Mhariri wa Sema Kenya anasema

Makala ya BBC Sema Kenya wiki jana mjini Nairobi ilifanikiwa sana licha ya changamoto nyingi.

Kwanza, kujiondoa kwa dakika za mwisho mwisho kwa vigogo wa muungano unaotawala wa Jubilee katika kushiriki kupiga msasa utendaji kazi wa rais Uhuru Kenyatta kulileta hofu kidogo.

Walikuwa wamekubali mwaliko mwetu.

Ilibidi mipango ya dharura kufanywa na shukrani za dhati ziwaendee watayarishi wa Sema Kenya, Wairimu Gitahi na Lilian Muendo kwa kukuna vichwa usiku kucha hadi kipindi cha Nairobi kikafanikiwa.

Hata hivyo, ni jambo la kutia moyo kwamba mwakilishi wa muungano wa Jubilee kwenye jopo la viongozi, Bw Moses Kuria, mbali na kutekeleza wajibu wake vizuri, aliandika makala katika gazeti moja la nchini Kenya ( The Standard on Sunday 21/07/13) kusifu na kufafanua umuhimu wa kipindi cha Sema Kenya kuwahamasisha wananchi wa kawaida na kuwahoji viongozi.

Jumapili hii

Jumapili hii tunakita hema katika kaunti ya Siaya magharibi mwa Kenya.

Siaya ni kaunti iliyo na sifa za kipekee hapa nchini Kenya na kimataifa.

Wasomi wengi kama babake rais wa Marekani, Barack Obama, mmoja wa wasisi wa siasa za upinzani nchini Kenya, hayati Jaramogi Oginga Odinga na mwanawe Raila Odinga, pamoja na maprofesa chungu nzima waliotapakaa duniani kote wengi wao wanatoka Siaya.

Lakini licha ya Siaya kuwa na sifa hizo, ikiwemo kuwa ni asili ya kiongozi wa nchi yenye uwezo mkubwa duniani- Marekani, kiwango cha maendeleo ni cha kusononesha.

Je, ni sababau ya msimamo wao wa kisiasa ambao tangu jadi unachukuliwa kama ni wa ki upinzani?

Sasa je, mfumo mpya wa serikali za ugatuzi ndiyo suluhisho la matatizo ya Siaya?

Basi nakuomba kwa moyo mkunjufu uchangie kuhusu mada hii kwa kutembelea tovuti yetu na mitandao ya kijamii: bbcswahili.com/sema Kenya, Facebook, BBCSemaKenya, Twitter bofya @bbcsemakenya.

Pia waweza kushiriki kwa kuskiliza redio: Idhaa ya Dunia ya BBC (Nairobi 93.9FM, Mombasa 88.1FM) kila Jumapili saa saba alasiri na televisheni, KBC Channel 1 kila Jumapili saa kumi na mbili jioni.

Wanyama wa Chebusiri

Mhariri wa Sema Kenya