Got a TV Licence?

You need one to watch live TV on any channel or device, and BBC programmes on iPlayer. It’s the law.

Find out more
I don’t have a TV Licence.

Muhtasari

  1. Yahya Jammeh bado hajaondoka madarakani Gambia
  2. Rais wa Guinea Alpha Conde ameenda Gambia kumshawishi kuondoka kwa amani
  3. Majeshi ya Afrika Magharibi yamesema yako tayari kumtoa kwa nguvu
  4. Adama Barrow aliapishwa kuwa rais Alhamisi katika ubalozi wa Gambia nchini Senegal
  5. Wanajeshi wa Senegal tayari wameingia Gambia

Habari za moja kwa moja

time_stated_uk

Jammeh "kuachia madaraka na kuondoka"

Kiongozi wa Gambia Yahya Jammeh atawachia madaraka na kuondoka nchini Gambia, kwa mujibu wa maafisa wanaongoza mapatano. 

Wapatanishi wa Afrika Magharibi walitumia masaa kadha wakikutana na bwana Jammeh siku ya Ijumaa kuzungumzia hatma yake. 

Msafara wa magari uliowabeba marais wa Guinea na Mauritania, umeondoka makao ya Jammeh lakini hayaaminiwi kuondoka nchi humo. 

Bwana Jammeh alishindwa kwenye uchaguzi wa mwezi Disemba na mrithi wake Adama Barrow ameapishwa. 

Wafuasi wa Barrow walishangilia katika nchi jirani ya Senegal
AFP/getty images
Wafuasi wa Barrow walishangilia katika nchi jirani ya Senegal

Barrow: Yahya Jammeh amekubali kuachia madaraka

Rais wa Gambia anayetambuliwa na jamii ya kimataifa Adama Barrow ameandika kwenye Twitter kwamba Yahya Jammeh amekubali kuachia madaraka na kuondoka Gambia.

Msafara wa magari umeonekana ukiondoka ikulu, Banjul. Hata hivyo, haijathibitishwa iwapo Jammeh yupo kwenye msafara huo.

Jammeh amekuwa akifanya mazungumzo kwa saa kadha na marais wa Guinea na Mauritania.

I would like to inform you that Yahya Jammeh has agreed to step down. He is scheduled to depart Gambia today. #NewGambia

Jammeh ataondoka?

Mwandishi wa BBC Umaru Fofana anasema mmoja wa wasaidizi wa karibu wa Rais anayetambuliwa na jamii ya kimataifa Adama Barrow amemdokezea kwamba Jammeh amekubali kung'atuka.

Lakini habari hizo bado hazijathibitishwa.

A close aide to President Adama Barrow, Mai Fatty has confirmed to me that Yahyah Jammeh has agreed to step down. #Gambia.

Awali, zulia jekundu lililokuwa limeandaliwa uwanja wa ndege wa Banjul lilikuwa limeanza kuondolewa na wanajeshi bila kuwepo kwa Jammeh.

Ndege ya Gambia
BBC

Conde na Abdel Aziz wajiandaa kuondoka Gambia

Msafara wa magari umeonekana ukiondoka ikulu ya Gambia. Haijabainika iwapo Jammeh yumo kwenye msafara huo.

Katika uwanja wa ndege wa Banjul, maafisa wameonekana wakijiandaa, ishara kwamba marais Alpha Conde na Mohamed Ould Abdel Aziz wanatarajiwa kuondoka wakati wowote.

Haijabainika iwapo wataondoka na Jammeh.

#Gambia airport protocol getting ready for delegation as #Guinea & #Mauritania presidents have left State House, unclear if Jammeh w/ them..

Barrow anajiandaa kuanza safari?

Rais wa Gambia anayetambuliwa na jamii ya kimataifa Adama Barrow amedokeza kuwa huenda anajiandaa kuondoka Senegal.

Amewashukuru wenyeji wake kwenye Twitter: 

Thank you once again President @Macky_Sall for hosting me and my family twitter.com/pr_senegal/sta…

Jammeh 'anaandika taarifa ya kuondoka'?

  Mwanahabari wa France 24 ameandika kwenye Twitter kwamba kuna uwezekano Jammeh anaandika taarifa ya kukubali kuondoka kwenda Guinea. 

