Waafrika wanavyobaguliwa India

Waafrika wanaoishi ndani na nje ya mji mkubwa zaidi wa kibiashara nchini India, Mumbai (Bombay), wanalalamika kuhusu ubaguzi wa rangi na polisi kuwanyanyasa kila mara.

Sambo Davis ni raia wa Nigeria ambaye amemuoa mwanamke wa kihindi na wanaishi naye mjini Mumbai.

Stakabadhi zake zote ni halali lakini alikamatwa na polisi hivi karibuni baada ya kushukiwa kuhusika na bishara za mihadarati.

Yeye pamoja na waafrika wengine 30, walizuiliwa kwa masaa mengi kabla ya kuachiliwa na kuombwa msamaha.

Lakini siku iliyofuata, bwana Davis alisema kuwa alishtushwa sana kusoma kwenye magazeti kuwa walikuwa wamekematwa kwa kuhusika na biashara haramu ya mihadarati.

"polisi wanatuona sisi kama umbwa," anasema Davis.

Bwana Davis anadai kuwa mara kwa mara yeye hubaguliwa anapojaribu kukodisha nyumba katika sehemu zenye watu wa kipato cha kadri.

Hata hivyo yeye ni mmoja wa wale wenye bahati. Alifanikiwa kupata nyumba nzuri ya kukodisha na yote hayo ni shukrani kwa mkewe mhindi na pia anamiliki mkahawa mjini Mumbai.

Lakini wenzake kutoka Nigeria, wanakabiliwa na tatizo la ubaguzi wa rangi. ''Wanapokwenda kutafuta nyumba, katika maeno fulani, wao huambiwa, 'wewe ni mweusi, wewe ni mnigeria na hautakiwi hapa'. Huu ni ubaguzi wa rangi.'

Mchezo wa Paka na Panya

Hakuna idadi kamili ya waafrika wanaoishi mjini Mumbai, lakini tangu uchumi wa India kuanza kuimarika katika miaka ya hivi karibuni wengi wamekuja kufanya kazi ndani na karibu na mji huu.

Takwimu zisizo rasmi zinasema kuwa idadi yao ni zaidi ya watu 5,000.

Wengi wao wanahusika na biashara ya kuuza nguo nchini Nigeria na katika nchi zengine za kiafrika.

Wengine ni wanafunzi wakiwa kwenye vyuo vikuu vya kifahari na taasisi zengine za elimu.

Lakini pia kuna mamia ya waafrika, wengi wao wa Nigeria wanaoishi hapa kama wahamiaji haramu. Aidha wamepoteza pasi zao za usafiri au muda wao wa kuishi nchini humo umekwisha.

Kila siku watu hawa hujificha ili wasikamatwe na polisi , kwa sababu ikiwa watakamatwa watatiwa ndani.

Ikeorah Junior kutoka Lagos anamiliki mkahawa wa vyakula vya kiasili katika eneo moja lenye shughuli nyingi mjini Mumbai.

"sielewi kwa nini polisi wanafanya msako wa nyumba hadi nyumba, kuwakamata watu wasio na stakabadhi zao. Ikiwa hawana stakabadhi halali basi warejeshwe makwao,'' anasema Junior.

Ahmed Javed, mwenye jukumu la kuhakikisha sheria inafuatwa, katika jimbo la Maharashtra,anasema kuwa hilo sio rahisi kama inavyodhaniwa.''Wakati mwingine hawana pasi. Kwa hivyo ikiwa uraia wao haujulikani hawezi kuondolewa nchini humo.''

Mamia ya wahamiaji haramu wanaishi katika barabara ya Mira mjini Mumbai.

Waafrika wanajulikana kwa majina mawili hapa India, Negro au kaalia.

"sisi huwaita Negro kwa sababu ni weusi na wanaogopesha sana,'' alisema mwanamke mmoja.

''Hawawezi kupata nyumba mjini Mumbai,ndio maana wanaishi katika barabara hii ya Mira nje kidogo ya Mumbai. Kwa nini? Kwa sababu ya wanavyoendesha maisha yao. Wao huuza madawa ya kulevya na wanajihusisha na vitendo haramu. Hahawezi kuaminiwa,'' alisema mwanaume mmoja mkongwe.

Aibu kubwa

Licha ya hali hii, Sheeba Rani aliolewa na Sambo Davis miaka minne iliyopita na wana watoto wawili.

Bi Davis anasema kuwa wazazi wake ni wakristo na waliwatakia kila la kheri katika ndoa yao kwa sababu wanaamini kuwa ndoa yao ni mapenzi ya Mungu.

Lakini anasema kuwa marafiki zake, jamaa zake na jamii kwa ujumla walimtenga tangu alipooa.

Bi Davis anasema kuwa tabia ya watu wake kwa waafrika weusi inamtia aibu sana

"siku ambazo nilikuwa natembea naye tukienda zetu madukani, nilimtaka saa zote kunishika mkono. Lakini watu walipotuona, walidhani natoka kwa familia mbaya au hata kuwa mimi ni kahaba.''

Zamani kidogo hakujua kwa nini watu weusi wanabaguliwa sana lakini siku hizi anaelewa.

"kwa sababu watu wetu wanapenda ngozi nyeupe. Ikiwa ningeolewa na mzungu, watu wangenipenda sana na ningekubaliwa zaidi na jamii.''

Bwana Davis anasema anaamii kuwa anabaguliwa tu kwa sababu yeye ni mweusi. Kwa sababu anatoka Afrika na kuwa yeye ni mnigeria. Nadhani wahindi wanatuona sisi kama sio watu kama wao.