Got a TV Licence?

You need one to watch live TV on any channel or device, and BBC programmes on iPlayer. It’s the law.

Find out more
I don’t have a TV Licence.

Muhtasari

  1. Tume ya Uchaguzi inaendelea kupokea Fomu 34A za matokeo ya urais kutoka vituoni
  2. Matokeo ya awali yanaonesha Rais Kenyatta anaongoza akiwa na kura 8 milioni. naye Bw Odinga ana kura 6.6 milioni.
  3. IEBC imesema mitambo yake haidukuliwa, kinyume na madai ya muungano wa upinzani Nasa
  4. Jumanne kulitokea vurugu katika baadhi ya maeneo mtaa wa Mathare, Nairobi na baadhi ya maeneo Kisumu. Lakini kwa sasa hali ni tulivu
  5. Waziri wa usalama Fred Matiang'i amewaomba wananchi kuendelea na shughuli za kawaida bila wasiwasi
  6. Katika barabara za Nairobi magari yameanza kuonekana lakini bado hali ya kawaida haijarejea

Habari za moja kwa moja

time_stated_uk

Wanawake washinda nyadhfa za Ugavana Kenya

Aliyekuwa waziri wa ardhi nchini Kenya Charity Ngilu ni miongoni mwa wanawake watatu nchini Kenya wanaotarajiwa kuwa magavana wapya wa kaunti zao.

Ngilu ambaye aliwania wadhfa huo katika kaunti ya Kitui nchini Kenya kupitia chama Nark alimshinda Gavana Julius Malombe kwa wingi wa kura.

Mgombea mwengine mwanamke ambaye ameshinda wadhfa wa Ugavana ni aliyekuwa naibu wa spika bungeni Dkt Joyce Laboso .

Laboso amemshinda gavana Isaac Rutto ambaye hivi majuzi alikuwa miongoni mwa viongozi wakuu wa muungano wa upinzani Nasa.

Mwanamke huyo ambaye alikuwa akigombea wadhfa huo kupitia chama tawala cha Jubilee alikuwa ameshutumiwa na mpinzani wake aliyemtaka kuwania ubunge katika eneo la Nyanza alikoolewa.

Mgombea mwengine ni Anne Waiguru ambaye wakati mmoja alihudumu kama waziri wa maswala ya ugatuzi .

Waiguru ambaye alilazimika kujiuzulu katika wadhfa huo kutokana na madai ya ufisadi yaliomkabili anaendelea kupata ushindi dhidi ya Martha Karua aliyewahi wakati mmoja kugombea urais mbali na kuwa waziri..

Anne Waiguru
BBC
Anne Waiguru

Wafuasi wa upinzani 'washerehekea' Kisumu

Wafuasi wa muungano wa upinzani National Super Alliance katika mtaa wa Kondele, Kisumu wamekusanyika barabarani na kusherehekea tangazo la muungano huo kwamba haukubali matokeo yanayotangazwa na Tume ya Uchaguzi IEBC mtandaoni.

Viongozi wa Nasa wamesema wamedai mgombea wa upinzani Raila Odinga ndiye aliyeshinda uchaguzi huo.

Mwandishi wa BBC Peter Njoroge amepiga picha hizi za wafuasi hao barabarani:

Upinzani
BBC
Upinzani
BBC
Upinzani
BBC
Polisi
BBC
Upinzani
BBC

Wafanyabiashara Kenya wawaomba wananchi kurejea kazini

Muungano wa wafanyibiashara Kenya KEPSA umetoa wito kwa Wakenya kurejea kazini na kuendelea na biashara zao.

Siku tatu baada ya uchaguzi, taharuki imetanda katika baadhi ya maeneo ingawa utulivu umedumu katika taifa hilo. Maelfu ya wakenya waliosafiri kupiga kura nje ya baadhi ya maeneo wamekwama huku wamiliki wa magari wakihofia uharibifu wa magari hayo.

Hata hivyo, wafanyibiashara hao wakiongozwa na mwenyekiti wao, Vimal Shah, wamewataka Wakenya kutotiwa wasiwasi na ujumlishaji wa matokeo unaoendelea na badala yake kuwa na ujasiri wa kuendelea na shughuli zao.

“Turejee katika shughuli za kawaida, tusijifungie majumba,” alisema. Bwana Shah ametoa wito kwa tume ya IEBC kuwasilisha matokeo kuondoa wasiwasi.

