Ujumbe wa mhariri

Caroline Karobia - Mhariri wa Sema Kenya
Image caption Caroline Karobia - Mhariri wa Sema Kenya

Katika msimu huu mpya, Sema Kenya itazuru takriban maeneo 30 ya nchi, kujadili maswala nyeti yanayowakabili wakazi wa maeneo hayo.

Kwa mara nyingine tena raia watapata fursa ya kuwahoji viongozi wao moja kwa moja. Makala haya yatapeperushwa kuanzia jumapili tarehe 16 Juni 2013 hadi mwisho wa mwezi Januari hapo mwakani.

Mambo mapya

Katika msimu huu wa pili, mambo kadha wa kadha yamejumuishwa kuhakikisha kipindi hiki kinaendelea kuwaelimisha raia kuhusu maswala ya uongozi.

Tofauti na msimu wa kwanza ambapo Sema Kenya ilijadili maswala mbali mbali katika kipindi kimoja, wakati huu tutakuwa na mada maalum kila juma ili kuhakikisha maswala muhimu yanajadiliwa kwa kina.

Sema Kenya huzuru maeneo tofauti kila wiki, msimu huu tutatembelea maeneo mbalimbali na kufika hadi mashinani.

Kuanzia mji wa Mwingi, kaunti ya Kitui , Lodwar katika kaunti ya Turkana, hadi Kwale pwani ya Kenya, Sema Kenya itakuwepo kila jumapili kupitia Idhaa ya BBC, redio washirika na kituo cha televisheni cha KBC channel 1.

Msimu huu pia unaanza punde tu baada ya serikali mpya ya ugatuzi kuchukua hatamu, hivyo basi tutakupa fursa ya kukutana na viopngozi wako wapya uliowachagua.

Kuanzia waakilishi wa kaunti, wabunge, maseneta, waakilishi wa akina mama, magavana na pia viongozi wa ngazi za juu serikalini.

Tutawajumuisha pia wataalamu wa maswala mbali mbali, waakilishi wa mashirika ya kijamii na viongozi wa kidini.

Tovuti/mtandao wa kijamii

Katika tovuti ya bbcswahili.com\semakenya ambapo unaweza kupata vipindi vyetu, tumeongeza mambo kadhaa kama vile blogu ya kila wiki ya msimulizi wa kipindi Joseph Warungu ambapo atazungumzia zaidi kuhusu matukio kabla, wakati na baada ya kipindi kupererushwa.

Pia utapata fursa ya kutizama picha safi zaidi zilizochukuliwa wakati wa kurekodi kipindi. Unaweza kutizama timu mpya ya Sema Kenya katika tovuti hii.

Redio washirika

Aidha, katika msimu huu, unaweza kutegea vipindi vyetu kupitia redio tofauti nchini. Baadhi ya redio tunazoshirikiana nazo ni: Coro FM, Kitwek FM na Pwani FM zote za shirika la utangazaji nchini KBC; Mwanedu FM; Pamoja FM, Redio Sahara,Redio Mambo, Star FM na KU FM.

Ndio meli ya Sema Kenya imeng’oa nanga, jiunge nasi katika safari hii.

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii