MAtukio

Tarehe 14 Agosti 2009

Jane Mweni ndiye mshindi wa Faidika na BBC 2009! Alifanikiwa kubeba taji hilo baada ya kuwabwaga wenzake watano katika fainali kali iliyofanyika Mombasa nchini Kenya, tarehe 13 Agosti 2009.

Bi Mweni ambaye ni mkazi wa Mombasa anakuwa mkenya wa kwanza kushinda shindano hilo tangu lilipoanzishwa mwaka 2007 na kufanyika kwa mara ya kwanza nchini Tanzania.

Picha za Faidika na BBC

Tarehe 12 Agosti 2009

Mambo yamekwishawiva, vijana wajasiriamali wako Mombasa wakijiandaa kwa kivumbi cha fainali itakayofanyika Alhamisi, 13 Agosti 2009.

Tarehe 15 Julai 2009 - Mshindi wa Burundi apatikana

Image caption Ciza Bone wa Burundi

Mshindi wa fainali ya Burundi ni Ciza Bone, mwenye umri wa miaka 23 kutoka mkoa wa Makamba. Mchanganuo wake ni kutaka kufanya biashara ya kutoa mbegu bora za zao la muhogo. Anajiandaa kuchuana katika fainali kuu mjini Mombasa, 13 Agosti 2009.

Tarehe 13 Julai 2009

Mshindi wa Kongo apatikana!

Image caption Nyota Angelique wa Congo

Katika fainali ya kitaifa huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, mwanadada Nyota Angelique, mwenye umri wa miaka 23 ndiye aliibuka mshindi. Angelique ataungana na washindi kutoka Kenya, Uganda, Tanzania, Rwanda na Burundi katika fainali ya Faidika na BBC 2009 itakayofanyika Mombasa nchini Kenya tarehe 13 Agosti 2009.

Tarehe 23 Juni 2009

Muda umeongezwa! Muda umeongezwa! Mwisho ya kupokea michanganuo ni tarehe tatu Julai 2009, badala ya 30 Juni iliyokuwa imepangwa awali. Muda umeongezwa kutoa nafasi kwa wale ambao walikuwa bado hawajapata taarifa za shindano la Faidika na BBC 2009.

Mambo yanaenda yakiongezeka. Tunapenda kuwafahamisha vijana wanaoshiriki kuwa mshindi wa Faidika na BBC 2009 pia atapata fursa ya kusafiri kwenda visiwa vya Trinidad na Tobago (Caribbean) ambako atahudhuria kongamano la vijana katika mkutano wa viongozi wa Jumuiya ya Madola mwezi Novemba 2009.

Tarehe 10 Juni 2009

Faidika na BBC imezindua ukurasa wa Facebook kuwezesha mawasiliano zaidi kati ya washiriki wa shindano hili.

Hapa utaweza kupata ushirikiano wa mawazo na maswala mengineyo yatakayokuwezesha kuandaa mchanganuo maridadi, unaoweza kukupa ushindi.