Kuhusu Kimasomaso

Kipindi cha Kimasomaso kilitokana na mradi wa pamoja kati ya BBC na shirika la IPPF (International Planned Parenthood Federation) uliojulikana kama Sexwise.

Mradi huo wa Sexwise ulitoa habari kuhusu afya ya uzazi na afya bora ya watu binafsi pamoja na kuwapa njia tofauti za kufanya maamuzi na kuwajulisha haki zao. Wanaharakati wengi kutoka sekta ya maswala ya afya ya uzazi mashinani walihusishwa.

Kutokana na uhusiano huu na vijana wa Afrika Mashariki pamoja na wataalamu wa kiafya ikifuatiliwa hatimaye na uandaaji wa kipindi cha Sexwise katika lugha ya Kiswahili, shirika la BBC World Service Trust liling’amua umuhimu wa kuandaa makala ya kipindi kinacholenga vijana wa eneo hili ambayo ingepeperushwa hewani kila wiki katika idhaa ya Kiswahili ya BBC.

Umuhimu wa Kimasomaso

Afrika Mashariki, kwa mfano, ilikuwa jambo la kuvutia kukutana na vijana wakifanya kazi kama waelimishaji rika katika kituo cha vijana cha Eastleigh, jijini Nairobi. Waelimishaji hawa, walihisi kwamba ukosefu wa elimu kuhusiana na mambo ya kijinsia pamoja na dhana husika ndiyo iliyokuwa changamoto kubwa inayofaa kukabiliwa.

Kwa maoni yao, maswala muhimu zaidi yanayowahusu vijana katika Afrika Mashariki, hasa katika nyanja ya afya ya uzazi, ni ukosefu wa elimu madhubuti kuhusu afya ya uzazi, ukosefu wa ujasiri na uzoefu katika kujadili na kufanya uamuzi kuhusu mahusiano na kuelewa jinsia zao, magonjwa ya zinaa, mimba za mapema na uavyaji mimba au abortion.

Ili kupiga hatua yoyote muhimu, ni lazima kufahamu na kukubali kwamba swala la afya ya uzazi siyo tu swala la kiafya pekee. Kwa kiasi kikubwa ni kuhusu umaskini, ukosefu wa usawa wa kijinsia na mila, na ni mkusanyiko wa maswala haya kunakochangia uelewa wa watu kuhusu ujinsia wao, ambayo kwa wengi ni mwiko.

Katika tajiriba yetu, upendo mkubwa na imani inayohusishwa na usikilizaji wa redio unaweza kutumiwa kutoa jukwaa mahsusi la kujadili kwa undani maswala nyeti na mazito yanyayohusiana na afya ya uzazi.