Got a TV Licence?

You need one to watch live TV on any channel or device, and BBC programmes on iPlayer. It’s the law.

Find out more
I don’t have a TV Licence.

Muhtasari

  1. Takriban viongozi wa mataifa 13 kuhudhuria hafla hiyo
  2. Upinzani kuandaa mkutano sambamba jijini Nairobi
  3. Rais Magufuli wa Tanzania miongoni mwa wageni waalikwa
  4. Rais Kenyatta akabiliwa na awamu ngumu wa kuunganisha taifa

Habari za moja kwa moja

time_stated_uk

Kenyatta na Ruto wafunga sherehe kwa maombi

Rais Kenyatta na Naibu Rais William Ruto wamekamilisha sherehe za leo uwanja wa Kasarani kwa maombi, Bw Kenyatta ameongoza kwa Kiingereza na Bw Ruto kwa Kiswahili.

Baadaye, wimbo wa Jumuiya ya EAC umechezwa na kisha wimbo wa taifa la Kenya kuhitimisha sherehe za leo.

Wageni wameanza kuondoka uwanjani, wakianza na viongozi wa nchi.

Kenyatta awahimiza Wakenya kuishi kama majirani

Kwa mara nyingine, Bw Kenyatta amewahimiza Wakenya kuishi kama majirani. Amesema majirani hufaana sana na ndio hutegemewa wakati wa shida.

Ameagiza watahiniwa wote wa darasa la nane waliofanya mtihani wao mwaka huu wawe wamefahamu shule za sekondari watakazojiunga nazo kabla ya Krismasi.

Kenyatta: Mwafrika yeyote atapata viza akifika Kenya

Rais Kenyatta ametangaza kwamba Mwafrika yeyote atapewa viza akifika katika kiingilio chochote mpakani au viwanja vya ndege Kenya.

Amesema hataweka masharti kwamba lazima mataifa mengine yafanye hivyo.

Amechukua hatua sawa na iliyochukuliwa na Rwanda majuzi.

Nchini Rwanda hata hivyo, ni raia wa taifa lolote lile.

Ameahidi pia kufufua moyo wa Jumuiya ya Afrika Mashariki. Amesema wananchi wa nchi wanachama watahesabiwa kama Wakenya. Watahitajika tu kutumia kitambulisho. Wanaweza kuingia au kutoka na kufanya kazi, kumiliki mali au hata kuoana bila kuwekewa masharti.

Amesema hata hivyo kwamba sheria nayo itatumika kwa njia sawa.

Kenyatta: 'Siasa si chakula'

Rais amesema siasa zimetumiwa vibaya Kenya kutatiza ustawi wa taifa "badala ya ilivyo nchi za Asia."

Amesema "hakuna aliyewahi kula siasa".

Kenyatta: Tutazungumza na mahakama kuhusu kesi

Rais Kenyatta amesema atazungumza na Idara ya Mahakama kujadiliana kuhusu kuharakishwa kwa kesi ambazo zimekwama miaka mingi.

Aidha, amesema watazungumzia kesi nyingi ambazo zinatumiwa kukwamisha miradi ya serikali.

Kenyatta: Gharama ya umeme itapunguzwa usiku

Rais Kenyatta amesema kuanzia Desemba mwaka huu, gharama ya umeme itapunguzwa usiku, kwa asilimia 50, kati ya saa nne usiku na saa thenashara alfajiri.

Amesema hii ni kusaidia ukuaji wa uchumi wa saa 24.

Kenyatta: Nitaangazia umoja wa taifa na huduma ya afya

Kenyatta amesema ana malengo mawili muhula wake wa mwisho. Kwanza kuimarisha uwiano na umoja miongoni mwa Wakenya.

Amesema ameanza kuwasiliana na viongozi wote na kueleza nia yake ya kuendeleza umoja.

Amesema lengo la pili ni kuhakikisha huduma ya afya inawafikia Wakenya 100%.

