Washindi

Jane Mweni, mshindi wa Faidika mwaka 2009
Image caption Jane Mweni, mshindi wa Faidika mwaka 2009

Faidika na BBC 2009 ina malikia mpya, Bi Jane Mweni, raia wa Kenya ambaye aliwabwaga washindani wenzake watano kwenye fainali zilizofanyika Mombasa tarehe 13 Agosti 2009.

Bi Mweni ambaye anasubiri matokeo ya mitihani yake ya elimu ya diploma, aliwasilisha mchanganuo wa kuanzisha biashara ya kuzoa katika jiji la kitalii la Mombasa ambako anaishi.

Akizungumza baada ya kutangazwa mshindi, Bi Mweni alibainisha kuwa ameishiwa maneno kutokana na furaha ya ushindi: "Nimeishiwa maneno....hapa nilipo natetemeka!"

Vijana sita walifuzu kuingia katika fainali za 2009. Washindani mwaka huu walikuwa Nyota Anjelique Kikukama kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Chiza Bonye wa Burundi, Hakizimana Aladin aliyeiwakilisha Rwanda, Gakuo Roy wa Uganda, Mbaraka Juma kutoka Tanzania na wenyeji Kenya waliibuka kidedea baada ya ushindi wa Jane Mweni.

Mshindi alijizolea dola elfu tano za kimarekani (US$ 5,000) pamoja na kikombe. Vile vile atapata fursa ya kusafiri kwenda visiwa vya Trinidad na Tobago (Caribbean) ambako atahudhuria kongamano la vijana katika mkutano wa viongozi wa Jumuiya ya Madola mwezi Novemba 2009.

Walengwa wa shindano hili ni vijana wenye umri kati ya miaka 16 hadi 24 na kwamba washiriki wanapaswa kuandika mchanganuo wa aina ya biashara ambao utafafanua jinsi watakavyoiendesha kwa bajeti ya fedha ambazo zitatolewa kama zawadi ya kwanza.

Hakika shindano hili tangu kuanzishwa kwake miaka kadhaa limekuwa likivutia wasikilizaji wetu wengi, na hata katika fainali wageni wa heshima wamekuwa wakiipongeza BBC kwa shughuli pevu kama hiyo. Baadhi wamekuwa wakiomba shindano kama hili lirudiwe, na sisi bila hiana, tumefanya hivyo.

Kwa mashabiki wa Facebook sasa wanaweza kufuatilia mambo ya Faidika na BBC 2009. Jiunge nasi usikie wenzako wanasema nini.

Image caption Ashura Kisesa, mshindi wa Faidika na BBC 2008

Ashura Kisesa, raia wa Burundi, wakati huo akiwa na umri wa miaka 24, ndiye aliibuka mshindi wa Faidika na BBC 2008. Alikabidhiwa zawadi ya juu ya shindano hilo na Waziri mkuu wa Uganda, Bw Apolo Nsibambi.

Bi Ashura alikabidhiwa tuzo maalum pamoja na hundi yenye thamani ya dola elfu tano za Marekani, ili aweze kuanzisha mradi wake wa kujenga vyoo vya kulipia, katika miji ya Afrika Mashariki na Kati.

Ashura Kisesa, alikuwa msichana pekee aliyeingia kwenye fainali hizo, zilizorushwa moja kwa moja, kupitia BBC Idhaa ya Kiswahili na Televisheni ya UBC, aliwashinda vijana wengine wanne, kwa kuwashawishi majaji na jinsi atakavyotumia fedha za zawadi kuanzisha mradi wenye mafanikio na kunufaisha jamii inayomzunguka.

Akizungumza katika hafla hiyo, Waziri Mkuu wa Uganda, Profesa Apolo Nsibambi alisema “ Wakati shindano hili likianzishwa mwaka jana, hawakuwepo wasichana katika fainali, hivyo natoa pongezi kwa Ashura. Natoa wito kwa BBC kuchukua hatua thabiti kuhimiza wanawake zaidi kuingia katika biashara. Hii ni jitihada nzuri ya BBC ya kusaidia vijana kuwa wabunifu na kuwafanya wawe waundaji wa nafasi za kazi, badala ya kuwa watafutaji kazi.”

Wakati akiingia fainali Bi Ashura alikuwa mwanafunzi wa uchumi wa kilimo (agronomia) katika chuo kikuu cha Burundi.

Ashura alishiriki katika shindano la Faidika na BBC 2007 lakini hakupata mafanikio. Hatimaye ndoto hiyo ilitimia kwa Ashura kutokana na kuibuka mshindi wa jumla wa Faidika na BBC 2008, kwenye fainali iliyoungura Kampala, Uganda.

Image caption David Ssegawa, mshindi wa kwanza wa Faidika na BBC mwaka 2007

Mwaka 2007 ilikuwa mara ya kwanza kufanyika mashindano ya Faidika na BBC. Takriban michanganuo zaidi ya 5,000 iliwasilishwa kutoka Afrika Mashariki na Kati.

Vijana wawili, Francis Wakara Baraka na Geofrey Kibiki, kutoka Tanzania, Arthur Buliva kutoka Kenya na David Ssegawa kutoka Uganda, waliingia kuchuana fainali.

Baada ya mchuano mkali wa kukata na shoka, hatimaye majaji Zablon Karingi Muthaka kutoka Kenya, Humphrey Polepole kutoka Tanzania na Halima Abdallah kutoka Uganda wakamchagua David Ssegawa kuwa mshindi.

Washiriki watatu waliongia fainali, Francis Baraka na Geofrey Kibiki wa Tanzania na Arthur Buliva wa Kenya walizawadiwa fedha taslimu na simu za mkononi kila mmoja.

Fainali hiyo ilirushwa moja kwa moja kupitia BBC Idhaa ya Kiswahili, kutoka Jijini Dar Es Salaam, Tanzania, kwenye mtandao bbcswahili.com na vilevile kupitia kituo maarufu cha televisheni nchini Tanzania ITV na pia EATV kinachorusha matangazo yake katika eneo la Afrika Mashariki na Kati.

Mashindano ya Faidika na BBC yalifanyika kwa mara ya kwanza kama sehemu ya maadhimisho ya miaka 50 tangu kuanzishwa kwa Idhaa ya Kiswahili ya BBC.