Wavulana na kubalehe

Ni nini kinachotokea kwa wavulana?

  • Kifua chako na mabega hukua na kutanuka kwa haraka.
  • Nywele nywele huota kama kifuani na miguuni, kwengine zikawa nyingi hasa kwenye makwapa na kuzunguka uume wako (hizi huitwa mavuzi).
  • Ndipo pia kidevu kinapotokea
  • Uume na makende yako hukua na kuongezeka ukubwa
  • Makende huanza kuzalisha manii (shahawa)
  • Umme wako utaanza kutoa manii, jambo hilo linaweza kutokea katika ndoto wakati umelala usingizi.
  • Unaweza kusimika bila tahadhari. Hili laweza kuwa jambo la kuaibisha na kutia wasiwasi, lakini mara nyingi hakuna mtu anayeweza kugundua.
  • Sauti yako nayo itaanza kuwa nzito

Je niko sawa?

Mambo kadhaa yanayowatatanisha wanaume.

Tuanze na mwili wako.

Kama tulivyosema wengine wetu hupata wasiwasi kuhusu miili yetu, hasa wakati huo wa kubaleghe, kwa vile kunatokea mabadiliko ya kasi mno.

Pia wasiwasi huo huongezeka kunapokosekana maelezo kuhusu hali hiyo na huku muhusika anaona haya kujadili swala hilo.

Tunajua katika tamaduni nyengine ni mwiko kuzungumzia maumbile yetu ya sehemu za siri na hasahasa maswala ya ngono kwa kurahisha mambo basi hapa tuna maswali na majibu kwa maswala yanayohusu viungo vyetu vya uzazi ambayo mara nyingi hutatanisha.

Tunatumai yatakuondolea hofu na kukutuliza.

1. Nisaidie! Mbona mimi uume wangu hauonekani kuwa sawa?

Habari njema ni kwamba hakuna kitu kama uume (yaani mboo) iliyo sawa.

Kwa hakika kuna maumbo na ukubwa unaotofautiana wa kiungo hiki cha uzazi.

Ni jambo la kawaida kwa mfano, kwa uume kupinda kidogo upande mmoja. Ukubwa kadhalika huwa swala linalozusha wasi wasi – lakini kumbuka iwe ni swala la ukubwa au udogo, urefu au ufupi hiyo si hoja, kwa kawaida mboo hizo zinazofautiana kwa ukubwa huwa karibu saizi moja wakati wa kusimika.

Kwa kawaida uume wa mtu mzima, wakati umepwaya huwa na urefu wa sentimita kati ya 6 na 10. Lakini wakati wa kusimika huwa na karibu urefu wa sentimita kati ya 12 na 19. Wavulana wenye umri wa miaka 12 nao huwa na uume wa urefu wa sentimita 3 hadi 6 wakati umepwaya yaani ukiwa katika hali ya kawaida, na urefu wa chini ya sentimita 8 unaposimama.

2. Siwezi kudumisha kusimika – nina kasoro?

Mara nyingi vijana hukumbwa na tatizo hili kwa sababu za kisaikologia tu! Yaani inatokea wakati unapokuwa na wasiwasi, mfadhaiko au kuchanganyikiwa hasa kwa wale wanaofanya mapenzi kwa mara ya kwanza.

Kwa bahati mbaya kila hali hiyo inapozidi ndivyo inakuwa vigumu kusimika tena, na hivyo basi kusababisha mfadhaiko zaidi.

Jaribu kutokuwa na pupa wakati wa kufanya mapenzi, kuwa mtulivu na jipe mda wewe na mpenzi wako. Itasaidia sana pia kujadili swala hilo na mpenzi wako.

3. Mbona mimi wakati nimesimika na kufikia kilele manii yangu hayatoki kwa nguvu yanamiminika polepole tu? Je hali hiyo itaathiri uwezo wangu wa kupata watoto,kumtosheleza mpenzi wangu kimapenzi, na kudumisha kusimika ili nimridhishe mpenzi wangu?

Nguvu za kutoa manii zinatofautiana. Rekodi kubwa iliyowekwa ya kurusha manii ni mita tano (kwa hivyo kama unataka kujaribu kuvunja rekodi hiyo, hakikisha umo katika chumba kirefu na una futi ndefu ya kupimia!). Lakini usiwe na shaka kama rekodi hiyo umeshindwa kuivunja.

Ukweli ni kwamba kiwango cha manii kinachotoka uumeni kwa kawaida huwa ni kiasi cha kijiko kimoja kidogo cha chai.

Manii hayo huwa na mamilioni ya mbegu za kiume, hivyo hata kama yatatoka kwa kumiminika, kutiririka au kwa matone, na kwa upole gani hakutaathiri uwezo wako wa kutunga mimba mwanamke mradi tu mbegu hiyo imekutana na yai la mwanamke.

Hivyo utaweza kupata watoto kwa njia ya kawaida. Na wala hali hiyo haitatatiza uwezo wako wa kumridhisha mpenzi wako.

4. Makorodani yangu hayajashuka ilhali nina umri wa miaka 15. Nifanyeje?

Hali hiyo kwa kingereza huitwa "undescended testes", yaani makorodani ambayo hayajashuka kutoka kinenani na kuingia kwenye kifuko chake ambapo ndio huwa makende kamili.

Hili ni tatizo ambalo hutokea uchangani, na kwa kawaida hugunduliwa kabla mtoto hajaingia ujanani. Labda kinachofanyika ni kwamba makorodani yako hayajakua na kufikia ukubwa unaofaa, na hili ni jambo ambalo hutokea wakati wa kubaleghe.

Wakati huo wa kubaleghe, makende na uume hukua, sambamba na kufanyika kwa mabadiliko mengine mwilini, kama vile sauti kuwa nzito na kifua kutanuka.

Wavulana wengi hubaleghe kati ya umri wa miaka 11 na 17, kwa hivyo jipe mda. Kuwa mvumilivu, na mwili wako utakupa ishara unazosubiri.