Sheng inanajisi Kiswahili

Imebadilishwa: 9 Novemba, 2012 - Saa 15:24 GMT

Logo ya Kiswahili

Sheng inanajisi Kiswahili

Sheng ama lugha simo ni lugha inayotumiwa na watu wa kundi maalum kwa ajili ya kutaka waelewane wao kwa wao na pengine kuwatenga watu wengine. Katika mukhtadha huo ni sawa kusema kuwa ni lugha isiyokuwa na mfumo wa rasmi wa sarufi kwani watu hubuni majina wanavyofikiria.

Majina yanaweza kubuniwa kutoka kwa vipande vya lugha tofauti, kubadilisha maneo kwa mfano kutoka nyuma ukirudi mwanzo na kadhalika. Kwa mfano neno bata unaweza kuwasikia vijana wakenya wakisema taba na kuoga wanasema kugao.

Nimeanza na maelezo hayo kuonyesha namna lugha hiyo inayotajwa kuwa ya kihuni na baadhi ya wasomi wa Kiswahili inatofautiana kutokana na mtu anachosema na mahali anaposemea.

Hata hivyo kwa wataalamu wa isimu jamii ( social linguists) watakupiga mawe ukikashifu matumizi ya sheng. Wengine hata wamefanyia utafiti kipengee hicho.

Ingawa kuna mvutano mkubwa kuhusu matumizi ya sheng ama lugha simo, ni muhimu kutaja kuwa kuna baadhi ya maneno yaliyoanza kama sheng na yakaswahilishwa.

Kwa mfano nchini Kenya, Matatu ni magari ya uchukuzi wa umma ama matwana kwa Kiswahili sanifu. Vivyo hivyo, Tanzania chombo hicho kinaitwa daladala ambalo si jina la Kiswahili sanifu lakini limetiwa katika matumizi.

Hata hivyo kuna hasara kubwa ya kutumia baadhi ya majina ya sheng ambayo yanapotosha maana halisi ya maneno hayo ya Kiswahili.

Kwa mfano nchini Rwanda mtu akiwa hajakamilika kwa namna moja au nyingine watu wanamuita kasorobo. Kwa hakika kasorobo ni neno la Kiswahili kumaanisha kuna upungufu wa robo ya kitu kujalizia mahali fulani kama vile dakika kumi na tano za saa na kadhalika.

Hivyo inapotumika katika mazungumzo inawakanganya waswahili. Si hayo tu, Burundi ndio kuna mambo, eti muasi kwa lugha simo ya huko ni msichana mrembo.

Kwa Kiswahili sanifu muasi ni mwanamgambo ama mtu msumbufu tu asiyeambilika wala kusemezeka.

Kenya na Tanzania ni nchi ambazo zinajulikana pia kuibuka na misimo mbalimbali na inayopotosha maana halisi ya maneno ya Kiswahili. Nchini Tanzania nilimsikia mtangazaji mmoja akisema msichana mrembo anaitwa Mkwaju. Tunavyojua katika Kiswahili mkwaju ni namna moja ya kiboko cha kumchapa mtu. Je sasa twabadilisha jina la mrembo kuwa kiboko? Mambo mawili kando kabisa. Tanzani amtu atakwambia anasikia ubao kumaanisha kuwa anaona njaa. Inavyoeleweka ni kuwa ubao ni sehemu ya mti ama mbao katika Kiswahili sanifu. Na huko Tanzania mtu anapokwambia patachimbika ana maana ya kuwa pameharibika jambo. Utata unaojitokeza hapa ni kuwa patachimbika ni kitenzi cha Kiswahili kumaanisha hali ya pengine kufanya shimo mahali ama kutoboa kitu ilhali kuharibika ni kusambatarika kwa hali ama kitu fulani. Hizo ni dhana mbili tofauti kabisa kama mbingu na ardhi.

Nchini Kenya pia mambo ya sheng yanapigiwa upatu sana hususan na vijana. Hata hivyo ni muhimu kutaja kuwa matumizi ya maneno fulani huvuruga Kiswahili Kabisa. Kwa mfano katika lugha simo Kuro ni kahaba lakini ukweli ni kuwa katika Kiswahili kuro ni mnyama wa porini wa jamii ya paa anyefanana na kulungu. Yaani hapa kosa la kwanza ni kumlinganisha binadamu na mnyama. Pili neno mbuyu Kenya lina maana ya baba lakini katika Kiswahili ni mti unaozaa mibuyu na ikiwekwa semi na iwe "kuzunguka mbuyu" basi inamaanisha kutoa hongo.

Kadhalika neno demu ambalo linatumika Tanzania, Kenya na Jamhuri ya demokrasia ya Congo lina maana ya msichana lakini katika Kiswahili sanifu ni kitambaa kinachofunika mwanamke maziwa anapolima ama tambara hivi. Je unapomwita msichana demu hujui kwa Kiswahili unamlinganisha msichana huyo natambara labda? Je huo ni uungwana? Kenya watu wanasema masa ni mama katika lugha simo lakini katika Kiswahili sanifu masa ni matendo mabaya yanayofanywa na mtu.

Athari nyingine ya lugha simo ni kuwa inaweza kuwafanya watu waache kuyatumia maneno mengine ya Kiswahili wakidhania ni Sheng. Baadhi ya maneno hayo ni kama vile manzi ambalo ni neno la Kiswahili sanifu kumaanisha msichana ila wengi hulitumia kama sheng. Ashara kumaanisha idadi kumi ni sawa kwa Kiswahili lakini Kenya watu wandhania hiyo ni sheng.

Taarifa zinazohusiana

BBC © 2014 Ilani: BBC haihusiki na yaliyoandikwa na tovuti za nje ya BBC.

Ukurasa huu unaonekana vyema kwa kivinjari cha kisasa kikiwa na laha mtindo (CSS).Wakati unaweza kuona yaliyomo katika ukurasa huu kwa kivinjari ulichonacho, hautaweza kufaidi kuona kila kitu vizuri. Tafadhali zingatia uwezekano wa kuboresha progaramu ya kivinjari au kuwezesha laha mtindo (CSS) endapo unaweza kufanya hivyo.