Katika miaka mitano ijayo, nitahakikisha Wakenya 13 milioni wanafaidi kupitia huduma ya NHIF. NHIF itafanyiwa mageuzi pamoja na sheria za kusimamia kampuni za bima za kibinafsi.

Amesema atafanikisha mpango wa kumiliki nyumba na makazi.

"Kwa miaka mitano ijayo serikali yangu itaangazia kuhakikisha watu wengine 500,000 wanajipatia nyumba," amesema.

Uwanja wa Jacaranda ni kama mahame

Uwanja wa Jacaranda, Embakasi jijini Nairobi ambapo muungano wa upinzani Kenya Nasa ulipanga kufanya mkutano umebaki kama mahame.

Polisi wamezingira milango yote ya kuingia uwanja huo.

Mwandishi wetu Roderick MacLeod ametutumia picha hii ya hali ilivyo ndani ya uwanja:

Jacaranda
BBC

Kenyatta: Najivunia ugatuzi na miundo mbinu

Rais amesema anajivunia mambo manne ambayo serikali yake ilitimiza miaka minne iliyopita. Mwanzo ugatuzi wa mamlaka na rasilimali, pili ni msingi wa ukuaji wa kiuchumi na kibiashara. Pia ujenzi wa reli ya kisasa na kusambazwa kwa umeme mashinani.

"Tatu tumewekeza katika mageuzi yanayoboresha utoaji wa huduma ya afya. Aidha, upanuzi wa miundo mbinu ya hospitali na Bima ya Afya ya Taifa (NHIF).

"Nne, tumefanyia mageuzi mfumo wetu wa elimu. Kurejesha imani katika mfumo wa mitihani na kuimarisha tena taasisi za elimu."

Kenyatta: Tunaweza kujenga Kenya tunayojivunia

Rais amesema kwa pamoja, bila kujali tofauti za kidini na za kijamii, Wakenya wanaweza kujenga Kenya imara na inayostawi kwa pamoja.

Lakini amesema lazima waacha kuangazia makovu ya kale, na pia kwa kufuata sheria.

"Sheria lazima itawale. Inafaa kuwa kimbilio kwa kila Mkenya na hakuna yeyote anafaa kuvunja sheria au kwenda nje ya mfumo wa sheria bila kujali ukubwa wa malalamiko yako.

"Niwakumbushe, Mahakama ya Nje ilipotutaka tujitee, tulitii. Mahakama ya Juu ya Kenya ilipofuta uchaguzi wetu, hata baada ya kushindwa, baada ya kuambiwa utaratibu ulikuwa muhimu kuliko kula, tuliheshimu uamuzi huo.

"Serikali yangu imedhihirisha kujitolea kuheshimu sheria. Tunatarajia raia wote wengine wafanye hivyo."

"Katiba yetu imeunda mihimili mitatu huru ya serikali...lazima kila mtu afanye kazi yake."

"Matamanio ya binadamu wakati mwingine huzidi kipimo, na yasipodhibitiwa, yanaweza kulibomoa taifa. Ili kuishi pamoja, lazima watu wakubaliane kufuata sheria fulani. Kenya ni nchi ya watu zaidi ya 40 milioni. Tumeishi pamoja ishara kwamba hata tukitofautiana huwa twajua jinsi ya kuungana tena.

"Matatizo mengi hutokea tunapokosa kufuata sheria hizi. Miezi minne iliyopita, tumefanyia majaribio sheria hizi. IEBC, Mahakama, Idara za Usalama. Hizi zote zimefanyiwa majaribio na siasa, na zimesalia imara.

"Uamuzi usipoenda unavyotaka, unaheshimu, hiyo ni demokrasia.

"Tumejifunza kwamba taasisi zetu ni kakamavu kuliko tulivyodhani awali."

"Hatufai kubomoa taasisi zetu kila wakati zikikosa kutoa matokeo tunayotaka."

