Tazama kipindi cha Sema Kenya Kajiado

Imebadilishwa: 23 Oktoba, 2012 - Saa 12:53 GMT

Mshiriki wa kipindi cha Sema Kenya Kajiado auliza swali.

Jumapili iliyopita, tarehe 21 Oktoba, SemaKenya ilikuwa katika Kaunti ya Kajiado.

Mbunge wa Kajiado ya Kati, Jenerali Joseph Nkaissery na viongozi wengine wa Kaunti hilo walijiunga na jopo letu siku hiyo.

Kaunti ya Kajiado ni eneo linalo tambulika na wengi kama makazi ya jamii ya Wamaasai, ambao tangu jadi wameweza kudumisha mila na desturi zao, tofauti na jamii nyingi nchini Kenya.

Hata hivyo, Wakenya kutoka sehemu mbalimbali wamenunua mashamba katika kaunti hiyo na kuhamia maeneo kama vile Kitengela, Ngong, Rongai, Kiserian na mengineo.

Kaunti hii iko katika mkoa wa bonde laufa, ina maeneo bunge tatu, na inapakana kwa upande mmoja na nchi ya Tanzania.

Lakini mbali na athari zinazotokana na wakaazi wa eneo hili kuendelea kushikilia mila na desturi zao za jadi, je, ni changamoto zipi zingine wanazokabiliana nazo?

Utafiti unaonyesha kuwa viwango vya elimu katika kaunti hii bado viko chini. Kuna shule chache za msingi na zile za upili. Hadi kufikia sasa, ni asilimia 48 ya watoto waliosajiliwa kuingia shuleni. Pamoja na hili idadi ya watu wasiojua kusoma iko juu.

Licha ya kwamba wakaazi wengi ni wafugaji, bado wengi ni maskini. Hii imechangiwa na kuwa na Wamaasai wengi hawajasoma na pia jamii hii kutegemea zaidi ufugaji kama njia pekee ya kujitafutia riziki.

Miundo msingi katika kaunti hii pia iko kwenye hali mbaya, ikilinganishwa na sehemu zingine zaKenya.

Kaunti hii imezungukwa na mbuga ya wanyama pori na hivi karibuni tu wakaazi wa eneo hilo waligonga vichwa vya habari baada ya kuwaua simba wasita. Hii ni ishara tosha kuwa tatizo la mizozo kati ya binadamu na wanyama pori limekithiri.

Taarifa hii imetayarishwa na Wairimu Gitahi, mtafiti wa Sema Kenya.

Taarifa zinazohusiana

BBC © 2014 Ilani: BBC haihusiki na yaliyoandikwa na tovuti za nje ya BBC.

Ukurasa huu unaonekana vyema kwa kivinjari cha kisasa kikiwa na laha mtindo (CSS).Wakati unaweza kuona yaliyomo katika ukurasa huu kwa kivinjari ulichonacho, hautaweza kufaidi kuona kila kitu vizuri. Tafadhali zingatia uwezekano wa kuboresha progaramu ya kivinjari au kuwezesha laha mtindo (CSS) endapo unaweza kufanya hivyo.