Kuhusu Faidika na BBC

Faidika na BBC ni shindano lililobuniwa na BBC kama njia moja ya kuwazawadi wasikilizaji wetu na pia kuwatia hamasa vijana pamoja na wasikilizaji ili wawe na moyo wa ujasiriamali. Shindano hili lilianza kama shindano la wasikilizaji wetu walio na umri kati ya miaka 16 na 24.

Washiriki walihitajika kuwasilisha maandishi yenye manene 1500 kuhusu mpango wa kibiashara katika lugha ya Kiswahili na mshindi alichaguliwa kutoka kila taifa lililokuwa likishiriki. Washindi walishiriki katika kinyang’anyiro cha zawadi kuu ya $5000 na kompyuta ndogo au laptop. Hata hivyo sura ya Faidika na BBC inabadilika.

Tangu kuasisiwa mwaka 2007, washiriki wa shindano la Faidika na BBC wameongezeka kutoka takriban 5000 mwaka 2007 hadi washiriki 10,000 mwaka 2009.

Kila mwaka wa shindano hilo, tulipokea maoni mzuri kutoka kwa wasikilizaji wetu na kutokana na hili tumepata moyo wa kuliboresha hata zaidi shindano la Faidika.

Mwaka 2010, usimamizi wa BBC uliamua kubadili zawadi tunazotowa kwenye faidika na BBC. Tumebuni mpango utakaowashirikisha wasikilizaji wetu ambapo tunatoa ushauri kuhusu njia zote za kuendesha biashara ikiwa ni pamoja na mipango ya kibiashara, bajeti na kadhalika. Pia tumebuni pia blogu kwenye mtandao wa internet ambapo washiriki wanaweza kujadili maswala mbali mbali yanayowahusu Lengo kuu la Idhaa ya Kiswahili hivi sasa ni kukuza asasi yenye kutegemewa kwenye tovuti ambapo wasikilizaji wetu wataweza kutuma mwaka mzima na wala sio wakati wa shindano pekee.

Shindano hili linarejea hivi punde kwa hivyo tega sikio na pia angaza macho…