Wapokonywa redio Zimbabwe. Kunani?

Redio kuu kuu zinazotumia kawi ya jua, huenda ni wazo zuri kuwasaidia raia wa Zimbabwe ambao wamekwama katika limbi la umaskini kupiga gumzo nyakati za jioni kabla ya usiku kuingia.

Lakini maafisa wakuu hawaonekani kuunga mkono hatua hiyo, na hadi sasa wamewapokonya wakaazi redio nyingi sana katika miezi ya hivi karibuni.

Wanakijiji mashariki mwa nchi walikuwa na hofu usiku mmoja wakati polisi walipovamia nyumba zao na kufanya msako wa nyumba hadi nyumba wakitafuta redio hizo.

"Ilipowadia usiku wa manane, polisi walikuwa wamepokonya watu redio thelathini,'' alisema Clara Kadzviti, anayeishi katika kijiji kimoja mashariki mwa Harare.

Yeye pamoja na wanakijiji wengine, walilazimishwa kuwatambua majirani zao ambao walikuwa wanamiliki redio hizo ambazo zina uwezo wa kushika masafa ya FM na AM ambazo zilitolewa na shirika moja lisilo la kiserikali, ambalo lilikuwa katika eneo hilo kwa shughuli za maendeleo kujenga barabara na vyoo.

"Walinipokonya simu zangu, na kutaka niwatambulishe watu walio kwenye simu yangu,'' alisema akielezea ambavyo vyumba vyao vilisakwa na kuchunguzwa.

"Watu wengi walipelekwa kwenye kituo cha polisi, na tukaonywa kuwa watakaopatikana na redio hizo watakiona cha mtema kuni.''

Watu wengi wanahofia kuwa huenda pasiwepo uhuru wa vyombo vya habari kama inavyotakikana katika katiba mpya ilivyopitishwa hivi karibuni.

Lakini polisi wamesema kuwa redio hizo zinatumika katika kueneza matamshi ya chuki yanayochochewa na makundi ya watu wasiojulikana kabla ya uchaguzi mkuu kufanyika mwezi Julai.

Hii ni baada ya miaka minne ya kuhudumu kwa serikali ya kugawana mamlaka kati ya chama cha Rais Robert Mugabe Zanu-PF na kile cha MDC chake waziri mkuu Morgan Tsvangirai.

"Tuna ushahidi kuwa redio hizo zimeingizwa hapa nchini kimagendo kutoka nchi za Magharibi, na redio hizi zinatumika kueneza propaganda katika maeneo ya mashinani,'' alisema msemaji wa polisi Charity Charamba.

Zaidi ya miradi 10 ya kijamii ya redio ambayo imeomba vibali kupeperusha matangazo yao, pamoja na vituo vingine binafsi vimeelezea wasiwasi tangu serikali ya muungano kuingia mamlakani bado hawajapata leseni za kufanya kazi.

Wanaharakati wamekuwa wakitetea wakisema kuwa wananchi wanahitaji vyombo vingine vya habari mbali na vile vya serikali ambavyo kazi yao ni kuendeleza propaganda ya serikali.

Baadhi ya stesheni za redio zimetajwa kuwa vyombo vya maharamia ambavyo ni tisho kwa usalama wa nchi.

Katika miaka ya nyuma, serikali ya rais Mugabe imetuhumu serikali za magharibi kwa kuingilia siasa za nchi na kupanga njama ya kumng'oa mamlakani.

Mapema mwezi huu mkurugenzi wa mradi wa 'kuendeleza amani nchini humo, Jestina Mukoko, alizuiliwa na polisi na kuhojiwa kufuatia madai ya kuendesha kinyume na sheria shirika lisilo la kiserikali.

Mukoko alikamatwa baada ya kufanywa msako katika ofisi za moja ya stesheni hizo mjini Bulawayo , moja ya stesheni ambazo hazijasajiliwa na serikali na ambayo husambaza vipindi vyake kwa CD.

Zaidi ya redio miamoja za masafa mafupi zilichukuliwa na polisi, na mhariri mmoja kukamatwa na kushtakiwa kwa kosa la kuingiza kimagendo nchini humo rediio hizo

Baadhi wanahoji kwa nini ni kinyume na sheria kwa mtu kusikiliza redio wakati kila mtu ana haki ya kumiliki redio?

Wanaharakati wanalalamika wakisema kuwa kulingana na sheria msikilizaji wa redio anapaswa kuwa na leseni lakini sio vyema watu kupokonywa redio zao kwa kuwa hawana leseni.

Katika kulinda sheria inayopatia watu uhuru wa kujieleza pamoja na uhuru wa vyombo vya habari, inatazamiwa kuwa katiba mpya itaweza kuzuia ghasia zilizotokea baada ya uchaguzi mwaka 2008.

Lakini wengi wanahisi kuwa itakuwa vigumu kubadilisha tabia ya serikali kukandamiza watu

Mwezi Julai Mugabe ambaye amekuwa mamlakani kwa miaka 33 na anaungwa mkono zaidi na watu wa mashinani na bado atakuwa na kibarua kumenyana na Morgan Tasvangirai wa MDC