wao ukawa wa karibu walipokaa mjini New York.

Harusi yao alifanyika Uingereza katika makaazi ya mlezi wa Suu Kyi Lady Gore-Booth chini ya imani ya Budhha.

Maharusi hao walianza maisha ya ndoa eneo la Oxford ambapo familia yao ilikuwa ya kawaida. Marafiki zake wanamtaja kama mama mtulivu aliyewalea wanawe kwa maadili na kumheshimu mumewe.

Na wakati, Aung San Suu Kyi akirejea nchi ambayo aliishi maisha kama mzazi na mke, ukweli ni kwamba daima Burma ndio kipau mbele chake siku zote.