Ujangili tatizo Kusini mwa Sahara

Haki miliki ya picha Getty
Image caption Tembo wanyama ambao wapo hatarini dhidi ya ujangili

Wadau wa masuala ya utalii kutoka nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara wamesema kuwa vitendo vya ujangili ni moja ya kikwazo kikubwa katika maendeleo ya sekta ya utalii katika nchi za ukanda huo.

Katika mdahalo ulioandaliwa na kampuni ya Hospitality Round Table (HRT), na kufanyika mjini Dar es Salaam,katika ukumbi wa JNICC, wadau hao wamesema kuwa Tanzania ni moja ya nchi ambazo zinaongezeko la wageni wanaokuja kwa lengo la utalii kwa mjibu wa utafiti wa mashirika yanayojishughulisha na uingizaji wageni katika Mahoteli, ambao ni watalii,kama lilivyo kwa shirika la kimataifa la Jovago, idadi ya wageni hao imeongezeka.

Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii Tanzania Dr. Adelhelm Meru, akizungumza katika mkutano huo anasema idadi ya Hoteli kwaajili ya watalii zimeongezeka pia nchini Tanzania,lakini suala la ujangili analitaja kama moja ya vikwazo na vinadhoofisha utalii.

Andrea Guzzoni mdau wa masoko ya hoteli kutoka kampuni ya Jovago Tanzania, anasema sekta ya utalii katika nchi za kusini mwa jangwa la Sahara kwa mwaka jana na mwaka huu imeboreshwa tofauti na miaka 10 iliyopita.

Image caption Andrea Guzzoni, Meneja mkazi wa kampuni ya JovagoTanzania

Kwa mjibu wa Andrea Guzzoni, Meneja mkazi wa kampuni ya JovagoTanzania ni kwamba utalii unaweza kukuza pato la taifa kwa zaidi ya asimia 10 ya pato la taifa Dunia nzima, lakini baadhi ya nchi kutoka bara la Ulaya, Marekani na Asia ndio wanaoongeza pato hilo kwa kiasi kikubwa.

Hata hivyo Kusini mwa Jangwa la Sahara haijafikia kiwango kizuri kutokana na majanga kama njaa, ubovu wa miundombinu, kiwango cha chini cha Afya na uwezo mdogo wa elimu katika sekta ya utalii

Kutokana na ripoti iliyotolewa na Global Travel and Tourism ya mwaka 2015, inaonyesha nchi zinazoshika nafasi 10 bora ndani ya sekta ya utalii ni kutoka Marekani, Ulaya, na Asia. Afrika kusini imeshika nafasi ya 48, Namibia nafasi ya 70, Kenya ya 78 na Tanzania ni ya 93 kati ya nchi 141 Dunia nzima.