Kenyatta: Leo ni mwisho wa shughuli yetu ya uchaguzi

Kenyatta amesema leo ni siku ya 123 tangu kufanyika kwa uchaguzi Agosti 8 na kusema shughuli ya uchaguzi sasa imefikia kikomo, na akasisitiza tena.

Anaonekana kupuuzilia mbali upinzani ambao umekuwa ukisisitiza kwamba uchaguzi wa 26 Oktoba haukuwa huru na wa haki na kwamba uchaguzi mpya unafaa kuandaliwa.

Kenyatta: Nitakuwa rais wa Wakenya wote

Bw Kenyatta amesema aliwasikiliza kwa makini wapinzani wake uchaguzini na kwamba atatekeleza baadhi ya mawazo na mapendekezo yao.

"Naahidi kulinda ndoto za wote na maono ya wote, walionipigia kura na waliokosa kunipigia kura. Nitakuwa rais wa wote. Na nitajitolea muda wangu na nguvu kujenga madaraja, kuunganisha Wakenya na kuleta ustawi."

Kenyatta aishukuru mahakama kwa maamuzi huru

Bw Kenyatta amesema Mungu aliyajibu maombi na kwamba atawafikisha Wakenya mbali.

Ameishukuru tume ya uchaguzi kwa kuendesha uchaguzi, chini ya shinikizo nyingi.

Ameisifu Mahakama na kusema ilifanya maamuzi yake kwa uhuru.

Kenyatta: Asanteni sana Wakenya

Rais Kenyatta sasa anahutubu na ameanza kwa kuwashukuru waliohudhuria.

Ameomba kuhutubia kwa Kiingereza kwa sababu ya wageni.

Museveni awahimiza Wakenya wazingatie amani

"Hamjambo Wakenya?" ameanza, na kusema amefika kutuma hongera, na kuwapongeza Wakenya kwa kudumisha amani.

"Nawaomba Wakenya wote wakumbuke mambo matatu manne muhimu. Jambo la kwanza ni amani. Jambo la pili ni ustawi wa jamii. Jambo la tatu maendeleo. Na jambo la nne siasa."

"Msifikirie siasa peke yake mkasahau yale mengine matatu."

Lungu: Kama marafiki tulikuwa na wasiwasi

Rais wa Zambia Edgar Lungu amealikwa kuhutubu kwa niaba ya viongozi wengine wa mataifa.

"Wakenya Mpo? Asante sana," ndivyo alivyoanza.

Amewapongeza Wakenya.

"Tuna furaha sana kwamba shughuli hii imekamilika, tunawahimiza tu mrejee kazini. Kama marafiki, tulikuwa na wasiwasi kwamba shughuli hii ilichukua muda mrefu. Tunatumai mtalifikiria hilo siku za usoni.

Ali Bongo Ondimba wa Gabon pia amealikwa kuhutubu na kusema anajivunia sana leo kuwa Mwafrika.

"Nyinyi watu wa Kenya mmetufanya kujionea fahari sana," amesema.

"Wananchi wa Kenya hamjambo? Tumekuja hapa kusema hongera, hongera sana," huyo naye ni Paul Kagame wa Rwanda.

Kumalizia ni mwenyekiti wa sasa wa Jumuiya ya Afrika Mashariki Yoweri Museveni.

Ruto: Tumekusanyika pia kusherehekea demokrasia

Bw Ruto amesema leo pia Wakenya wamekusanyika kusherehekea demokrasia ya Kenya, baada ya uchaguzi.

"Kwamba tuna uwezo wa kuamua mustakabali wetu, kuwachagua viongozi wetu na mwelekeo wa taifa letu la Kenya."

Amesema uchaguzi wa wakati huu ulikuwa na mambo mawili wakuu, tofauti na ule wa 2013.

Kwamba serikali iliungana chini ya chama cha Jubilee na upinzani uliungana chini ya Nasa.

