Watoto wasajiliwa kuwa wanajeshi Sudan K

Image caption Watoto wanajeshi

Kiasi cha watoto wapatao 11,000 wamesajiliwa kupigana katika makundi yaliojihami nchini Sudan kusini likiwemo jeshi la serikali SPLA. Watoto wenye umri wa kuanzia miaka minane, wamekuwa wakitumika katika mapigano sio tu katika mzozo wa sasa wa kisiasa, lakini kwa miongo mitano ya vita vya kiraia vilivyoshuhudiwa dhidi ya Sudan kaskazini.

Shule moja katika mji wa Bentiu haina wanafunzi na badala yake ni silaha nzito za maafisa wa jeshi la serikali wanaopigana vita vinavyoendelea nchini ambao wanalala katika shule hiyo.

Lakini miezi kadhaa iliyopita waasi walifika katika shule hiyo na kuwachukua kwa lazima wanafunzi wapatao mia darasani mwao.

'Steven' ana umri wa miaka 16 na anaishi katika kambi ya Bentiu.

Yeye na wenziwe wanne wamelazimishwa kupigana vita katika mzozo uliopo nchini.

'David' mwenye umri wa miaka 15 anasema wakati kikosi cha jeshi kilipowasili shuleni mwao aliwauliza ni kwa nini inambidi akapigane - jibu alilopewa, ni lazima apigane kulilinda kabila lake.

Image caption watoto wanajeshi

Anasema kikosi alichokuwemo kilikuwa na idadi kubwa ya watoto.

Paul amesema, 'Mimi na watoto wengine mia mbili tulipelekwa katika kambi ya mafunzo ya kupigana, na iwapo hatukuyashika tuliofunzwa, tuliishia kupigwa na hata mara nyengine tulikaa siku mbili bila ya kula chakula'.

Watoto hawa ni miongoni mwa wengine waliofanikiwa kutoroka katika kikosi walichosajiliwa, na sasa wanaishi miongoni mwa watu wengine wapatao elfu hamsini katika kambi kubwa nchini Sudan kusini- Bentiu.

Msimu wa mvua umesababisha mafuriko katika eneo zima la kambi ya Bentiu.

Licha ya hali duni ya maisha katika kambi hiyo, watoto hao wanasema wako radhi kukabiliana na hayo kuliko kutoka nje na kukabiliwa na hatari kubwa zaidi kwa uhai wao.

Mashirika ambayo yamekuwa yakikabiliana na tatizo hili la watoto kusajiliwa katika makundi yaliojihami, wanasema watoto hawa wanakabiliwa na hali ngumu wanapotumiwa vitani.

Sylvester Ndorbor wa shirika la Unicef anasema, "Baadhi yao wanajeruhiwa, wanapigwa, wakijaribu kutoroka wengine wanauawa, wanatumiwa vibaya kwa kweli ".

Licha ya kwamba serikali imeuahidi Umoja wa mataifa mnamo mwezi Juni mwaka huu haitowashirikisha watoto katika jeshi, bado tatizo hili linadhihirika katika baadhi ya miji inayokumbwa na mzozo nchini.

Msemaji wa jeshi nchini Sudan kusini Kanali Philip Aguer amesema, ' Vita vimezuka wakati tupo katikati ya zoezi la kuwakagua watoto kuwatoa katika jeshi. Tunakubali wajibu wetu kwa sababu wao ni sehemu ya SPLA na tunahakika watakaguliwa na kuachiliwa huru'.

Kuna maelfu ya wanawake nchini Sudan kusini wanaoendelea kunung'unika kwa kutojua mahali walipo watoto wao, baada ya kulazimishwa kuushika mtutu wa bunduki.