Guinean officials tell @FRANCE24 that Jammeh currently writing statement where he accepts to leave, in the presence of Guinean officials

Barrow na Sall waombea amani Gambia

Rais wa Gambia anayetambuliwa na jamii ya kimataifa Adama Barrow amepakia kwenye Twitter picha yake na rais wa Senegal Macky Sall "wakiombea amani Gambia".

Macky Sall na Adama Barrow
Adama Barrow/Twitter
Macky Sall na Adama Barrow

Muda wapita tena bila Jammeh kuondoka

Yahya Jammeh
AFP

Jammeh alikuwa ameomba apewe hadi saa 16:00 (saa moja jioni Afrika Mashariki) kufanya uamuzi kuhusu iwapo ataachia madaraka au la.

Makataa ya kwanza ya kumtaka aachie madaraka kufikia saa sita mchana yalikuwa yamepita.

Taarifa zinasema makamu wa rais wa zamani wa Gambia, Isatou Njie-Saidy, yupo ikulu ambapo anashiriki mazungumzo ya dakika za mwisho.

Marais wa Mauritania na Guinea wanajaribu kumshawishi Jammeh kuondoka.

"Tutawakaribisha wanajeshi wa Ecowas kwa chai"

Ousman Badjie
Reuters

Mkuu wa majeshi ya Gambia Jenerali Ousman Badjie ameambia Reuters kwamba anamtambua Rais Adama Barrow kama amiri jeshi mkuu mpya amesema hatapigana vita dhidi ya wanajeshi wa kanda wanaotaka kumuondoa kwa nguvu Yahya Jammeh. 

Tutawakaribisha kwa maua na kuwaandalia kikombe cha chai

Huu ni mzozo wa kisiasa. Ni suitafahamu tu. Hatutapigana na wanajeshi wa Nigeria, Togo au wanajeshi wa taifa lolote lile watakaofika hapa.

Jammeh aenda msikitini kwa sala

Mazungumzo yanapoendelea ikulu kati yake Yahyah Jammeh na marais wa Guinea na Mauritania, baadhi ya wanahabari walienda msikitini wakati wa sala ya Ijumaa ulipofika.

Lakini mwandishi wa BBC Umaru Fofana anasema katikati mwa hotuba ya imamu Alhaji Jallow, wanahabari walitakiwa kuondoka safu nne za mbele.

Baadaye walitolewa nje. Mmoja wa walinzi wa rais alimnong'onezea kwamba bila shaka, Jammeh na wageni wake walikuwa wanatarajiwa kuingia msikitini.

Barrow: Jammeh anafaa kuondoka Gambia

Mwanahabari mwenye makao yake Dakar Nicolas Haque anasema amezungumza na Rais wa Gambia anayetambuliwa na jamii ya kimataifa Adama Barrow ambaye amemwambia Yahya Jammeh anafaa kuondoka nchini humo.

WIki iliyopita, Barrow alisema hakukuwa na haja kwa Jammeh kwenda uhamishoni.

Aliahidi kwamba hatashtakiwa na serikali mpya.

Habari za hivi pundeJammeh aomba muda zaidi Gambia

Mwandishi wa BBC Thomas Fessy, ambaye yupo Banjul, anasema Yahya Jammeh, ambaye alikuwa amepewa hadi saa sita mchana (saa tisa Afrika Mashariki) kuachia madaraka, ameomba aongezewe muda. Ameomba apewe hadi saa kumi alasiri saa za Gambia (16:00 GMT).  

Jammeh 'huenda akenda Guinea'

Mwandishi wa BBC Umaru Fofana anasema amewasili ikulu ya Gambia akiandamana na marais wa Guinea na Mauritania.

Muda wa mwisho uliotolewa na Ecowas kwa Jammeh kuondoka madarakani umeongezwa kutoa fursa ya kufanyika kwa mazungumzo.

Fofana amesema duru zinadokeza kuwa kuna uwezekano mkubwa wa Jammeh kuondoka na kwenda Conakry, Guinea leo. Watu wamejitokeza barabarani na wanainua mikono na kuimba "amani".

Jammeh hajafika kumlaki Abdul Aziz

Yahya Jammeh hajafika uwanja wa ndege kumlaki Rais wa Mauritania Mohamed Ould Abdul Aziz. Aidha, hakumlaki mjumbe wa UN Afrika Magharibi.

Habari za hivi pundeWanajeshi wa Ecowas kusubiri mazungumzo

Muda wa Yahya Jammeh kuachia madaraka kwa Amani umepita.

