Huwezi kusikiliza tena

Kisa na Mkasa Wiki Hii

Sheria msumeno

Waswahili wanasema sheria ni msumeno. Unakata mbele.. Na nyuma.

Waziri wa sheria wa Swaziland, huenda akakabiliwa na adhabu wa kifo, baada ya kukutwa akifanya mapenzi na mke wa kumi na mbili wa mfalme Mswati wa tatu wa Swaziland.

Mke huyo, Nonthando Dube, alifumaniwa -- Jahra Bin Su--- yaani red handed-- akiwa na waziri wa sheria, Ndumiso Mamba, ambaye ni rafiki wa karibu wa Mfalme Mswati.

Mke huyo wa kumi na mbili, ambaye umri wake ni miaka ishirini na mbili hivi sasa yuko katika kifungo cha nyumbani.

Waziri Ndumiso Mamba anatuhumiwa kwa kosa la kuingilia nyumba ya mwanaume mwingine, na hukumu yake ni kifo. Bi Dube, ambaye ana watoto wawili na mfalme Mswati, alichumbiwa wakati akiwa na umri wa miaka kumi na sita, baada ya mfalme kumuona wakati akishiriki katika michuano ya kusaka mlimbwende.

Huenda bibie huyo akakabiliwa na adhabu ya kufukuzwa na kuishi nje ya himaya hiyo ya kifalme ya Swazi.

Mke huyo wa mfalme na waziri, walifumaniwa katika hoteli ya kifalme, iitwayo Royal Villas, iliyopo kwenye mji mmoja karibu na mji mkuu, Mbabane.

Kwa mujibu wa gazeti la Daily Mail, wachambuzi wa kisiasa waliliambia gazeti la Daily Telegraph kuwa uhusiano kati ya wawili hao, ni jambo lililokuwa likijulikana na kila mtu nchini Swaziland.

Bi Dube aliolewa na mfalme Mswati, miaka sita iliyopita, na alijifungua mtoto wa kwanza mwaka mmoja baada ya ndoa, na mtoto mwingine wa kiume akafuatia.

Ziara za mwana mfalme

Mwana mfalme William wa hapa Uingereza amesema anapenda sana ziara za nchi za Afrika kwa sababu watu wa huko hawafahamu yeye ni nani.

Prince William, mwenye umri wa miaka ishirini na nane aliyasema hayo wakati akiwa kwenye ziara yake nchini Botswana mapema mwaka huu.

Mwana mfalme William ni mtoto wa kwanza wa mwana mfalme Charles na marehemu Princess Diana.

William ni mjukuu wa Malkia Elizabeth wa pili mtawala wa sasa wa Uingereza.

Prince William amesema akiwa Uingereza au nchi za Ulaya, hufuatwa fuatwa sana na waandishi wa habari na wapiga picha na hata watu wa kawaida.

"Afrika ni mahala pazuri kabisa" amesema mwana mfalme William " Yaani kokote niendapo wengi hawajui mimi ni nani, napenda sana hali hiyo" ameongeza Prince William.

Vita vya mbu

Mwanamama mmoja nchini Taiwan, anayeongoza vita dhidi ya mbu nchini humo, amekamata mbu millioni nne katika kipindi cha mwezi mmoja.

Mbu husumbua sana wananchi wa Taiwan.

Watengenezaji wa mitego maalum ya kukamata mbu waitwao Imbictus International waliandaa shindano, ili kupata mtu atakayekamata mbu wengi.

Mwanamama Huang Yu-yen kutoka mji wa kusini wa Yunlin ameweza kuwashinda washindani wenzake sabini na wawili.

Mbu hao milioni nne walikuwa na uzito wa kilo moja na nusu, uzito ambao ni mara dufu ya mtu aliyeshika nafasi ya pili.

Gazeti la Metro la hapa London limesema mshindi huyo amekabidhiwa donge nono la dola elfu tatu. Imbictus, inayotengeneza mitego ya kukamata mbu, imewasilisha maombi maalum kwa idara ya kumbukumbu za Guiness, kutaka Bi Huang atambulike kama muuaji hodari wa mbu duniani.

