Kiamsha kinywa ni muhimu kwa moyo wako!

Watu wanapaswa kula kiamsha kinywa ili kuweka mioyo yao katika hali nzuri , kulingana na utafiti uliofanywa nchini Marekani.

Utafiti wao uliowahusisha wanaume 27,000 ulionyesha kuwa wale wasiokula kiamsha kinywa wako katika hatari ya kupata matatizo ya moyo.

Kikundi hicho cha wataalamu katika chuo kikuu cha Havard kitivo cha afya ya umma,kilisema kuwa kukosa kiamsha kinywa kunasababisha mwili kutumia nguvu nyingi zaidi kuliko kawaida.

Taasisi ya matibabu ya moyo Uingereza inasema kuwa kiamsha kinywa huwazuia watu kula vitu vyenye sukari kabla ya chakula cha mchana.

Wanaume waliofanyiwa utafiti wako kati ya umri wa miaka 45-82, na walichunguzwa kwa miaka 16. Wakati wa utafiti huo, zaidi ya watu 1,500 waliathirika kutokana na mshtuko wa moyo.

Hata hivyo, watu waliokosa kiamsha kinywa wako katika hatari kubwa ya kupata matatizo ya moyo kwa asilimia 27 kuliko wale wanaokula asubuhi.

Hata hivyo watafiti walizingatia mambo kama uvutaji sigara na kufanya mazoezi sana.

Mtafiti mkuu Dokta Leah Cahill aliambia BBC: "ujumbe muhimu kwa wote ni kuwa kula kitu asubuhi unapoamka au katika kipindi cha saa moja baada ya kuamka. ''

"matokeo yanaonyesha kitu kodogo ni bora kuliko kutokakula kitu chochote, lakini ni bora kupata lishe bora.''

Alisema kuwa muda ambao mtu anakula ni muhimu na kusubiri hadi nyakati za mchana kabla ya kula chochote ni vibaya kwa mwili wa binadamu.

Aliongeza kuwa hali hii inaweza kusababisha shinikizo la damu mwilini , unene kupindukia na ugonjwa wa kisukari, maradhi yanayoweza kuathiri moyo.

"usikose kiamsha kinywa,'' alisisitiza Dokta Cahill.

Hata hivyo wakosoaji wa utafiti wanasema kuwa , waliwachunguza wanaume pekee na tena wale walio na umri wa miaka 45 na zaidi kwa hivyo itakuwa muhimu kuthibitisha kuwa kukosa kiamsha kinywa kunaweza kuathiri watu wengine walio na umri wa chini ya miaka 45.