Shirika la habari la Reuters limeripoti kwamba wanajeshi wa Ecowas watasubiri mazungumzo yafanyike kati ya Yahya Jammeh na marais wa Mauritania na Guinea.

Mwandishi wa BBC anasema ndege ya rais wa Mauritania imetua Banjul.

Jammeh ataongezewa muda?

Marais wa Mauritania na Guinea, ambao wanatarajiwa kujaribu kumshawishi, kwa mara ya mwisho, Rais Yahya Jammeh kuondoka kwa amani, wanatarajiwa kuwasili Banjul.

Hii ina maana huenda muda aliopewa Jammeh kuondoka madarakani ukaondoka kutoa fursa kwa mashauriano kufanyika.

Kuna zulia jekundu na magari ya kirais ya Rolls Royce uwanjani Banjul kuwasubiri marais hao, kama unavyoona pichani.

Banjul
BBC
Gari
BBC
Gari
BBC

Habari za hivi pundeNdege ya rais wa Mauritania yatua Banjul

Ndege ambayo inatumiwa na rais wa Mauritania Mohamed Ould Abdel Aziz imewasili uwanja wa ndege wa Banjul. Tayari ni saa sita nchini Gambia, muda wa mwisho uliotolewa kwa Rais Yahya Jammeh kung'atuka.

Marais wanataka kuondoka na Jammeh

Jammeh
AFP/Getty Images

Wanahabari mjini Banjul wanaripoti kuwa marais wa Mauritania na Guinea watamwambia Yahya Jammeh kwamba lazima aondoke nao kwa ndege watakayokuwa wanatumia, la sivyo aondolewa kwa nguvu.

Mwenyekiti wa tume ya Ecowas Marcel de Souza, amesema majeshi ya muungano huo yataingilia kati “asipokubali kuondoka Gambia”.

Jammeh ameahidiwa hifadhi Nigeria na Morocco.

Mke wa Jammeh, Zineb alizaliwa nchini Morocco – babake ni mzaliwa wa Guinea na mamake raia wa Morocco.

Jammeh anadaiwa kuwa bado ikulu na mkewe na mwana wao wa kiume.

Haijabainika hatima ya Jammeh itakuwa gani iwapo atakamatwa na wanajeshi wan chi jirani.

Wiki iliyopita, Barrow aliambia BBC kwamba hakuna haja ya Jammeh kutafuta hifadhi nje ya nchi.

„Twamtaka Jammeh awe Gambia, sidhani anahitaji kwenda nchi nyingine,” alisema.

Alhamisi, msemaji wa Barrow, Halifa Sallah, alisema Jammeh hafai kushtakiwa kwa makosa aliyotekeleza tangu achukue madaraka kupitia mapinduzi yasiyokuwa na umwagikaji wa damu mwaka 1994.

Bw Sallah alisema pia kuwa Jammeh atajivunia hadhi inayopewa viongozi wa zamani.

Jina na sifa nyingi za Yahya Jammeh

Yahya Jammeh anafahamika sana kwa kujilimbikizia sifa. Amekuwa akijiongezea sifa hizo kwenye jina lake rasmi.

Mwaka 2015, alijiongezea  Babili Mansa kwenye jina lake rasmi.

Kulingana na kabila la Mandika jina hilo lina maana ya 'mjenzi daraja mkuu' ama 'mshindi wa mito'.

Jina lake kamili likawa Mtukufu Sheikh Profesa Alhaji daktari Yahya AJJ Jammeh Babili Mansa.

Soma zaidi: Rais wa Gambia aongezewa jina jingine

Watu 45,000 waikimbia Gambia

Raia 45,000 wa Gambia wameikimbia nchi hiyo na kuingia Senegal kutokana na mzozo wa kisiasa unaoendelea, shirika la UN linalowashughulikia wakimbizi limesema.

Taifa jirani la Senegal linaweza kuwahudumia hadi wakimbizi 100,000, msemaji wa UNHCR  Babar Baloch amesema.

45,000 people have arrived in Senegal amid continuing political uncertainty in The #Gambia – @iBabarBaloch

Jammeh atawaambia nini Conde na Abdel Aziz?

Mwandishi wa BBC Thomas Fessy aliye mjini Banjul anasema maandalizi ya kuwalaki marais wa Guinea na Mauritania uwanja wa ndege, Alpha Conde na Mohamed Ould Abdel Aziz.