“Tunawaomba wahusika waweze kutekeleza majukumu yao bila wasiwasi na kuwa na usawa na haki kwa wote,” aliongeza.

Kwa upande wake, mwenyekiti wa muungano wa wamiliki wa magari ya usafiri, maarufu matatu, Simon Kimutai, amewarai waajiriwa sehemu tofauti kujitokeza wamiliki wa magari kuyaruhusu magari

Aliyekuwa mlinzi wa mbunge sasa ni mbunge

Nimrod Mbithuka Mbai wakati mmoja aliwahi kuwa mlinzi wa wabunge na maafisa wa serikali , lakini baada ya kupata ushindi wa uchaguzi wa Agosti 8 sasa atahudumu kama mbunge kwa kitui mashariki.

Gazeti la Daily Nation nchini Kenya limesema kuwa afisa huyo wa zamani wa polisi alimshinda mbunge aliyepo madarakani na sasa atajiunga na mbunge aliyekuwa akimlinda bungeni baada ya wote wawili kuchaguliwa katika bunge jipya.

Mbithuka aliwahji kuwa mlinzi wa mbunge
Nation
Mbithuka aliwahji kuwa mlinzi wa mbunge

Wafuasi wa upinzani washerehekea Kenya

Wafuasi wa kiongozi wa upinzani nchini Raila Odinga wamejitokea katika barabara nyingi mjini Kisumu na Magharibi mwa Kenya maeneo yanayodaiwa kuwa ngome za upinzani.

Mwandishi wa BBC aliwapiga picha wakisherehekea baada ya kiongozi mmoja wa muungano wa upinzani wa NASA kusema kuwa mgombea wao alikuwa ameshinda uchaguzi wa Jumanne.

Muungano huo unapinga matokeo ya tume ya uchaguzi ya IEBC yanayoonyesha kwamba rais Uhuru Kenyatta anaongoza kwa kura.

Habari za hivi pundeUpinzani wadai Odinga alishinda uchaguzi Kenya

Mudavadi
BBC

Muungano wa upinzani Kenya umeendelea kupinga matokeo ya uchaguzi wa urais yanayotangazwa na tume hiyo kwenye mtandao wake.

Viongozi wa muungano wa National Super Alliance wamesema walikutana na wakuu wa Tume ya Uchaguzi Kenya na kuwasilisha rasmi malalamiko yao kupitia barua.

Ajenti mkuu wa upinzani Musalia Mudavadi, ambaye ni naibu waziri mkuu wa zamani, amesema upinzani umepata maelezo zaidi kwamba matokeo ya uchaguzi yalivurugwa baada ya kudukuliwa kwa mitambo ya IEBC.

Wakuu wa IEBC wamekanusha kwamba mitambo ilidukuliwa. Mwenyekiti Wafula Chebukati amesema kulikuwa na jaribio la kudukua mitambo hiyo, lakini halikufanikiwa.

Bw Mudavadi amedai mgombea wa upinzani Raila Odinga ndiye aliyeshinda uchaguzi huo.

“Twamtaka mwenyekiti wa IEBC atangaze matokeo na kumtangaza Odinga na Kalonzo rais mteule na naibu rais mteule wa Kenya mara moja,” amesema Bw Mudavadi.

Nchini Kenya, ni kinyume cha sheria kwa mtu yeyote kutangaza matokeo au kusambaza matokeo ambayo hayajatoka kwa tume ya taifa ya uchaguzi. Ni tume hiyo ya uchaguzi pekee inayoruhusiwa kutangaza matokeo.

Bw Mudavadi ameendelea kuwaomba Wakenya kuwa watulivu.

Wafuasi wa wagombea wakabiliana Garissa

Sehemu ya soko kuu mjini Garissa, kaskazini mashariki mwa Kenya, imeteketea baada ya mfarakano kati ya wafuasi wa wagombea wawili wa ugavana katika kaunti hiyo.

Fujo zilizuka baada ya matokeo ya uchaguzi huo uliofanyika Jumanne kutangazwa.

Ali Bunow Korane wa chama cha Jubilee chake Rais Kenyatta alitangazwa mshindi.

Taarifa zinasema watu wasioridhishwa na matokeo hayo walichoma moto sehemu za soko hilo.

Hali ya utulivu imerejea lakini wazima moto wameendelea kukabiliana na moto huo.

