Je Kenya inaweza kujizuia na umwagikaji damu?

Imebadilishwa: 19 Oktoba, 2012 - Saa 06:26 GMT

Ghasia za baada ya uchaguzi nchini Kenya.

Zaidi ya watu 1,000 waliuawa katika ghasia za baada ya uchaguzi mkuu mwaka 2007 na kuna wasiwasi na hofu kuhusu vitendo vibaya zaidi vya kutia hofu huku Kenya ikielekea kwenye uchaguzi mkuu kwa mara nyingine.

Miaka minne baada ya mzozo mbaya zaidi kuhusu uchaguzi kuwahi kutokea tangu Kenya kujipatia uhuru mwaka 1963, taharuki imetanda kabla ya uchaguzi kuu.

Mwandishi na mwanahabari nchini Kenya Gray Phombeah anaamini kuwa Kenya inajiandaa kwa umwagikaji damu wakati uchaguzi ukikaribia.

Katika kile baadhi wanaona kama hali inayorejesha tasiwra au picha za ghasia zilizotokea nchini humo baada ya uchaguzi wa mwaka 2007 na 2008, ghasia za kikabila , mauaji na matamshi ya chuki vimeongezeka.

Matukio haya ni onyo kuwa nchi hiyo huenda ikatumbukia katika ghasia zilizoshuhudiwa mwaka 2007 kufuatia uchaguzi

Ghasia zilianza kushuhudiwa katika eneo la Tana Delta ambako zaidi ya watu 100 waliuawa mwezi Agosti wakati wa mapigano kati ya jamii za Pokomo ambao sana sana ni wakulima na Orma ambao ni wafugaji . Chanzo cha ghasia kilikua rasilimali za maji na ardhi.

Ghasia za baada ya uchaguzi nchini Kenya 2007

Mnamo mwezi Septemba mauaji ya mhubiri wa kiisilamu mjini Mombasa , yalifuatiwa na ghasia na makabiliano makali kati ya polisi na waandamanaji mjini humo.

Tangu hapo, naibu waziri Ferdinand Waititu amefikishwa mahakamani kwa kosa la matamshi ya chuki na kuchochea ghasia mjini Nairobi.

Ghasia zaidi zimeripotiwa Pwani mwa Kenya na katika eneo la Kaskazini Mashariki mwa nchi.

Ghasia hizi zimesababisha wasiwasi na hofu huku kinyang'anyiro cha uchaguzi kikishika kasi kabla ya uchaguzi wenyewe mwezi Machi mwaka 2013. Mauaji hayo huenda yakafungua ukurasa wa uchaguzi mpya wenye ghasia.

Baada ya uchaguzi wa mwaka 2007 na ghasia zilizofuata, serikali ya muungano iliundwa mwaka 2008 lakini hadi kuundwa kwa serikali hiyo takriban watu 1,000 walipoteza maisha yao huku maelfu wakiachwa bila makao.

Ghasia hizo zilikuwa mbaya sana kiasi kwamba aliyekuwa katibu mkuu wa umoja wa mataifa Kofi Annan kulazimika kuingilia kati kushawishi pande zote kwenye mzozo huo, vyama vya ODM na PNU vya Waziri Mkuu Raila odinga na Rais Mwai Kibaki kufanya mazungumzo na kusitisha ghasia.

Wananchi waliunga mkono mageuzi ya katiba baada ya kura ya maoni kuhusu katiba mpya kupata kura ya ndio na kushinda. Wengi walitaka utawala wa majimbo na kuwepo sheria kuhusu haki za watu.

Kiongozi wa kundi la MRC linalotaka kujitenga kwa Pwani mwa Kenya, Omar Mwamnuadzi

Lakini kabla ya juhudi za kuunda jopo maalum kusikiliza kesi za washukiwa wa ghasia za baada ya uchaguzi zilizuiwa na wanasiasa, hasa wale waliohusishwa na ghasia za baada ya chaguzi .

Huku ripoti maalum zikiwa zingali kuchapishwa, wakenya wengi bado hawajasahau matuko ya mwaka 2007.