View more on twitter

Amesema pia badala ya ukabila, kampeni ziliangazia zaidi masuala ya umuhimu kwa wananchi.

"Hizi ni ishara za hatua tulizopiga kama taifa kuelekea kwenye siasa zilizokomaa," amesema.

Ameahidi kumuunga mkono Rais Kenyatta kuunganisha jamii mbalimbali za Kenya.

"Sote (kama Wakenya) lazima tuungane pamoja na kukataa chuki, ukabila, migawanyiko na kukataa ghasia," amesema, na kuongeza kuwa muhimu zaidi ni ustawi na maendeleo ya nchi, mambo ambayo ameeleza kuwa hayawezi kupatikana bila amani.

"Na amani haiwezi kupatikana bila haki, na haki haiwezi kupatikana bila kuheshimu sheria," amesema.

William Ruto ahutubu Kasarani, aongoza wimbo

Baada ya kipindi cha burudani, Naibu Rais Ruto ameanza kuhutubu. Amesema wamefika walipo sio kwa nguvu zao bali mapengi ya Mungu.

"Ndio nimesikia mkiimba asubuhi, kwa si uchawi ni maombi."

Anaongoza wimbo: Hakuna Mungu kama Wewe.

Sherehe rasmi ya kumuapisha rais yakamilika

Msajili wa mahakama Anne Amadi ametangaza kwamba sasa sherehe rasmi ya kumuapisha Rais na Naibu wake imekamilika. Maafisa wakuu wa mahakama na Rais na Naibu wake wamepigwa picha kadha.

Sehemu inayofuata ya sherehe, ambayo ni burudani na hotuba sasa inaanza.

Mizinga 21 itafyatuliwa pia kwa heshima ya Rais.

Maraga amtambulisha Naibu Rais Ruto

Baada ya Bw Ruto kula kiapo na kutia saini hati za kiapo, Jaji Mkuu amemtambulisha kama Naibu Rais kwa wananchi Kasarani.

Maraga amtambulisha Naibu Rais Mteule

Jaji Mkuu David Maraga sasa anamtambulisha Rais Mteule William Ruto ambaye pia atalishwa kiapo cha utiifu na kiapo cha kuhudumu kama Naibu Rais wa Kenya.

Maraga: Namtambulisha sasa Rais Wakenya

Jaji Mkuu Maraga: "Wananchi, sasa ni furaha yangu kuu kumtambulisha kwenu Rais wa Jamhuri ya Kenya."

Biblia ya uhuru yatumiwa kumwapisha Uhuru Kenyatta

Mfawidhi wa sherehe amefafanua kwamba nakala ya Biblia iliyotumiwa kumwapisha Rais ni ile iliyotumiwa kumwapisha rais wa kwanza wa Kenya Jomo Kenyatta ambaye ni babake rais wa sasa.

Nakala ya Katiba ni iliyotiwa saini wakati wa kurasmishwa kwa Katiba ya sasa mwaka 2010 uwanjani Uhuru Park.

Usalama umeimarishwa uwanjani Uhuru Park.

Gari la Uhuru
BBC

Habari za hivi pundeKenyatta aapishwa kutekeleza majukumu ya urais

Msajili wa Mahakama Anne Amadi, anamlisha sasa kiapo cha kutekeleza majukumu ya afisi ya rais.

Rais Kenyatta: "Nitatekeleza majukumu yangu, na wajibu wangu katika afisi ya rais wa Kenya, na kwamba nitatenda haki kwa wote kwa mujibu wa katiba hii kama ilivyo kwenye sheria, na sheria za Kenya bila woga, mapendeleo au ubaguzi au nia mbaya. Ewe mwenyezi Mungu nisaidie."

Baadaye, ametia saini viapo vyote viwili, kisha cheti cha kuapishwa, kuthibitisha kwamba sherehe ya leo imefanyika.