Korane alipata kura 55 335 (51,48%) naye mpinzani wake wa karibu Nathif Jama Adan wa chama cha Wiper akapata kura 50 471 (46,95%).

Bw Adan ndiye gavana anayeondoka.

Moto Garissa
BBC
Garissa
BBC

Watumishi wa umma watakiwa kurejea kazini

Mkuu wa utumishi wa umma nchini Kenya Joseph Kinyua amewaamuru watumishi wote wa umma kurejea kazini baada ya "kufanyika kwa uchaguzi wa kufana kwa njia ya amani."

Matokeo rasmi ya uchaguzi wa urais bado hayajatangazwa, ingawa tume ya uchaguzi imedokeza kwamba huenda yakatangazwa baada ya saa sita mchana kesho Ijumaa.

Serikali ilikuwa imetangaza Jumanne pekee, siku ya uchaguzi, kuwa siku ya mapumziko.

Hapa chini ni taarifa iliyotumwa na Bw Kinyua:

Taarifa ya Kinyua
BBC

Hali ya utulivu yashuhudiwa Kisumu

Hali ya kawaida ilirejea mjini Kisumu, magharibi mwa Kenya baada ya polisi kukabiliana na vijana waliokuwa wanaandamana na kufunga barabara katika baadhi ya maeneo.

Mwandishi wetu Peter Njoroge, ametutumia picha hizi:

Utulivu Kisumu
BBC
Barabara wazi
BBC

Ekuru Aukot akubali kushindwa Kenya

Mgombea wa pili wa urais nchini Kenya Dkt Ekuru Aukot amekubali kushindwa.

Ndiye wa pili kutangaza kushindwa baada ya Dkt Japheth Kavinga Kaluyu kukubali kushindwa jana.

Dkt Aukot amesema anaamini "Wachache walipata fursa ya kusikika, na wengi walishinda."

"Jiwe la Daudi halikumuweza Goliathi wakati huu, na asiyekubali kushindwa si mshindani," amesema.

Ametoa wito kwa Raila: "Hatungekuwa hapa bila wewe, demokrasia ya Kenya ya sasa haiwezi kuzungumziwa bila wewe kuwepo.

Kenya yataka kusonga mbele, Wakenya wanataka kurejelea shughuli za kawaida.

Kwa kuchunguza Fomu 34A tulizopata, tumegundua kwamba hakuna sababu ya kuamini kuna chochote kitabadili matokeo ya sasa."

Amemtaka Rais Kenyatta, akitangazwa mshindi, aunde serikali yake kwa kujumuisha wote.

Dkt Aukot amedokeza kwamba huenda akawania tena urais mwaka 2022.

Soma zaidi kumhusu Dkt Aukot hapa: Ekuru Aukot: ‘Daktari wa Katiba’ anayetaka kuwa rais Kenya

Nkurunziza akimbia kumpongeza Kenyatta

Hata kabla ya matokeo rasmi ya uchaguzi nchini Kenya ujumbe wa kumpongeza mshindi wa urais umechapishwa katika akaunti ya Twitter ya Rais wa Burundi Pierre Nkurunziza.

Bw Nkurunziza anaonekana kumpongeza Rais Kenyatta.

Lakini labda ni afisa wa mawasiliano wa Nkurunziza ambaye ameandika ujumbe huo.

Kwenye maelezo katika ukurasa huo wa Twitter, ambao una wafuasi 59,000, ujumbe wa moja kwa moja kutoka kwa rais huyo unafaa kuwa na sahihi ya PN.

View more on twitter

Chebukati: Wadukuzi walijaribu lakini wakashindwa

Mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati amethibitisha kwamba kulikuwa na jaribio la kudukua mitambo ya tume hiyo.

Hata hivyo, amesema wadukuzi hawakufanikiwa.

Muungano wa upinzani NASA ulikuwa umedai mitambo ya tume hiyo ilidukuliwa siku ya uchaguzi na matokeo yaliyokuwa yakipeperushwa katika tovuti ya tume hiyo yalikuwa 'yamechakachuliwa'.

Chebukati: Waangalizi wamekubali uchaguzi ulikuwa huru na wa haki

Mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati anahutubia wanahabari ukumbi wa Bomas, Nairobi akiandamana na Afisa Mkuu Mtendaji Ezra Chiloba.

Bw Chebukati amesema matokeo yamekuwa yakiingia kutoka vituoni usiku na asubuhi.

