Wazungu wasituletee ukoloni

Image caption Paul Nabiswa

Wazungu wasituletee ukoloni – Na Paul Nabiswa

Mojawapo wa sifa kuu za lugha yoyote ile ulimwenguni ni kuwa ‘lugha hukua’. Katika misingi hiyo ni sawa kusema kuwa lugha hujisimamia ikiwa ina msamiati mpana tena wa kutosha.

Ni sawa kusema kuwa lugha inaponawiri wasemaji na wazawa wake hujimudu kuitumia kwa wepesi bila mahangaiko ya kutafuta msamiati ama kutumia msamiati mdogo tu.

Nimeanzia mbali kidogo kwa sababu nimetambua kuwa waswahili wananyanyaswa na wazungu katika kutumia lugha yao ya Kiswahili. Nasema wazungu wametukalia kwa sababu wamewatumia waswahili wenyewe kudunisha lugha yao.

Katika taaluma ya uanahabari watangazaji wa Kiswahili wanabanwa zaidi ili watumie maneno fulani mahsusi.

Hii inafanya lugha ya Kiswahili kuonekana kuwa ina umasikini mkubwa mno wa maneno. Wazungu wanahabari wenyewe wanatumia visawe vya maneno na hakuna anayewakashifu.

Japokuwa tunajua kuwa umuhimu wa habari ni kuwasiliana, lakini palepale ni vyema kutambua kuwa kubadilisha maneno katika taarifa ni hatua muhimu.

Mwanzo inaonysha kuwa kuna demokrasia katika lugha ya Kiswahili, na pili inaleta picha kuwa Kiswahili kina msamiati mpana.

Katika kutoa mifano utapata wazungu wakisema figures, digits, numbers na statiscs kwa maana ya idadi. Hata hivyo Mswahili hujikita katika majina mawili tu. Takwimu na tarakimu. Kenya wanatumia sana Takwimu.

Je makosa yako wapi mimi nikisema mahaba, mwenzangu aseme huba, mwengine aseme mapenzi na hata mwingine aite hawa? Waswahili tumefinywa eti tuseme tu mapenzi na hao wanaosema hivyo ni watu wenye uwezo wa kusema Kiswahili lakini wanajifanya kuwa wamo katika mbawa salama za Kiingereza.

Kuna haja ya dharura kwa Kiswahili kupata wakombozi wao ili meli yao isizamishwe na mawimbi ya Kiingereza. Ni muhimu kutaja kuwa Kiswahili kina zaidi ya lahaja ishirini na ikiwa jina haliko kwa lahaja ya Kimtang’ata kwa mfano si dhambi jina lenye mizizi ya lahaja ya Kivumba kutumiwa.

Vivyo hivyo wapemba hawatakiwi kusutwa wanapotumia maneno yasiyopatikana katika lahaja ya Kiswahili sanifu. Yaani lahaja inayotumika katika mazingira rasmi.

Hivyo basi nikisema kidole na jirani yangu asema chanda ni neno moja. Nikiona ni bora kuita mshipi na mama yangu aone neno mkanda linafaa hamna dhambi. Kwa hoja hiyo hiyo, ikiwa kwetu tumezoea kumwita mama ya mzazi nyanya na mwingine aseme bibi pia ni sawa. Kadhalika ukimwita mama kuwa ni nyina hutakiwi kusulubiwa.

Ikiwa wasemaji wa Kiswahili wataanza kufikiria mambo kwa mawanda hayo, ni sawa kusema kuwa Kiswahili kitakuwa kimepata watetezi.

Hata hivyo ni muhimu kupima mahali unapozungumzia maneno hayo. Ikiwa ni mazingira ya mazungumzo ya kawaida ni sawa zaidi lakini darasani kidogo kuna utata. Kwa hivyo wazungu wakiachwa watumie maneno yao, waswahili wasifinywe wakifanya hivyo.

Paul Nabiswa ni mwanahabari wa BBC na hayo ni maoni yake.