Eti waafrika ni waraibu wa pombe?

Image caption Waraibu wa pombe nchini Nigeria

''Afrika ina tatizo la ulevi" haya ndiyo yalikuwa maandiko kwenye jarida la Time Magazine.

Lakini je kuna ushahidi wowote kuthibitisha madai haya?

Kate Wilkinson, mtafiti katika mtandao wa Africa Check ,anaweza kuwa na jibu kwa swali hili akisema kuwa viwango vya ulevi vinatofautiana katika mataifa 55 ya bara hilo.

"kuna dhana tofauti kuhusu pombe. Baadhi ya imani za dini mbali mbali kuhusu pombe na taarifa hii ya ujumla kuhusu tabia ya ulevi barani Afrika sio sahihi, '' anasema Kate

Takwimu za kuaminika zilizopo kuhusu utumizi wa pombe duniani sio rahisi kupatikana na tarakimu zilizopo kwa sasa ni za zamani sana.

Takwimu za shirika la afya duniani zilizotolewa mwaka 2011 zimeangazia sana data kutoka mwaka 2003-2005.

Shirika la afya duniani linapendekeza kuwa zaidi ya asilimia (70.8) ya waafrika hawajagusa hata tone la pombe kwa kipindi cha mwaka mmoja.

"hiyo ni kwa sababu nchi nyingi za Afrika zina waumini wa kiisilamu,'' anasema Boniface Ndirangu mshauri nasaha kwa waraibu wa pombe nchini Kenya.

Hiyo bila shaka ni kinyume na taarifa hii kuwa waafrika wengi wanapenda sana pombe.

Ndio, kuna waafrika ambao ni waraibu wa pombe.

Boniface Ndirangu, ana visa vingi vya kusimulia kuhusu ulevi mwanzo yeye mwenyewe alikuwa mraibu.

"pombe imekuwa njia pekee ya watu kujiliwaza baada ya kazi zao , njia pekee ya kujiondoa kwenye mawazo ya umaskini na ukosefu wa ajira,'' anasema Boniface

Analaumu aina mbali mbali ya pombe ambazo ni kali , zina bei nafuu na kwa maoni yake ni hatari sana.

''Kwa dola moja tu unaweza kulewa chakari na hata kuwalewesha wenzako wawili au watatu'' anasema Ndirangu.

Lakini visa kama hivi havimaanishi kuwa ni Kenya pekee ambayo ina walevi , bara zima lina tatizo la ulevi. Lakini Kenya ndiyo iliyoangaziwa sana na taarifa ya jarida la Time.

Pombe pia huuzwa katika baadhi ya nchi za kiisilamu mfano Misri

Kwa mujibu wa takwimu za shirika la afya duniani, kote duniani kila mwaka kiwango cha pombe ambacho mtu mmoja anakuntwa kwa mwaka mmoja ni lita 6.13. Cha kuzinggatiwa hapa ni kila mtu mmoja aliye na zaidi ya umri wa miaka 15.

Barani Afrika kiwango hicho ni lita 6.15, milimita 20 zaidi ya kiwango kinachotumiwa duniani kila mwaka kwa kila mlevi. Hiyo ni zaidi ya milimita hamsini za pombe aina ya Whisky kila mwaka .

Nchini Kenya licha ya kuwa asimilia 85 ya wananchi hawanywi pombe, waliokunywa walikunywa kupita kiasi, kwa mujibu wa taarifa hiyo.

Zaidi ya hayo, ripoti ya shirika la afya duniani, iliziwacha nje nchi saba za Afrika kwa sababu ya kuwa na waumini wa dini ya kiisilamu, ambako pombe inadhibitiwa au imepigwa marufuku.

Ikiwa hizi nchi zingine zingejumuishwa kiwango cha ulevi Afrika kingekwenda chini.

Ulaya mlevi hutumia lita 12.18 za pombe kila mwaka ikiwa mara dufu ya kiwango kinachotumika Afrika. Sasa je kwa nini Afrika isemekane kuwa na tatizo la ulevi?

Kulingana na shirika la afya duniani, mraibu wa pombe ni yule anayekunywa zaidi la gramu sitini au zaidi ya pombe halisi kwa wiki na hii ni chupa tatu za pombe nchini Uingereza

Wakati shirika la WHO, lilipoangalia vipindi ambavyo watu hulewa mfano mara fulani kwa wiki, na ikumbukwe kuwa Afrika hina walevi wengi, ilipatikana kuwa katika bara la Afrika, walevi hunywa pombe nyingi kwa wiki kuliko mahala pengine popote duniani ikisemekana kuwa mara dufu ya hali nchiniUingereza.

Mfano nchini Kenya, walevi sio wengi lakini wanaolewa wanakunywa pombe nyingi sana.

Bila shaka kwa kutathmini takwimu, tunajiacha tukihoji kwa nini Afrika isemekane kuwa na walevi wengi? bila shaka ripoti hii inawaacha wengi na shaka ikiwa utafiti huu ni kweli kwamba Afrika ina waraibu wengi wa pombe.

Lakini kwa undani ni sawa kusema kuwa ndio walevi wa Afrika wanakuvywa pombe nyingi