WW1:Mashujaa wa Kenya waliosahauliwa

Image caption Munene analalamika babu yake alishiriki vita vya kigeni

Jamaa za wakenya waliopigana kwa upande wa Uingereza wakati wa vita ya kwanza ya ulimwengu wamesahauliwa.

Karne moja baada ya vita hiyo kuanza.

Mwanahabari wa BBC Emmanuel Igunza alizuru mji wa Taveta kulikopiganiwa vita hiyo.

Othiniel Mnene anatembea taratibu akielekea kwa kaburi lililoko pembezoni mwa eneo la makaburi linalotumiwa na jamii ya hapa.

Anapitia njia iliyobetabeta na kukaa chini, na kuonesha kaburi moja.

“Lile ni kaburi la babu yangu. Hakuwa nilivyomfahamu aliporejea kutoka vitani,” ananiambia.

“Aliuliza mara kwa mara kwa nini Waafrika walihusika kwenye vita hii ambayo haikuwa yao.”

Babuye bwana Mnene, Jeremiah Folonja, alikuwa jasusi wa Uingereza katika mji wa Taveta, lakini alikuwa kati ya kundi la Wakenya walionaswa na wanajeshi wa Ujerumani na kupelekwa jela Tanganyika, Tanzania ya leo, iliyokuwa koloni ya Ujerumani.

Image caption James Wilson anapigania kutambuliwa kwa wapiganaji wa Kiafrika

“Papa hapa, Taveta, kuna makaburi ya Wajerumani, Waingereza, na hata wanajeshi wa Ki-Hindi.

Makaburi ya Waafrika yako wapi?

Kwa nini hatuwezi kuwa na nakshi mahala hapa kwa ajili ya kuwakumbuka?” anasema.

Takriban Waafrika milioni mbili wanaaminiwa kuhusika kwenye vita hiyo, iliyokuwa vita ya muda mrefu zaidi Afrika Mashariki.

Wengi walichukuliwa na kujiunga na jeshi, lakini wengi kati yao walikuwa wabeba mizigo waliobebea Wajerumani na Waingereza silaha, vyakula na mahitaji mengine.

Kampeni ya Shamba

Katika mji wa Taveta, kilomita 200 kutoka mji wa Mombasa, kuliko sasa uga mkubwa ulio wazi, kulikuwepo eneo la mkutano la watu hao.

Lakini kumbukumbu za historia hazikurekodiwa vyema na wenyeji au serikali ya Kenya.

James Wilson, Muingereza kwa asili, mwandishi wa “Guerillas of Tsavo,” anasema mengi yanahitajika kufanywa ili kuhifadhi kumbukumbu za Waafrika waliopigana kwenye vita hiyo.

"Tumeungana na viongozi wa mashinani, na marafiki kutoka Uingereza, katika harakati ya kuimarisha nakshi katika mji wa Taveta, itakayoashiria kuwakumbuka Waafrika waliofariki wakipigania Uingereza na Ujerumani,” anasema bwana Wilson, ambaye ameishi Kenya tangu mwaka 1947.

Hatua chache kutoka tunakosimama katika eneo la makaburi la Taveta, kuna jumba kubwa lililochakaa.

Jumba hilo lilikuwa kituo cha maafisa wa polisi karne moja iliyopita.

Sasa jumba hilo ni makao ya walinzi wa gerezani.

'Eneo lenye umuhimu'

Image caption Baadhi ya vitu vilivyopatikana katika eneo la vita

Ni hapa, siku 11 baada ya vita ya kwanza ya ulimwengu kutangazwa huko Ulaya, afisa wa serikali wa Uingereza alifyatua risasi na kumuuwa mwanajeshi wa ki-Jerumani.

“Kwa jinsi fulani, huenda risasi hiyo iliashiria mwanzo wa kampeni ya mashamba Afrika Mashariki,” anasema bwana Wilson.

Lakini kampeni hiyo ilikuwa imeanza hapo awali- tarehe 8 Agosti 1914 waIngereza walitekeleza shambulizi la bomu dhidi ya Dar es Salaam, ambayo kwa wakati huo ilikuwa mji mkuu wa Afrika Mashariki ya Kijerumani.

Takriban watu 100,000 waliuwawa Afrika Mashariki kufuatia vita hiyo.

Eneo mojawapo kubwa kulikopiganiwa vita hiyo nchini Kenya ni Mlima Salaita ulioko Taveta.

Wanajeshi wa Uingereza na wa Jumuiya ya Madola walijaribu kuchukua utawala na kudhibiti mlima huo mara tatu, lakini juhudi zao hazikufua dafu.

"Hili lilikuwa eneo lenye umuhimu. Lilikuwa kama kifuniko cha chupa ya mvinyo, katika Afrika Mashariki ya Kijerumani, iliwabidi kuchukua Mlima Salaita,” bwana Wilson anasema.

"Mapigano hapa hayakuwa kama vita ya Ulaya.

Vita ya Ulaya ilikuwa kubwa na ya muda mrefu, kati ya majeshi yaliyojipanga, lakini hapa kulikuwepo na mapigano madogo madogo ya mara kwa mara.

Image caption Moja ya makaburi ya wazungu Pwani ya Kenya

Nia kubwa ya Wajerumani ilikuwa kuvuruga miundomsingi iliyokuwepo Afrika Mashariki ya Kiingereza; nchini Kenya, hususan reli,” anaongezea.

Mlima Salaita bado una ujenzi wa majeshi ya Kijerumani.

Japo kumbukumbu za historia hazikurekodiwa vyema na wenyeji, majina ya kimafumbo ya maeneo ya hapa yana maana fiche kutoka ziku za awali- kuna Mlima Salaita (Salaita lililotoholewa kutoka kwa “Slaughter”), eneo lililoko kati ya Mlima Kilimanjaro na Milima ya Pare.

Halafu kuna Maktau (lilitoholewa kutoka kwa “marktime”) linalodokeza operesheni za kijeshi, na Mwashoti (lililotoholewa kutoka kwa “corruption of more shots”).

Ugunduzi wa silaha za kijeshi vichakani hivi majuzi, kumeongezea wagivu wa eneo hilo.

Kati ya vitu vilivyogunduliwa, kuna silaha za kijeshi, zenye tarehe ya utengenezaji ya mwaka 1914, bia maalum, chupa za jusi, sare za majeshi ya Uingereza, vifungo na vibweta vya wino vilivyotumika- vyote vikikisiwa kuwa vya karne moja iliyopita.

Image caption kenya ilitawalwa na mabeberu hadi mwaka wa 1963

"Kuna habari chache kukusiana na vita ya ulimwengu iliyopiganiwa humu nchini, Kenya.

Ilhali, ilikuwa vita ya muda mrefu zaidi, na iliendelea hata baada ya kusitishwa kwa vita ya Ulaya kwa muda,” bwana Wilson asema.

Majeshi ya Ujerumani yalizidi kuthibiti maeneo kadhaa baada ya mkataba wa amani kutiwa saini huko Ufaransa- Kamanda wa Ujerumani, Luteni-kanali Paul Emil von Lettow-Vorbeck alipokea taarifa kuwa ujerumani imeshindwa kupitia ujumbe wa simu ya maandishi, tarehe 14 Novemba 1918, na ilichukua muda wa siku tisa kupeleka vikosi vyake kupatana na vikosi vya Uingereza na kujisalimisha rasmi.