Jaji Mkuu David Maraga pia ataweka saini yake kwenye stakabadhi zote tatu (vipao viwili) na cheti cha kuapishwa kwa Rais.

Habari za hivi pundeRais Kenyatta ala kiapo cha utiifu

Rais Kenyatta: "Naapa kwamba nitakuwa mwaminifu, kikamilifu, kwa Jamhuri ya Kenya, kwamba nitatii, nitahifadhi, kulinda na kutetea Katiba ya Kenya kama ilivyo kwenye sheria, na sheria nyingine zote za Jamhuri. Na kwamba nitalinda mipaka na heshima ya watu wa Kenya. Ewe Mwenyezi Mungu nisaidie."

Maraga amtambulisha Rais Mteule Uhuru Kenyatta

Jaji Mkuu David Maraga amesema kwa mujibu wa Katiba na Sheria: "Mimi David Kenani Maraga, Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Kenya, hapa, namtambulisha kwa watu wa Kenya Rais Mteule Mheshimiwa Uhuru Kenyatta." Hadhira inashangilia.

Maraga aalikwa jukwaa la kumwapisha Rais

Bi Amadi amekaribishwa jukwaa la kumwapishia rais. Amemtambua Rais mteule Uhuru Kenyatta, huku hadhira ikishangilia. Amemtambulisha mkewe rais, Margaret, Naibu Rais mteule na mke wake William Ruto na Rachel.

Amewatambua pia wageni wengine waheshimiwa.

Msajili wa mahakama ajiandaa kumlisha kiapo rais

Msajili wa Mahakama Anne Amadi amechukua usukani, ambapo anatarajiwa kumlisha kiapo rais mbele ya Jaji Mkuu David Maraga.

Anafafanua kuhusu utaratibu wa kulishwa kiapo ulivyo kwenye katiba na sheria.

Polisi wakabiliana na wafuasi wa upinzani Jacaranda

Mwandishi wetu David Wafula ambaye anafuatilia mkutano wa upinzani, ameshuhudia makabiliano kati ya polisi na wafuasi wa upinzani.

Anasimulia:

View more on facebook

Matairi yachomwa barabara inayoelekea Jacaranda

Mwandishi wetu David Wafula ametutumia picha hizi za matairi yakiwa yanachomwa barabarani kwenye barabara inayoelekea uwanja wa Jacaranda, eneo la Embakasi jijini Nairobi.

Upinzani ulikuwa umepanga mkutano sambamba wa kuombolewa wafuasi wa upinzani waliouawa wakati wa makabiliano na polisi.

Jacaranda
BBC
Jacaranda 2
BBC
Jacaranda
BBC

Kenyatta hatimaye awasili Kasarani

Rais mteule Uhuru Kenyatta ameingia uwanjani Kasarani. Anauzunguka uwanja akiwa kwenye gari rasmi akiwasalimia na kupokea salamu kutoka kwa wananchi waliohudhuria.

Museveni aingia uwanjani Kasarani

Rais wa nchi jirani ya Uganda Yoweri Museveni amewasili uwanjani Kasarani huku msafara wa magari ya Rais Kenyatta ukielekea uwanjani humo.

Bw Museveni aliwasili Kenya jana jioni na kulakiwa na waziri wa mambo ya nje wa Kenya Bi Amina Mohamed na mwana wa Rais mstaafu Daniel Moi, Gideon Moi.

Museveni baada ya kutua uwanja wa ndege wa Jomo Kenyatta jana
Amina Mohamed /Twitter
Museveni baada ya kutua uwanja wa ndege wa Jomo Kenyatta jana

Kagame pia awasili Kasarani

Rais wa Rwanda Paul Kagame pia amefika Kasarani. Wengine waliofika ni marais wa Djibouti, Gabon na Namibia.

