Hodi Hodi kombe la mataifa bingwa Afrika

Imebadilishwa: 29 Novemba, 2012 - Saa 14:37 GMT

Wachezaji wa Bafana Bafana

Baada ya kuandaa mashindano ya kombe la dunia mwaka wa 2010, Afrika Kusini, je Afrika Kusini iko tayari kuandaa fainali za mataifa bingwa barani?

Siku 50 zijazo, Tarehe 19 Januari mwaka wa 2013, wachezaji wa timu ya taifa ya Afrika Kusini wanaanza kampeini yao ya kuwania kombe la pili la michuano ya mataifa bingwa barani Afrika.

Timu hiyo inayojulikana kama Bafana Bafana inacheza mechi yake ya kwanza dhidi ya Cape Verde ambayo inashiriki katika fainali hizo kwa mara ya kwanza katika uwanja wa Soccer City mjini Soweto, kabla ya kutoana jasho na Angola kisha Morocco katika hatua ya makundi.

Mataifa mengine 15 barani Afrika yatashiriki katika fainali hizo za 29 tangu kubuniwa mwaka wa 1957, wakati nchi tatu zilishiriki.

Shirikisho la mchezo wa soka duniani FIFA, lililimbikizia Afrika Kusini sifa nyingi kwa kuandaa fainali hizo za dunia, na kuandikisha historia ya kuwa nchi ya kwanza Afrika kuwa mwenyeji wa mashindano hayo na pia kujenga viwanja vipya na vya kisasa.

Shirikisho la soka duniani lilipongeza Afrika Kusini kwa kuandaa michuano ya kombe la dunia 2010

Rais wa FIFA Sepp Blatter alisema Afrika Kusini ilipata karibu asilimia 100 katika maandalizi yake.

Naye rais wa Afrika Kusini Jacob Zuma alisema kuwa wao wameafikia malengo yao na wale waliokuwa wakidhani kuwa nchi hiyo haina uwezo wa kuandaa mashindano hayo, hawana budi ila kusalimu amri.

Afisa mkuu mtendaji wa kamati andalizi Danny Jordan kwa upande wake alisema ''wale waliokuwa na mashaka, sasa wanaamini kuwa tunaweza''.

Huku taifa hilo likijiandaa na mashindano mengine na kuimarika kwa mchezo huo, miezi 28 tangu nahodha wa Uhispania Iker Cassillas kupandisha bendera ya FIFA mjini Johannesburg wengi wanatarajia kuwa mbali na ufanisi wa maandalizi, timu ya Bafana Bafana pia inatarajiwa kufanya vyema.

'' Sisi tunacheza mchezo bora kuliko tulivyokuwa. Tuna viwanja bora zaidi lakini itachukua muda wa miaka minne zaidi ili, tuwe na uwezo wa kuonyesha mchezo ambao unastahili kuonyeshwa katika viwanja vya hadhi hii'' alisema Cavin Johnson, kocha mkuu wa klabu ya Platinum Stars inayoshiriki kwenye ligi kuu ya premier nchini Afrika Kusini.

Johnson ndiye kocha anayesifika kwa kutambua kipaji cha mcheza kiungo wa Newcastle Steven Pienaar wakati alipokuwa katika chuo cha kiufundi cha soka nchini humo na ana matamaini makubwa kuwa wachezaji wengine bora zaidi ambao wanasubiri kupewa fursa ili waonyeshe vipaji vyao na kuimarisha matokeo ya timu ya taifa.

'' kila wakati, Afrika Kusini itakuwa na wachezaji wenye talanta, unazungumza kuhusu mataifa ya Brazil, Nigeria, Italia, kuna vijana walio na talanta katika mataifa hayo, lakini la msingi ni jinsi wachezaji hao wanavyochaguliwa na mafunzo wanayopewa. Wachezaji wa Afrika Kusini walizaliwa na talanta ya soka kama wachezaji wa Barcelona ambao wanatambuliwa wakiwa na umri mdogo. Tatizo langu ni jinsi tunavyokuza talanta hiyo, kama wakufunzi na jinsi kila klabu inapata wachezaji wake ili kuiga mfano wa wachezaji wa Barcelona,'' aliongeza Johnson.

