Watalii wabaguliwa Ugiriki

Imebadilishwa: 10 Januari, 2013 - Saa 22:55 GMT
Christian Ukwuorji

Ukwuorji alikuwa mtalii kutoka Marekani lakini polisi walifikiria ni mhamiaji haramu na kumpiga kiasi cha kulazwa hospitali

Maafisa wa polisi nchini Ugiriki wamekuwa wakitekeleza hatua kali katika kipindi cha miezi michache katika juhudi za kuwakamata wakimbizi haramu wanaoishi nchini humo.

Ugiriki imekuwa ikiendesha oparesheni kali ya kukagua pasipoti na vitambulisho vya watu wanaoshukiwa kuwa wahamiaji haramu.

Lakini katika juhudi hizo, watalii pia wamekamatwa, na wawili kati yao, kupigwa vibaya mno.

Mwezi Julai mwaka jana, Christian Ukwuorji, raia wa Marekani aliyezaliwa nchini Nigeria, na mwenye umri wa miaka 38, yeye na mke wake, na watoto watatu, waliamu kutalii nchini Ugiriki.

Walifika Rhodes na Santorini, na kisha kuamua kupitia Athens walipokuwa safarini kurudi nyumbani.

Alipokuwa akitembea katikati ya mji wa Athens, akiwa na rafiki yake mmoja, Ukwuorji alisimamishwa na maafisa wa polisi wa Ugiriki, na kuulizwa kuonyesha kitambulisho.

Polisi katika hali ya kamatakamata mjini Athens

Juhudi kali za kuwakamata wahamiaji haramu sasa ni kero kwa watalii

Lakini licha ya kuonyesha pasipoti, yeye pamoja na kundi moja la wahamiaji haramu walitiwa pingu na kupelekwa hadi kituo cha polisi.

Akiwa huko, Ukwuorji anaeleza kwamba alijaribu kuzipiga picha pingu mikononi kwa kutumia simu yake ya mkononi, na maafisa hao wa polisi walipotambua alikuwa anajaribu kufanya nini, walimrukia na kumpiga hadi kupoteza fahamu.

Alipopata fahamu alijipata hospitalini.

Ubalozi wa Marekani ulithibitisha kwamba Wamarekani weusi wamo kizuizini, chini ya polisi wa Ugiriki, ambao wamekuwa wakipambana na tatizo hilo la wahamiaji haramu mjini Athens.

Polisi hawakumueleza Okwuorji ni kwa nini walimkamata.

"Nilikwenda huko kutumia senti zangu, lakini walinisimamisha kutokana na rangi yangu," alieleza. "Ni wabaguzi wa rangi."

Ni vigumu kuthibitisha ni watu wangapi ambao wamejipata katika tatizo hilo - lakini ni idadi tosha ambayo imeifanya idara ya mashauri ya nje ya Marekani kutoa onyo kwa raia wake wanaonuia kuelekea Ugiriki.

Katika tovuti ya idara hiyo, tangu tarehe 15 Novemba, iliandika "tunathibitisha taarifa za raia Wamarekani weusi kukamatwa katika misako ya polisi kuwatafuta wageni wahamiaji mjini Athens", na pia juu ya miji ya Ugiriki kwa jumla "pasipo sababu kuwasumbua na kuwashambulia watu, ambao kutokana na rangi yao, wanadhaniwa kuwa ni wageni".

Polisi walimrudishia Ukwuorji pasipoti yake na simu yake iliyoharibiwa.

Hakushtakiwa kwa kosa lolote lile.

Ubalozi wa Marekani umetaka uchunguzi kufanyika, lakini miezi sita tangu hayo kufanyika, polisi hawajaeleza chochote.

Ukwuorji anaamini alibaguliwa, na amekiri kwamba hawezi kufika tena nchini Ugiriki.

Naye mtalii kutoka Korea Hyun Young Jung aliposimamishwa na jamaa mmoja mrefu katikati ya mji wa Athens, mtu ambaye alionekana kuchakaa, na akimzungumza kigiriki, alidhani ilikuwa ni tukio tu la ulaghai.

Kwa hiyo, kwa unyenyekevu aliomba radhi, na akaendelea kutembea.

Lakini baada ya muda mfupi, alisimamishwa tena, wakati huu, na aliyevaa magwanda ya polisi, na kumuuliza makaratasi yake.

Polisi akikagua vitambulisho na pasipoti

Polisi wamezidisha juhudi za kuwasaka wahamiaji haramu katika barabara za mjini Athens

Kwa kuwa ni msafiri mzoefu, alikuwa tahadhari mno.

Nchi ya Ugiriki ilikuwa ni kituo chaka cha 16 katika mwaka wake wa pili katika safari ya kuzunguka dunia nzima, na alikuwa tayari ameonywa kuhusu polisi bandi katika nchi hiyo, na ambao hutaka pesa kutoka kwa watalii.

Hivyo basi, alimuuliza afisa huyo kumuonyesha kitambulisho chake cha polisi.

Jung anasema, kinyume na matazamio yake, alitandikwa ngumi ya uso.