Wanajeshi uwanjani wanatabasamu na kuonesha urafiki.

Mjumbe wa UN Afrika Magharibi Mohamed Ibn Chambas ambaye amemtaka Jammeh kung’atuka tayari amewasili.

Jijini, kimya kimetanda na biashara nyingi zimefungwa.

Wengi wanaamini mwisho wa mzozo wa sasa wa kisiasa unakaribia lakini wanasubiri Jammeh atawaambiaje marais hao wanaofika kumshawishi kuondoka kwa Amani.

Mwenyekiti wa tume ya Ecowas, Marcel de Souza, amependekeza Jammeh apelekwe Guinea kabla ya hatima yake kuamuliwa.

Mauritania si mwanachama wa Ecowas.

Rais wa Guinea Alpha Conde amekuwa akipinga pendekezo la majeshi kutumia kumuondoa Jammeh. Anasema diplomasia inafaa kutumiwa.

Hakuna aliye tayari kufa kwa ajili ya Jammeh

Waziri wa zamani wa mambo ya nje wa Gambia Sidath Diop ameambia BBC kwamba Bw Jammeh amekataa ushauri wa viongozi wa Afrika Magharibi kwa sababu anaamini wanajeshi watampigania.

Hata hivyo, amesema wanajeshi wengi hawana imani na Bw Jammeh.

"Jammeh anaamini anamili Gambia," amesema Diop, na kuongeza kuwa kiongozi huyo hajui afanye nini utawala wake unapofikia kikomo.

Gambia
BBC

Yahya Jammeh amevunja baraza la mawaziri

Taarifa zinasema Yahya Jammeh amevunja baraza la mawaziri baada ya mawaziri wake wengi kujizulu.

Anapanga kusimamia shughuli zote za wizara za serikali.

Makamu wake wa rais ni miongoni mwa waliojizulu.

Amechukua hatua hiyo siku moja tu baada ya Adama Barrow kuapishwa kuwa rais mpya wa Gambia ubalozini Senegal.

Breaking News: Yahyah Jammeh has sacked the remainder of his cabinet after mass resignations.

Wanajeshi wako tayari kumtoa kwa nguvu

Wanajeshi wa Senegal
AFP
Wanajeshi wa Senegal ni miongoni mwa waliopokea mafunzo zaidi Afrika

Juhudi za mwisho za kumshawishi Bw Jammeh kuondoka kwa hiari, ambazo zinaongozwa na Rais wa Guinea Alpha Conde, zinatarajiwa kufanyika Ijumaa asubuhi.

Mwenyekiti wa tume ya Ecowas, Marcel Alain de Souza, alisema iwapo mkutano huo utakaoongozwa na Bw Conde hautafaulu, basi hatua ya kijeshi itafuata.

"Iwapo kufikia saa sita mchana, yeye (Bw Jammeh) hatakubali kuondoka Gambia chini ya Rais Conde, tutaingilia kijeshi," amesema.

Hatua ya Ecowas kutaka kumtoa kwa nguvu Jammeh inaungwa mkono na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lenye wanachama 15, ingawa baraza hilo lilisisitiza kwamba suluhu ya amani inafaa kupoewa kipaumbele.  

Jammeh ana hadi saa sita mchana kuondoka

Yahya Jammeh
Reuters

Viongozi wa nchi za Afrika Magharibi wamempa Yahya Jammeh fursa ya mwisho kuachia madaraka, huku wanajeshi wa Senegal wakiingia nchini Gambia.

Bw Jammeh amepewa hadi saa sita mchana Ijumaa (saa tisa Afrika Mashariki) kuachia madaraka la sivyo aondolewe kwa nguvu na wanajeshi wa nchi za Afrika Magharibi wanaoungwa mkono na Umoja wa Mataifa.

Wanajeshi hao wametakiwa kusubiri hadi makataa hayo yamalizike.

Jumuiya ya Kiuchumi ya nchi za Afrika Magharibi (Ecowas) inaunga mkono Adama Barrow, ambaye aliapishwa kuwa rais mpya wa Gambia katika ubalozi wa nchini hiyo nchini Senegal.

Soma zaidi:Jammeh apewa makataa ya mwisho 

Hujambo!

Hujambo! Karibu kwa taarifa za moja kwa moja kuhusu yanayojiri nchini Gambia. Rais Yahya Jammeh amepewa makataa ya mwisho kuondoka madarakani.