Je ukabila unahujumu demokrasia Afrika?

Imebadilishwa: 28 Novemba, 2012 - Saa 10:35 GMT

Ghasia za baada ya uchaguzi nchini Kenya

Kipindi cha mpito katika demokrasia barani Afrika kinapigwa darubini kwa mara nyingine.

Wasiwasi sio tena juu ya wababe kutaka kusalia mamlakani , lakini ni juu ya wanasiasa kuhujumu demokrasia.

Ghasia za baada ya uchaguzi wa Kenya mwaka 2007-2008 zilidhihirisha ambavyo ukabila unaweza katika muda mfupi kuitumbukiza nchi katika vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Changamoto kubwa kwa demokarsia barani Afrika sio fahari ya kuwa na makabila mengi, bali ni kutumia makabila hayo kuendeleza siasa za ubinafsi ambazo zinachochea siasa za kikabila . Huo ni ukabila.

Kuna baadhi wanaosema kuwa ukabila unatokana na mipaka ya kikoloni iliyowagawanya watu katika mafungu ya kikabila.

Dhana hii inapendekeza kuwa kila jamii inapaswa kuwa na eneo lake , ambalo linakuza ushindani wa kikabila.

Vyama vya kisiasa nchini Kenya vilichukua takriban miaka kumi kumwondoa mamlakani rais mstaafu Daniel Arap Moi.

Miaka ishirini iliyopita ya vita nchini Somalia, imeonyesha hatari ya ushindani wa kikabila na kudhihirisha umuhimu wa kutumia mawazo kujenga nchi kuliko ukabila.

Ukabila ni adui mkubwa wa demokrasia

Kilichopewa kipaombele katika miaka ishirini iliyopita imekuwa kuwang’oa madikteta na kuendeleza siasa za vyama vingi.

Lakini kilichokosekana kabisa ni juhudi za kujenga vyama vya kisiasa ambavyo vina misingi mizuri. Nchi nyingi za kiafrika zimetumbukia katika siasa za kikabila kama kigezo cha ushindani wa kisiasa.

Ramani ya Afrika ikionyesha idadi ya makabila

Wanasiasa mara kwa mara hutumia makabila yao kuendeleza siasa za ubinafsi zisizo na misingi.

Lakini makabila hayajengwi kwa kuzingatia demokrasia na wala hakuna ushindani wowote.

Na kwa sababu ya hilo, ukabila ni adui ya kuimarika kwa demokrasia.

Kimsingi, ukabila umechukua nafasi ya taasisi thabiti za kidemokrasia ambazo hazijaweza kuimarishwa.

Ukabila umechangia pakubwa kuwepo mizozo ya vita vya wenyewe kwa wenyewe barani Afrika.

'Wajanja na wako makini’

Kulingana na utafiti uliofanywa nchini Marekani mwaka huu, nchi 19 za Afrika, zilisemekana kuzingatia demokrasia ikilinganishwa na utafiti wa mapema ulioonyesha nchi 24 mwaka 200-2008 kujitahidi kuimarisha demokrasia.

Utafiti huu unadhihirisha athari za ukabila kwa demokrasia barani Afrika.

Mnamo siku ya Ijumaa Idhaa ya kiswahili ya BBC itajadili swala hili na unaweza kuchangia kwa kutuma maoni yako kwenye ukurasa wetu wa facebook bbcswahili.

Nchi zenya makabila mengi

  • DR Congo: Idadi ya watu : Milioni 72, Zaidi ya makabila 250
  • Nigeria: Watu milioni 170 Zaidi ya makabila 250
  • Tanzania: Watu milioni 47; makabila 130
  • Chad: Watu milioni 11, zaidi ya makabila 100.
  • Ethiopia: Watu milioni 91 makabila 77
  • Kenya: Watu milioni 42 , zaidi ya makabila 70

Mfano nchini Kenya, wanasia walijikita zaidi tatika kujinufaisha kutokana na makabila yao kuliko kuungana kuwa na msimamo mmoja wa kisiasa.

Walinaswa kwenye mtego wa serikali iliyokuwa uongozini ambayo iliwagawanya kwa misingi ya kikabila.

Vyama vingi vya kisiasa vyenye misingi ya kikabila havina manifesto kwa sababu muda wote wanatumia kujiimarisha kikabila badala ya kuwa na mwelekeo wa kisiasa wenye manufaa kwa wananchi.

Ni wajanja sana.

Wanasiasa hukumbatia mitindo ya kisasa, huvalia mavazi ya kisasa ili kujiimarisha kisias. Hubuni miungano ya muda na kutaka uungwaji mkono kutoka dola za kigeni kama Uingereza, Ufaransa na Marekani.

Lengo lao kubwa ni kujiimarisha wenyewe huku wakiponda demokrasia. Kwao ukabila ni mchezo wa pata potea kwa hivyo hutumia lugha ya uchochezi kusababisha ghasia.

Sasa je siasa za ukabila zitawahi kuisha?

Kubuni vyama vya kisiasa ndio njia mojwapo ya kumaliza siasa za ukabila.

Mijadala hukusu sera pia ni kiungo muhimu katika kuchagiza demokrasia.

Manifesto zenye mwelekeo pia zinaweza kuleta ushindani ambao utalazimu vyama vya kisiasa kujitofautisha na vyama vingine.

Nchini Rwanda maelfu waliuawa wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe mwaka 1994 kwa sababu ya ukabila

Na pia mijadala kama hii itaweka wazi mambo yanayowahusu wananchi kwa ujumla.

Ni wazi kuwa maswala kama kawi, usafiri, kilimo na mawasiliano, pamoja na ajira kwa vijana, yanaibuka kama kauli mbiu katika siasa za Afrika licha ya tofauti za kimawazo.

Vyama vya kisiasa huenda visitofautiane kuhusu maswala kadhaa lakini vinaweza kupendekeza njia mbadala za kusuluhisha mambo .

Na kwa kuwa demokrasia inatoa nafasi kwa maendeleo endelevu na mafanikio, siasa za kikabila lazima zitiwe kwenye kaburi la sahau na pahala pake kuchukuliwa na taasisi za kisasa zenye kushinikiza demokrasia. La sivyo, bara la Afrika litaendelea kutumbukia katika athari za siasa za ukabila.

Taarifa zinazohusiana

BBC © 2014 Ilani: BBC haihusiki na yaliyoandikwa na tovuti za nje ya BBC.

Ukurasa huu unaonekana vyema kwa kivinjari cha kisasa kikiwa na laha mtindo (CSS).Wakati unaweza kuona yaliyomo katika ukurasa huu kwa kivinjari ulichonacho, hautaweza kufaidi kuona kila kitu vizuri. Tafadhali zingatia uwezekano wa kuboresha progaramu ya kivinjari au kuwezesha laha mtindo (CSS) endapo unaweza kufanya hivyo.