Mbu wamekuwa kero kubwa nchini Taiwan, hasa kwa usambazaji wa malaria - hadi ilipofika mwaka 1965 wakati malaria ilipotokomezwa rasmi kisiwani humo.

Hata hivyo kwa sasa mbu hao wamekuwa wakisambaza homa ya dengue.

Jambazi juha

Jambazi moja lenye silaha lililofanya wizi katika mgahawa fulani nchini Marekani, lilipata ghadhabu baada ya kukuta fedha kidogo mno katika hoteli hiyo.

Jambazi huyo alikasirishwa kiasi cha kupiga simu mara mbili katika mgahawa huo kulalamika kuwa, kwa nini walikuwa na fedha kidogo.

Mitandao mbalimbali ya habari imesema jambazo huyo alifanya wizi wake katika mgahawa wa Wendys, uliopo Atlanta, Georgia, Jumamosi iliyopita.

Jambazi huyo aliibuka katika mgahawa huo, usiku, na kumshikia bunduki muuzaji na kudai fedha zote za mauzo, na kisha kukimbia bila ya kuhesabu kiasi cha fedha alichoiba.

Baadaye baada ya kutazama fedha alizokwiba, na kugundua kuwa sio nyingi sana, alisikitishwa mno.

Mwizi huyo aliamua kupiga simu katika mgahawa huo na kulalamika kuwa hakupata fedha za kutosha. "siku nyingine nikija nikute zaidi ya dola mia tano" jambazi huyo amesema alipopiga simu mara ya kwanza.

Ili kusisitiza azma yake alirejea tena kupiga simu na kulalamika na kuwasilisha madai ya kukuta fedha nyingi siku nyingine atakapokwenda kuiba.

Polisi bado wanamtafuta jambazi huyo.

Hoteli ya paka

Hoteli ya kifahari imefunguliwa hapa Uingereza... Maalum kwa ajili ya paka.

Longcroft Cat Hotel inatoa huduma za kifahari kuanzia mandhari hadi chakula maalum kwa ajili ya paka.

Wanaomiliki paka wanapata fursa ya kuwachagulia paka wao, vyumba sita vyenye mvuto mbalimbali. Hoteli hiyo ina vyumba vyenye joto maalum kwa ajili ya wageni wake, ambao ni paka, huku kukiwa na vitanda laini vya kipaka na maeneo maalum ya kufanyia mazoezi na sehemu ya kuchezea.

Wageni hao pia wanapatiwa menu ya kukata na shoka, ambapo vyakula vinavyopikwa hapo ni pamoja na samaki aina ya salmon na tomato tuna surprise pamoja na maini ya kuku yenye hadhi ya nyota tano, yaani 5 star.

Na katika kuwapunguzia mawazo na kuwapa utulivu paka, muziki nyororo unasikika kwa mbali, huku ukuta wa hoteli hiyo ukiwa umepambwa na picha za kuvutia za ndege.

Bei ya vyumba vikubwa ni pauni kumi na tano kwa siku, sawa na takriban dola thelathini, huku vyumba vikubwa zaidi ni pauni kumi na tisa, karibu dola arobaini. Aidha kuna gharama za ziada, kama vile kuchana manyoya ya paka-- yaani kama kuchana nywele kwa binaadam-- kutinda nyusi na hata kuchonga kucha.

Huduma nyingine kwa gharama ya pauni tano kwa wiki, ni kutumiwa barua pepe tatu kwa wiki ukielezwa jinsi paka wako anavyofaidi, na hata picha zake utatumiwa.

Hayo ndiyo mambo ya fedha....

Na kwa taarifa yako.. Mbu huvutiwa na rangi ya bluu, mara mbili zaidi kuliko rangi nyingine.

Hongera Kenya kwa kupiga kura salama salimini... Mmedhihirisha ule usemi usemao, si lazima.

Tukutane wiki ijayo... Panapo majaaliwa...

Habari zimekusanywa kutoka vyanzo mbalimbali mtandaoni.