"Tume imejitolea kutekeleza wajibu wake.

Tunakaribisha taarifa za awali za waangalizi wa uchaguzi wa nchini na hata nje ya nchi, ambao wote wanakubali kwamba uchaguzi ulikuwa wa uwazi, huru na wa haki

Tunawahakikishia Wakenya kwamba tutadumisha kiwango hiki cha uwazi.

Kufikia sasa tumepokea Fomu 34A kutoka vituo 29,499 kati ya vituo vyote 40,883.

Kuhusu Fomu 34B, za kujumlisha matokeo maeneo bunge, tumepokea kutoka maeneo 117 kati ya 290.

Fomu 34B ni za kujumlisha matokeo ya Fomu 34A katika eneo bunge, na zitaongoza tangazo la jumla la matokeo ya urais.

“Tumefanya kila tuwezalo kuhakikisha uchaguzi umekuwa huru na wa haki.

“Tunajizatiti kutoa matokeo haraka iwezekanavyo.

“Tunatarajia matokeo yote yafike kituo cha taifa cha kujumlishia matokeo kufikia saa sita mchana kesho.”

Kazi kama kawaida Kericho

Wafanyakazi wa kuchuma majani ya cha eneo la Kericho, kusini mwa Bonde la Ufa nchini Kenya wamerejea kazini katika mashamba ya kampuni ya Unilever. Walikuwa wamepewa rasmi siku moja kupumzika siku ya uchaguzi Jumanne.

Majani chai
BBC
Majani chai
BBC

Mbeki: Jukumu la waangalizi ni kuangalia

Kiongozi wa waandalizi wa uchaguzi wa Umoja wa Afrika (AU) Thabo Mbeki amesema hawawezi kuzungumzia madai ya upinzani kwamba mitambo ya IEBC ilidukuliwa.

Kiongozi huyo mstaafu wa Afrika Kusini amesema jukumu la waangalzii ni kuangalia shughuli ya uchaguzi inavyofanyika.

"Sisi si wachunguzi wa uchaguzi," amesema.

Iwapo tungeona kitu kikifanywa vibaya, kinyume na sheria za Kenya na viwango vya AU, tungeingilia kati.

Katika baadhi ya visa, NASA wamewasilisha malalamiko kwetu kuhusu uchaguzi, mfano kupatikana kwa sajili ya wapiga kura na usalama pia - mfano kusafirishwa kwa maafisa takriban 40 wa polisi kwenda kwingine.

Tuliangazia haya, na baadhi tukawapasha IEBC kuhusu malalamisho ya sajili na kuhusu polisi tukawasiliana na kukutana na waziri wa usalama Dkt Fred Matiang'i.

Mbeki: Shughuli ya upigaji kura iliridhisha

Kiongozi wa waandalizi wa uchaguzi wa Umoja wa Afrika (AU) Thabo Mbeki amesema shughuli ya upigaji kura nchini Kenya ilikuwa ya uwazi na waangalizi hao waliridhishwa na shughuli hiyo.

Hata hivyo amesema kulikuwa na changamoto kadha, mfano ingawa karatasi zilikuwa za rangi tofauti pamoja na masanduku, kulikuwa na rangi mbili ambazo zilikuwa zinakaribiana sana.

Hata hivyo, amesema maafisa wa uchaguzi waliwasaidia wapigaji kura kutofautisha rangi hizo.

Bw Mbeki ameipongeza pia serikali na tume kwa kuhakikisha wafungwa walipiga kura.

"Tunafahamu kwamba IEBC bado inahesabu na kukagua matokeo. Shughuli ya uchaguzi bado inaendelea hivyo bado ni mapema hivyo. Hata hivyo, waangalizi wa AU wanafurahi kwamba uchaguzi ulikuwa wa amani, siku ya uchaguzi watu walifika kwa wingi, na waliruhusiwa kuopiga kura kwa kufuata taratibu za uchaguzi Kenya na zinazokubaliwa na AU," amesema.

Tunaweza kusema kwamba shughuli tulizohesabu, upigaji kura na upeperushaji wa matokeo, vilitimiza viwango vya ubora vya Kenya na AU.

Amesema wamepokea malalamiko kuhusu upeperushaji wa matokeo. Ametoa wito kwa wadau kutumia mifumo wa kisheria iliyopo.

