Kero la saratani ya watoto Uganda

Imebadilishwa: 7 Disemba, 2012 - Saa 10:42 GMT

Saratani ya watoto Uganda

Kuna visa vingi vya saratani barani Afrika vinavyosababishwa na maradhi mengine. Hiyo ndio habari mbaya. Lakini habari njema ni kuwa zinaweza kuzuiwa kwa kutumia chanjo.

Zaidi ya nusu karne iliyopita, daktari mmoja kutoka Irelend ,Denis Burkitt alihamia Uganda na kufungua kliniki moja ya matibabu.

Aligutushwa na idadi kubwa ya visa vya watoto walio kuwa wanapata uvimbe kwenye uso ambao baadaye ulikuwa mkubwa kiasi cha kusakama mtoto na hata kusababisha kifo. Ilikuwa aina ya saratani ambayo alikuwa hajawahi kuiona.

Saratani hiyo ilikuja kujulikana kama Burkitt's lymphoma.

Hii leo katika wodi ya watoto wenye saratani nchini Uganda, iliyo katika taasisi ya matibabu ya saratani ,vitanda vimejaa watoto walio na saratani hiyo.

Ni mojawapo ya saratani ambayo huwaathiri watoto sana katika maeneo ya Afrika ya kati na huanza kwa mtoto kuugua maradhi fulani.

"Inahusishwa na virusi viitwavyo Epstein-Barr," anasema daktari Abrahams Omoding, mtaalamu wa matibabu ya saratani katika taasisi hiyo.

“Epstein-Barr,” ambayo husababisha homa ijulikanayo kama Glandular pia inaonekana kusababisha saratani ya Burkitt's lymphoma. Malaria pia inasemekana kuwa chanzo cha saratani hiyo.

Daktari Omoding anasema kuwa watu wengi wanadhani kuwa saratani husababishwa na watu kula vyakula visivyofaa, kula vyakula visivyostahili au kutokana na kemikai au miale yenye sumu.

Saratani ya Burkitt

"Saratani ya Burkitt imepata jina lake kutoka kwa daktari Burkitt. Sana huwaathiri watoto katika sehemu za Afrika ya Kati. Uvimbe wa uso huwa mojawapo ya dalili za saratani hii. Pia huathiri tumbo na kusababisha uchungu mwingi "

Lakini anasema kuwa maradhi mengi yanaweza kusababisha saratani. Mfano,viini tete vya H. pylori, husababisha vidonda vya tumbo na wakati mwingine inaweza hata kusababisha saratani ya tumbo.

  • Kiini ambacho husababisha ugonjwa wa ''Schistosomiasis'' kunaweza kusababisha saratani ya kibofu cha mkojo.
  • Saratani ya kizazi husababishwa na virusi vya human papilloma (HPV)
  • Saratani ya maini nayo inahusisha na virusi vinavyosababisha Hepatitis B.
  • Kaposi's sarcoma, ambao ni uvimbe wa celi za mwili, husababishwa na virusi vinavyowaathiri watu wenye ukosefu wa kinga mwilini.

Nchini Uganda, ambako watu wengi wameathiriwa na virusi vya HIV, saratani ya ''Kaposi sarcoma'' ni janga kubwa.

"Orodha hii ni ndefu," anasema daktari Omoding. "Hizi ndizo saratani ambazo watu wengi wanaugua. Zote zinasababishwa na virusi.’’

Katika nchi ya Amerika Kaskazini mfano Canada, ni moja ya saratani 25 pekee, ambazo zinaweza kulaumiwa kusababishwa na maradhi, kulingana na utafiti uliofanywa katika jarida la Lancet, katika nchi zinazostawi, ni moja kati ya saratani nne ambazo husababishwa na virusi au maradhi mengine.

Sababu?

Ramani ya nchi ambazo zina visa vingi vya saratani duniani

Hali duni ya usafi katika nchi zinazostawi inamaanisha kuwa watu wengi huwa katika mazingira chafu yenye viini. Na watu Kusini mwa Janagwa la Sahara, mfano, kuna uwezekano wa wao kutopata chanjo dhidi ya virusi vinavyosababisha saratani kama Hepatitis B.

Utafiti unaendelea nchini marekani kufahamu ambavyo virusi vinasababisha saratani.

Watafiti hao hupata damu au seli kutoka Uganda kila mwezi kuzifanyia utafiti. Zote hizo husafirishwa nchini Marekani zikiwa zimehifadhiwa katika theluji.

Uhusiano wa saratani na maradhi mengine ni kwamba maradhi yaliyo mwilini hushambulia seli za mwili na kuathiri utenda kazi wao. Virusi vya ''Epstein-Barr'' kwa mfano huathiri kinga ya mwili na kushambulia seli za B cells na kuzifanya kukuwa.

Hali hii hufanya seli kukuwa kw wingi na kuanza kuwa saratani. Lakini watafiti wanasema habari njema ni kuwa kuna uhusiano kati ya saratani na maradhi na kwamba unaweza kuvunjwa na hivyo kinga kupatikana

Ikiwa utagundua kuwa maradhi ndiyo chanzo cha saratani, ikiwa utatibu maradhi yale basi unaweza kuzuia saratani

Wasichana wengi waliobaleghe sasa wanapokea chanjo ya saratani ya kizazi katika maeneo mengi ya Afrika

Hii inafanyika tayari na chanjo ya HPV ambayo inalinda mwili dhidi ya virusi vinavyosababisha saratani ya kizazi.

Nchi nyingi zinazostawi, hutoa chanjo kwa wasichana ili kuwalinda dhidi ya virusi vinavyosababisha maradhi ya zinaa yanayoweza kusababisha saratani ya kizazi.

Kuna mafanikio pia na chanjo dhidi ya Hepatitis B. inayoweza kusababisha saratani ya maini na ambayo ni chanzo kikubwa cha vifo nchini China.

Lakini sasa kwa sababu ya kuanza kutumia chanjo hiyo tangu mapema miaka ya tisini, idadi ya vifo vinavyotokana na saratani hiyo vimepungua nchini China.

Kwa sasa hakuna chanjo bado ya kuwalinda watoto nchini Uganda, dhidi ya kupata saratani ya uvimbe. Lakini wanasayansi nchini Marekani kwa ushirikano na madaktari nchini Uganda, wanajitahidi kutafuta chanjo hiyo.

Taarifa zinazohusiana

BBC © 2014 Ilani: BBC haihusiki na yaliyoandikwa na tovuti za nje ya BBC.

Ukurasa huu unaonekana vyema kwa kivinjari cha kisasa kikiwa na laha mtindo (CSS).Wakati unaweza kuona yaliyomo katika ukurasa huu kwa kivinjari ulichonacho, hautaweza kufaidi kuona kila kitu vizuri. Tafadhali zingatia uwezekano wa kuboresha progaramu ya kivinjari au kuwezesha laha mtindo (CSS) endapo unaweza kufanya hivyo.