Kulingana na raia huyo wa Korea, katika muda wa sekunde chache, mtu aliyekuwa amevaa mavazi ya polisi, na kachero aliyemsimamisha Jung mara ya kwanza, walikuwa wamemlaza chini na huku wakimtandika mateke.

Kwa kushtuka, Jung aliamini kwamba alikuwa amevaniwa na majambazi, na akaanza kupaaza sauti akitaka msaada kutoka kwa wapita njia.

Raia wa Korea Hyun Young Jung

Jung alipigwa na polisi wa Ugiriki kiasi cha kudhania alikuwa ni majambazi

Lakini alipotiwa pingu na kubururwa hadi mita 500 na kufikishwa katika kituo cha polisi kilichokuwa karibu na hapo, ndipo alipotambua kweli alikuwa amekamatwa.

Jung anaeleza kwamba nje ya kituo cha polisi, afisa aliyekuwa na mavazi ya polisi, ghafula alimzaba kofi usoni.

"Kuna raia ambao waliona yaliyotokea, kama mtu anayefanya kazi katika duka ambalo lipo kando ya kituo cha polisi, lakini waliogopa sana kunisaidia," alieleza.

Ndani ya kituo cha polisi, Jung alisema alishambuliwa kwa mara ya tatu, alipokuwa akipanda ngazi, na hapakuwa na mtu wala kamera.

“Ninaweza kuelewa ni kwa nini waliniuliza kitambulisho, na ni kwa nini walinipiga mara ya kwanza. Lakini ni kwa nini waliendelea kunipiga hata baada ya kunitia pingu?” aliuliza.

Jung ni kati ya watu waliozuiliwa katika kundi ambalo lilikuwa na wahamiaji kutoka Afrika na Asia, na ambao walikuwa wamekamatwa kupitia msako uliowalenga wahamiaji haramu.

Cha kushangaza, oparesheni hiyo ilibandikwa jinga la mungu wa zamani wa Wagiriki aliyehusika na ukarimu kwa wageni, Xenios Zeus.

Nia ya oparesheni hiyo ni kupambana na tatizo la wahamiaji, ambao katika kipindi cha mwongo mmoja, inadhaniwa wameibadilisha sura ya mji wa Athens.

Luteni kanali Christos Manouras wa kitengo cha polisi cha Hellenic, anasema oparesheni Xenios Zeus, iliyoanzishwa mwezi Agosti, imeweza kupunguza idadi ya wahamiaji haramu.

Yeyote yule ambaye anayeonekana kama mgeni, na kuzua hisia ni mgeni, huenda akasimamishwa.

"Ikiwa mtu atasimamishwa na polisi, na akose njia ya kujitambulisha, basi tutaandamana naye hadi kituo cha polisi, mpaka uraia wake utakapojulikana,” alielezea.

" Nadhani hilo ni jambo la kawaida, na natazamia Wagiriki kutazamia hatua kama hiyo wakiwa ng’ambo."

Lakini ikiwa huku zaidi ya watu 60,000 wameshawahi kuzuiliwa katika barabara za mji wa Athens, ni chini ya watu 4,200 waliokamatwa tangu mwezi Agosti mwaka 2012.

Barabara kuu kutoka Uturuki hadi Ugiriki

Wahamiaji wengi haramu wameitumia barabara kuu kutoka Uturuki kuingia nchini Ugiriki

Baadhi ya wageni nchini Ugiriki pia walizuiliwa, licha ya kuwaonyesha polisi pasipoti.

Utalii ni muhimu kwa uchumi wa Ugiriki, hasa kwa kuwa biashara nyingi zimeporomoka.

Lolote lile ambalo litawazuia watalii kuitembelea Ugiriki litakuwa ni pigo kubwa kwa uchumi.

Raia wa Korea, Jung, aliyebaguliwa, anasema kila mara watu wanapomtaka ushauri ikiwa waitembelee Ugiriki, yeye huwaambia “Ni vyema zaidi kwenda Uturuki”.

Christian Ukwuorji, ambaye pia aliwasilisha rasmi malalamiko ya kubaguliwa, kupitia usaidizi kutoka ubalozi wa Marekani, sasa amesubiri miezi sita pasipo jibu lolote.

Angelipenda kuhakikisha watu waliomshambuliwa wakishtakiwa, lakini alieleza hana matumaini ya haki kutekelezwa.

"Maafisa wa polisi ni fisadi mno, na hakuna lolote ambalo litafanyika,” alielezea. “Nimejifunza kwamba hivi ndivyo Ugiriki ilivyo.”

BBC © 2014 Ilani: BBC haihusiki na yaliyoandikwa na tovuti za nje ya BBC.

Ukurasa huu unaonekana vyema kwa kivinjari cha kisasa kikiwa na laha mtindo (CSS).Wakati unaweza kuona yaliyomo katika ukurasa huu kwa kivinjari ulichonacho, hautaweza kufaidi kuona kila kitu vizuri. Tafadhali zingatia uwezekano wa kuboresha progaramu ya kivinjari au kuwezesha laha mtindo (CSS) endapo unaweza kufanya hivyo.