Bw Mbeki amesema maafisa wa Nasa walikutana na waangalizi wa AU na kuwapa ripoti kuhusu madai ya udukuzi wa mitambo ya IEBC.

Amesema waliulizwa walipata vipi nyaraka walizokuwa nazo za madai ya udukuzi. Walisema walikuwa wamepewa 'ufunguo' fulani na IEBC wa kuweza kuingia kwenye sava.

Hata hivyo, tuliwaambia kwamba kwa kufuata fomu 34A itawezekana kwa kila mtu kubaini matokeo halisi.

Upinzani hata hivyo ulitilia shaka uhalisi wa fomu hizo na kusema katika baadhi ya vituo vya kupigia kura hawakuwa na maajenti na katika baadhi, maajenti wao walizuiwa kuingia.

Aidha, upinzani ulisema huenda fomu 34A katika baadhi ya vituo zilifanyiwa mabadiliko.

Mbeki
BBC

Waangalizi wa uchaguzi wa EAC wafurahishwa na upigaji kura

Waangalizi wa uchaguzi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki wamesema walifurahishwa na jinsi uchaguzi ulivyoandaliwa siku ya uchaguzi.

Wamekataa kuzungumzia madai ya upinzani kwamba mitambo ya Tume ya Uchaguzi IEBC ilidukuliwa.

Wamesema hawakuwa "wanaangalia udukuzi".

IEBC: Tunaendelea kupakia fomu za matokeo mtandaoni

Tume ya uchaguzi Kenya imesema inaendelea kupakia Fomu 34A (fomu za kuthibitisha matokeo katika vituo vya kupigia kura) mtandaoni.

Upinzani ulitaka matokeo yanayotolewa katika mtandao wa tume hiyo yawe yanaambatana na fomu hizo.

View more on twitter

Yasemavyo magazeti Kenya leo

Hivi ndivyo magazeti nchini Kenya yalivyoangazia matokeo ya uchaguzi mkuu uliofanyika Jumanne, hatua ya upinzani kupinga matokeo ya awali yanayotangazwa, kutokea kwa maandamano katika baadhi ya maeneo na hali ilivyo kwa jumla nchini humo:

Taifa
BBC
Standard
BBC
Nation
BBC
Star
BBC
People
BBC

Usiku wa shughuli nyingi Bomas matokeo yakikaguliwa

Ulikuwa ni usiku wa shughuli nyingi katika kituo cha taifa cha kujumlishia matokeo Bomas.

Maajenti wa vyama vya siasa walikuwa wakikagua Fomu 34A za matokeo kutoka vituo vya kupigia kura katika sehemu maalum.

Mgombea wa upinzani Raila Odinga alikuwa amelalamika awali kwamba IEBC ilikuwa ikitangaza matokeo bila kutoa fomu hizo.

Tume hiyo baadaye ilitoa fomu hizo. Kufikia sasa ni vituo 1,200 pekee kati ya 40,883 ambavyo havijawasilisha matokeo.

Tume ya uchaguzi imeahidi kutoa maelezo kuhusu matokeo yaliyo kwenye fomu zilizopokelewa Bomas baadaye leo.

Soma zaidi:

Matokeo Bomas
BBC
Ajenti wa Raila
BBC
Maafisa wa IEBC
BBC

Yaliyotokea usiku ukumbi wa kujumlishia matokeo Bomas

Mwandishi wa BBC Abdinoor Aden alikuwa ukumbi wa Bomas usiku ambapo maafisa wakuu wa tume ya uchaguzi wanajumlishia matokeo na kutoa taarifa kuhusiana na uchaguzi.

Mtazame hapa kuhusu yaliyojiri:

View more on facebook

Matokeo ya awali ya hivi punde zaidi uchaguzi wa urais

Matokeo ya awali ya hivi punde zaidi kutoka vituo 39758 kati ya 40883:

  • Uhuru Kenyatta wa chama cha Jubilee anaongoza akiwa na kura 8,030,434 (54.27%).
  • Raila Odinga wa chama cha ODM ana kura 6,635,035 (44.84%)

Kura zilizoharibika zimeendelea kuwa nyingi, kufikia sasa kura zilizoharibika ni 394,969.

Hujambo!

Karibu kwa siku nyingine ya taarifa za moja kwa moja za habari kuhusu uchaguzi mkuu Kenya uliofanyika Jumanne. Matokeo kamili yanaendelea kusubiriwa.