Naibu wa Rais Ruto awasili

Naibu wa Rais wa Kenya William Ruto amewasili Kasarani akiandamana na mkewe Rachel. Wamekaribishwa kwa shangwe na vifijo.

Bw Ruto anatarajiwa pia kulishwa kiapo leo kuhudumu kama naibu rais kwa muhula mwingine.

Rais wa Botswana an Khama naye pia amewasili Kasarani. Rais wa Sudan Kusini Salva Kiir pia amewasili.

Lucy na Seretse Khama: Hadithi ya mapenzi iliyoshangaza dunia

Samia Suluhu awasili Kasarani

Makamu wa Rais wa Tanzania Bi Samia Suluhu Hassan, ambaye anamwakilisha Rais Dkt John Magufuli amefika uwanjani Kasarani na kukaribishwa rasmi.

Viongozi waanza kuwasili Kasarani

Viongozi wa nchi mbalimbali wameanza kuwasili Kasarani, dalili kwamba sherehe rasmi inakaribia kuanza.

Wa kwanza kuwasili alikuwa Rais wa Zambia Edgar Lungu.

Msafara wa magari ya Naibu Rais William Ruto pia umeondoka ikulu Nairobi.

Polisi watumia mabomu ya machozi kuzuia mkutano wa upinzani

Muungano wa upinzani National Super Alliance ambao umesema hautambui ushindi wa Bw Kenyatta uchaguzi wa marudio wa 26 Oktoba ulikuwa umepanga kufanya mkutano sambamba uwanja wa Jacaranda, Nairobi.

Muungano huo unaoongozwa na waziri mkuu wa zamani Raila Odinga ulisusia uchaguzi huo wa marudio ukisema haungekuwa huru na wa haki.

Polisi, ambao walikuwa wametangaza hakutakuwa na mkutano mwingine Nairobi kando na sherehe ya kuapishwa kwa Kenyatta, wametumia mabomu ya machozi kuwatawanya wafuasi wa upinzani waliokuwa wanakusanyika nje ya uwanja huo.

View more on twitter

Magufuli kuwakilishwa na makamu wake Samia Suluhu

Samia Suluhu
@TZ_MsemajiMkuu / Twitter

Rais wa Tanzania John Magufuli, ambaye awali afisi yake ilikuwa imetangaza angehudhuria sherehe za kuapishwa kwa Rais Kenyatta, hatahudhuria sherehe za leo.

Taarifa kutoka ikulu Dar es Salaam inasema badala yake atawakilishwa na makamu wake Samia Suluhu Hassan.

Uhusiano kati ya Kenya na Tanzania umeonekana kudorora siku za karibuni hasa kufuatia kupigwa mnada kwa ng'ombe zaidi ya elfu moja kutoka Kenya waliokuwa wameingizwa Tanzania. Tanzania kadhalika ilichoma moto vifaranga waliodaiwa kutoka Kenya.

Soma zaidi: Kwa nini Tanzania ikawapiga mnada ng’ombe na kuteketeza vifaranga kutoka Kenya

Hii ndiyo taarifa iliyotolewa na ikulu
BBC
Hii ndiyo taarifa iliyotolewa na ikulu

Mkanyagano ulivyokuwa

Maafisa wa polisi walilazimika kutumia vitoa machozi ili kuwazuia maelfu ya watu waliojaribu kutumia nguvu kuingia katika uwanja wa Kasarani uliodaiwa kujaa .Katika kisa hicho watu kadhaa walipata majeraha baada ya kutokea kwa mkanyagano

Mkanyagano Kasarani
BBC
Mkanyagano Kasarani

Lowassa afika sherehe ya kuapishwa kwa Kenyatta

Kiongozi wa upinzani nchini Tanzania Edward Lowassa ni miongoni mwa wageni waliofika Kasarani sherehe ya kuapishwa kwa Bw Kenyatta.

Rais wa Tanzania John Magufuli anatarajiwa kuhudhuria sherehe hizo.

View more on twitter