Waaga maisha mazuri kwenda Somalia

Imebadilishwa: 28 Januari, 2013 - Saa 14:43 GMT

Huku serikali mpya ya Somalia inayosaidiwa na Umoja wa Mataifa ikizidi kujizatiti katika mji mkuu wa Mogadishu na maeneo mengine chini ya wanamgambo wa al-Qaeda, wanawake wengi wamepata nafasi ya kurudi na kusaidia kujenga taifa, kulingana na taarifa ya Kate Forbes wa BBC.

Ayan Yussuf, 18, aliyerudi Mogadishu toka Canada, amevalia abaya na hijab huku akisema, “Ukiwa kwa wengine inabidi ufanye wafanyavyo wao," huku akikiri kwamba akiwa Canada anakoishi hua havai hivyo.

Anakuja Somalia kwa likizo – hii ikiwa mara yake ya kwanza kutembelea nchi hiyo.

"Nilitaka kuona palivyo. Siku moja tunaweza kuamua kurudi," Bi Yussuf alisema.

Ana ogopa chochote?

"Bila shaka, ndio! Sielewi patakuwaje."

Mtu akitupa macho kwa mara ya kwanza atadhani kwamba hakujabalidika chochote tangu mapema 2012. Ingali inaonekana kuwa nchi iliyo vitani, na usalama bado ni changamoto.

Uwanja wa ndege umefanywa kituo cha kijeshi kinacholindwa vilivyo na jeshi la Umoja wa nchi za Afrika ,Amisom.

Nje, magari ya aina ya pick-up yaliyojaa wanajeshi, vifaru na walinzi raia wanasubiri kuingia na kutoka kambini. Upande mwingine wa barabara, kuna mkahawa uliozingirwa na ukuta mrefu wa futi nane uliotengenezwa na magunia yaliyojaa mchanga na seng’enge.

Lakini kwingine mjini Mogadishu kuna harakati za ujenzi na ukarabati.

Kwa vile kumekuwa na utulivu kwa muda, Wasomali wanarudi nyumbani toka ng’ambo kwa wingi.

"Ndege zimejaa," mwanamme mmoja alisema, akiongea kutoka uwanja wa ndege mjini Nairobi, akielekea Mogadishu.

Wengi wao ni wanawake wanaotaka pia kujenga taifa ambalo limekuwa vitani kwa miaka 20 iliyopita.

Safia Yassin Farah ana miaka 34 na unapomuona akichapa kazi katika meza yake kazini, anafanana na mtu yeyote mwingine kokote duniani, ila tu ukiangalia nje kuna ukuta mrefu, seng’enge na walinzi waliojihami kwa silaha.

Safia alitoka Marekani ili kufanya kazi na vijana mjini Mogadishu, akiwasaidia kusoma na kutafuta ujuzi wa kazi.

"Siendi popote. Nabaki hapahapa. Niliacha kazi huko," Bi Farah asema. "Nilikulia Marekana na nikapata shahada yangu kutoka Chuo Kikuu cha New Hampshire. Nilikuwa na ajira, nyumba, nilikuwa na kila kitu."

Anasema alipata mvuto kurudi baada kusikia habari kuhusu watoto wakisomali waliokuwa wameathiriwa na vita, hii ikiwa pamoja na wale waliokuwa wamesajiliwa na al-Shabab.

"Niliona kuwa watoto walikuwa wanahitaji sana kusoma, kama wenzao katika nchi za Magharibi," Bi Farah alisema.

Bi Farah ana wasiwasi kuhusu mambo kadhaa kama ukosefu wa huduma za afya na usalama, lakini anasema kwamba hali si mbaya kama wanavyofikiria wengi."

Mabadiliko

“Somalia imebadilika sana,” Maryan Hassan, mwanafunzi wa sheria aliyezaliwa Uingereza alisema. “Ingawaje wanaume ndiyo kwa kawaida hutegemewa kuwa viongozi wa jamii zao, wengi walikufa wakati wa vita na kuwalazimisha wanawake wachukue usukani,” aliendelea kusema.

Naye Maluka Abdulkadir, aliyeacha kazi yake na kampuni kubwa nchini Marekani ya Merrill Lynch ili kurudi Mogadishu, anasema jambo gumu kwake ni kutokuweko kwa uhuru wa kutembeatembea mjini.

"Ukiwa Marekani unaweza kwenda popote na kufanya utakalo, lakini hapa huwezi pakia tu gari na eti kwenda dukani. Hali ya usalama hairidhishi," alisema Bi Abdulkadir.

Bi Abdulkadir hawezi kwenda popote bila walinzi waliojihami kwa silaha, hasa kwa sababu anafanya kazi katika Ofisi ya Waziri Mkuu.

"Huwa nawaambia wasichana kuhusu maisha yangu – kama nilivyosoma chuo kikuu na nilivyojitahidi kufika hapo. Wakati mwingine, hiyo inakuwa mara ya kwanza kwao kutafakari kama wanaweza nao kwanda chuo kikuu," alisema Bi Hassan.

Lakini siyo kila mtu anayetaka kuishi Somalia.

Samira, 40, anasema kwamba watoto wake hawataki kurudi Somalia, hata kwa likizo. "Hawataki. Iwapo nitaamua kurudi itabidi nisubiri hadi wakue. Watu wananiuliza kwa nini nataka kurudi. Ni kichaa? Nami nawaambia: 'Inanibidi. Hii ni nchi yangu.'"

Taarifa zinazohusiana

BBC © 2014 Ilani: BBC haihusiki na yaliyoandikwa na tovuti za nje ya BBC.

Ukurasa huu unaonekana vyema kwa kivinjari cha kisasa kikiwa na laha mtindo (CSS).Wakati unaweza kuona yaliyomo katika ukurasa huu kwa kivinjari ulichonacho, hautaweza kufaidi kuona kila kitu vizuri. Tafadhali zingatia uwezekano wa kuboresha progaramu ya kivinjari au kuwezesha laha mtindo (CSS) endapo unaweza kufanya hivyo.