Mjadala wa kihistoria Kenya

Image caption Raila Odinga na Uhuru Kenyatta ndio wagombea wakuu wa uchaguzi huu. Wachanganuzi wanasema kinyang'anyiro ni kikali zaidi kati yao

Mamilioni ya wakenya walikaa kitako kujionea mjadala wa kihistoria wa wagombea wa urais nchini Kenya, Jumatatu Jioni. Wagombea saba wanaume waliokuwa wamevalia suti, hatua baada ya nyingine waliwasili kwenye jukwa la shule moja viungani mwa mji wa Nairobi.

Martha Karua, mwanamke pekee, kwenye jukwaa hilo , naye alikuwa amevalia vazi la kupendeza. .

Waliamkuana na kupigiana tabasamu kabla ya kijasho kuanza kuwatoka mbele ya mamilioni ya wakenya.

Kila mmoja alikuwa na dakika mbili za kujieleza kwa nini anataka kuwa rais wa nne wa Kenya kwenye uchaguzi utakaofanyika Machi tarehe nne.

Baadaye wageni waliokuwa wamefika kushudia mjadala huo takriban watu 200 nao walipata fursa ya kuwahoji wanasiasa hao.

Mjadala ulistahili kuchukua masaa mawili lakini ukazidi kwa lisaa limoja.

Mapema mjadala huo nusura kupata pigo baada ya mmoja wa wagombea Paul Muite, na Mohammed Abdubouba Dida kwenda mahakamani kulalamika kuwa hawakualikwa. Lakini waliweza kushirikikishwa.

'Mtihani mkubwa'

Kesi dhidi ya mgombea Uhuru Kenyatta ambayo inasubiriwa katika mahakama ya ICC ndiyo ilioneakana kuchangamkiwa na wagombea hao.

Image caption Ghasia zilizotokea Kenya baada ya uchaguzi wa 2008, zilisababisha maafa makubwa

Uhuru alitakiwa kujibu ni vipi ataongoza nchi hii wakati anakabiliwa na kesi ya uhalifu dhidi ya binadamu kufuatia ghasia zilizoibuka wakati wa uchaguzi wa mwaka 2007/2008.

Alitakiwa hasa kujibu hoja ya tabia ya viongozi wa Kenya kufanya makosa bila kujali, alipoulizwa kueleza kwa nini hawezi kujiondoa kwenye kinyang'anyiro wakati ana kesi ya kujibu ICC.

Kenyatta na mgombea mwenza wake William Ruto wana kesi ya kujibu Hague baada ya kuhusishwa na mauaji yaliyotokea wakati wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2007.

Zaidi ya watu elfu moja waliuawa na wengine laki tatu kuachwa bila makao baada ya Rais Kibaki na Waziri mkuu kutofautiana kuhusu matokeo ya uchaguzi huo.

Kenyatta alisema kuwa yeye na Ruto watajitetea vikali dhidi ya tuhuma zinazowakabili Hague. Kesi hiyo hata hivyo haitawazuia kufanya majuku yao ikiwa watapatikana na hatia, alijitetea Uhuru

Mpinzani mkuu wa Uhuru, waziri mkuu Raila Odinga naye alitakiwa kujibu kuhusu ghsia zilizokumba nchi baada ya uchaguzi huo. Raila alijibu kuwa aliibiwa ushindi wake na washirika wa Kibaki.

Wafuasi wa pande hizo mbili walipigana kwa misingi ya ukabila hadi makubaliano ya kugawana mamlaka yalipoafikiwa.

Wakati wa mjadala huo, Bi Karua alisema ghasia hazingetokea ikiwa Odinga wangepinga matokeo hayo kupitia mahakama kuliko kwenda barabarani na kusababisha vurugu.

Muite alikosoa aliyekuwa kiongozi wa mashtaka katika ICC Luis Moreno Ocampo kwa kuwafungulia mashtaka Uhuru na Ruto badala ya kuwajibisha Kibaki na Raila , ambao walikuwa wagombea wakuu wa uchaguzi huo.

Alisema ikiwa chama chake kingeshinda uchaguzi huo, ataweza kuanzisha upya kesi hiyo kutaka wawili hao kujieleza.

Kwa upande wake Raila alionya wakenya dhidi ya kumchagua kiongozi ambaye muda wake wote atakuwa ICC, kesi yake ikisikilizwa.

Image caption Aliyekuwa kiongozi wa mashtaka katika mahakama ya ICC Luis Moreno Ocampo

"huwezi kuongoza nchi kupitia kwa Skype," alisema Raila.

Wagombea hao pia walizungumzia maswala ya ukabila, elimu na afya.

Wakenya walioelezea BBC maoni yao walisema walifurahishwa na Bi Karua aliyekuwa mwanamke pekee anayegombea urais kwenye mjadala huo.

Hata hivyo walisema kuwa watabadili ambavyo walikuwa wamejiandaa kupiga kura.

Hata hivyo hili sio jambo la kushangaza kwa sababu wakenya wengi hupiga kura kwa misingi ya ukabila.

Wachanganuzi walisema mjadala huo haukuwa nuzito mkubwa kwa sababu idadi ya wakenya wenye kipato cha kadri ambao wangeweza kushawishiwa na mjadala huo ni wachache.