Roger Palmgren, ambaye ni kocha mkuu wa klabu ya AmaZulu anakubaliana na wazo la Johnson kuwa kuna wachezaji wengi ambao wana vipaji lakini tatizo kubwa limekuwa ni mafunzo wanayopewa na wakufunzi wao.

Michuano ya hivi karibuni ya mataifa bingwa barani Afrika.

Kinyume na ilivyokuwa wakati Afrika Kusini ilipoandaa michuano ya kombe la dunia, taifa hilo limekuwa likitekeleza mpango wa miaka sita ya kuimarisha mchezo huo, na hivyo maandalizi ya fainali za mwakani, imekuwa sio tatizo kubwa kwa waandalizi.

Awali, Libya ilikuwa mwenyeji wa fainali hizo, lakini kutokana na mapigano ya wenyewe kwa wenyewe tangu kuondolewa madarakani kwa Muammar Gaddafi, Libya ilipokonywa wadhifa huo, na badala yake Afrika Kusini ikakabithiwa jukumu hilo, la kuwa ilikuwa imeshinda fursa ya kuandaa fainali hizo mwaka wa 2012.

Mashabiki wa soka Afrika Kusini

Serikali ya nchi hiyo imetenga pauni milioni 32, kwa maandalizi ya fainali hizo. Pauni milioni tano nukta nane zitatumika na kamati andalizi huku masalio yakitumika kurembesha miji iitakayoandaa mashindano hayo na idara nyingine zitakazohusika na maandalizi.

Takriban mashabiki elfu 49 walitizama kila mechi ya kombe la dunia, na inakadiriwa kuwa asilimia 93 ya tikiti za mechi zote ziliuzwa, changamoto inayokumba kamati andalizi ya fainali hizo za Afrika, ni jinsi ya kuhakikisha kuwa mashabiki wengi wanafika uwanjani.

Mapema mwaka huu nchini Equatorial Guinea, mashabiki 200 walihudhuria mechi ya robo fainali kati ya Zambia ambao waliibuka mabingwa na Sudan mjini Bata.

Kamati andalizi ya fainali hizo nchini Afrika Kusini, imetangaza kuwa jukumu lao kuu ni kuhakikisha kuwa wanauza tikiti nyingi za mashindano hayo.

Katika awamu ya kwanza, tayari wameuza zaidi ya tikiti elfu 20, kiasi ambacho ni asilimia mia moja ya kiwango walichokuwa wakitarajia.

Shirikisho la mchezo wa soka nchini Ethiopia, limetuma maombi ya tikiti elfu 15, za mashabiki wake. Ethiopia inashiriki katika fainali hizo kwa mara ya kwanza kwa zaidi ya miaka 30 iliyopita.

Wachezaji soka wa Zambia

Zambia inatarajia kuuza zaidi ya tikiti elfu 10.

Lakini, kutokana na viwango vya umasikini nchini humo, bei ya tikiti imepunguzwa ili kuruhusu mashabiki wengi.

Mashabiki sasa wataweza kuhudhuria mechi mbili kwa tikiti itakayo gharimu randi 45 sawa na dola tano za Kimarekani.

Fainali hiyo ambayo ilianza kuonyeshwa moja kwa moja kupitia runinga, miaka ya 80, imekuwa kwa kiasi kikubwa.

Shirikisho la mchezo wa soka barani Afrika CAF, limesema, takriban watu bilioni 6.6 walitizama mechi 32 za mashindano hayo yaliyopita.

Rekodi ya Afrika Kusini Uwanjani

Ni jambo moja kuandaa mashindano hayo vyema, lakini je Afrika Kusini itawika mwaka ujao?

Wengi wanahisi kuwa Afrika kusini huenda ikiaibuka mshindi sawa na ilivyofanya mwaka wa 2006 wakati ilipokuwa mwenyeji wa fainali hizo miaka miwili tu baada ya taifa hilo kujinyakuliwa uhuru wake katika uchaguzi ulioshinda na chama cha Africa National Congress, kikiongozwa na Nelson Mandela.