Pia kulikua na juhudi za kuleta mageuzi kuhusu sera ya ardhi, mageuzi katika idara ya polis, na sheria ya uongozi bora.

Mabadiliko mengine ambayo yalihitajiwa kufanywa hasa baada ya uchaguzi uliokumbwa na utata yamepuuzwa.

Mdahalo mkubwa sasa ni kuhusu wanasiasa wawili ambao wanasubiri kufika mbele ya ,mahakama ya ICC wiki chache tu baada ya uchaguzi wa mwaka ujao, kwa tuhuma za kuchochea ghasia za baada ya uchaguzi mkuu 2007.

Waziri wa zamani wa fedha Uhuru Kenyatta na William Ruto, mwanasiasa mwenye utata sana , wote wanakana kuhusika na ghasia za baada ya uchaguzi na wanagombea urais.

Bwana Ruto anatuhumiwa kwa kuchochea ghasia za baada ya uchaguzi ingawa anatazamwa kama shujaa kaatika jamii yake ya Kalenjin.

Kanyatta naye bila shaka ni mwanawe Rais wa kwanza wa Kenya Jomo Kenyatta.

Kuwepo kwao kwenye kinyang'anyiro cha uchaguzi huu kumezua wasiwasi kuhusu ghasia mpya. Na Kofi Annan mwishoni mwa wiki alionya kuwa nchi iko katika hatari ya kutumbukia kwenye ghasia.

Mizizi ya ukosefu wa usawa

Bila shaka uchaguzi wa Kenya umekuwa ukija na ghasia za kikabila kwani vyama vya kisiasa hutegemea sana uungwaji mkono kutoka kwa makabila yao.

Lakini jambo moja muhimu ni kuwa hakuna usawa katika rasilimali za majimbo. Ni hilo kuliko hata umaskini ndiyo chanzo kikubwa cha ghasia na uhalifu.

Ukosefu wa ajira sasa umewadia asilimia arobaini huku vijana wakiwa wameathirika sana na zaidi kutokana na ukosefu wa ajira. Uhasama wa kikabila ni rahisi kusababisha taharuki.

Mojawapo ya maeneo yaliyoathirika kutokana na ghasia ni Kibera eneo bunge la waziri mkuu Raila Odinga

Wakati huhuo, wanasiasa wanaendelea kujilimbikizia mishahara minono wakati wafanyakazi wa sekta ya umma wakilazimika kugoma wakidai mishahara na mazingira bora ya kazi.

Ukweli ni kwamba maelfu ya wale waliopoteza makao yao kufuatia ghasia za baada a uchaguzi, bado wako katika kambi za muda.

Wakati wa uchaguzi mkuu uliopita, serikali ilisemekana kuhusika na ghasia za kikabila , mapigano kati ya makabila na hasira dhidi ya serikali.

Kama ripoti moja ilivyosema hivi karibuni, Kenya ingali kupona. Bado inauguza majeraha ya uchaguzi uliopita.

Nchi yenye makovu.

Ifikapo mwezi Machi, wakenya watapigia kura magavana na maseneta kwa mara ya kwanza. Ushindani utakuwa mkali katika nyadhifa za utawala wa mikoa na hivyo kuchochea uhasama na hata kusababisha ghasia na vurugu.

Ikiwa na majeraha tele kuhu ikielekea kwenye uchaguzi, Kenya huenda inaonyesha dalili za athari za yale taliyotokea miaka minne iliyopita na hali huenda ikawa mbaya kweli.

Taarifa zinazohusiana

BBC © 2014 Ilani: BBC haihusiki na yaliyoandikwa na tovuti za nje ya BBC.

Ukurasa huu unaonekana vyema kwa kivinjari cha kisasa kikiwa na laha mtindo (CSS).Wakati unaweza kuona yaliyomo katika ukurasa huu kwa kivinjari ulichonacho, hautaweza kufaidi kuona kila kitu vizuri. Tafadhali zingatia uwezekano wa kuboresha progaramu ya kivinjari au kuwezesha laha mtindo (CSS) endapo unaweza kufanya hivyo.