Licha ya sifa tele za kuandaa michuano hiyo, Je Afrika Kusini itawika?

Gordon Igesund, aliteuliwa kuongoza Bafana Bafana, baada ya kushindwa kufuzu kwa fainali za mwaka huu na alipewa jukumu la kuhakikisha kuwa Bafana Bafana wanafika fainali za mwaka ujao.

Benny McCarthy, aliteuliwa kuwa mchezaji bora zaidi wakati wa fainali ya mwaka wa tisini na nane na anatarajia kocha mkuu atamjumuisha katika kikosi chake.

Igesund amekuwa na sifa ya kuimarisha timu anazoziongoza na Barani Afrika anafahamika kama Jose Mourinho wa Afrika Kusini.

Wachambuzi wengi wa soka wanahisi kuwa kocha huyo ana uwezo wa kuwatambua wachezaji ambao wanaweza kuandikisha marokeo mema.

Hata hivyo, timu hiyo ya Afrika Kusini haijacheza mechi za kutosha za kujipima nguvu.

Katika mechi zao tano za mwisho, Afrika Kusini ilishindwa na Brazil, Poland na Zambia, lakini wakaibuka washindi dhidi ya Kenya na Mozambique.

Kwa sasa Afrika Kusini inashikilia nafasi ya 84 katika orodha ya timu bora duniani nafasi 18 chini ya ilivyokuwa wakati wa fainali ya kombe la dunia mwaka wa 2010.

Phil Masinga, ambaye aliongoza Bafana Bafana kushinda kombe hilo na ambaye amefunga jumla ya magoli 18, katika mechi za kimataifa anasema, kikosi cha sasa kinaweza kujifunza mengi kutoka kwa kikosi kikilichoibuka na ushindi mwaka wa 1996.

Masaibu ya Afrika Kusini

Ili kushinda kombe hilo Afrika Kusini, itabidi kukabiliana na miamba wa soka barani Afrika.

Ivory Coast inapigiwa upato kushinda huku wengi wakimtarajia nyota wake Didier Drogba ambaye ana uzoefu mkubwa kulipiza kisasi cha kupoteza fainali iliyopita kwa Zambia kupitia mikwaju ya Penalti. Katika mashindano yaliyopita, Ghana na Nigeria haikufanya vyema na wengi wanatarajia timu hizo mbili zitaandikisha matokeo mema.

Ghana ilishinda kombe hilo mara ya mwisho mwaka wa 1982 ili hali Nigeria ilishinda mwaka wa 1994.

Timu zingine zinazotarajiwa kuipa Afrika Kusini ushindani mkali ni pamoja na Misri, Cameroon na Senegal.

Rekodi ya Afrika Kusini katika kombe la Mataifa Bingwa Barani Afrika.

  • 1996 Mabingwa
  • 1998 Nafasi ya pili
  • 2000 Nafasi ya Tatu
  • 2002 Robo finaili
  • 2004 Hatua ya Makundi
  • 2006 Hatua ya Makundi
  • 2008 Hatua ya Makundi
  • 2010 Haikufuzu
  • 2012 Haikufuzu

Gordon Igesund kocha mkuu

Umri: 56

Alizaliwa: Durban

Mataji: alishinda ligi kuu na klabu ya Manning Rangers, Orlando Pirates, Santos na Mamelodi Sundowns kati ya 1997-2007

Taarifa zinazohusiana

BBC © 2014 Ilani: BBC haihusiki na yaliyoandikwa na tovuti za nje ya BBC.

Ukurasa huu unaonekana vyema kwa kivinjari cha kisasa kikiwa na laha mtindo (CSS).Wakati unaweza kuona yaliyomo katika ukurasa huu kwa kivinjari ulichonacho, hautaweza kufaidi kuona kila kitu vizuri. Tafadhali zingatia uwezekano wa kuboresha progaramu ya kivinjari au kuwezesha laha mtindo (CSS) endapo unaweza kufanya hivyo.