Huwezi kusikiliza tena

Kisa na Mkasa na Salim Kikeke

Mamba mtabiri

Image caption Pweza Paul

Baada ya mtabiri Paulo ambaye ni pweza, sasa ameibuka mamba aitwaye Harry, ambaye ametabiri ushindi kwa Julia Gillard kuwa waziri mkuu wa Australia, kwenye uchaguzi wa vuta nikuvute nchini humo unaofanyika Jumamosi.

Mamba huyo wa maji baridi alinyakua nyama ya kuku iliyoninginizwa ikiwa na picha ya Bi Gillard na kuiacha nyama nyingine ya kuku yenye picha ya mgombea wa chama cha upinzani Tony Abbott. "yaani hata bila kufikiri aliinua kichwa chake na kunyakua nyama iliyokuwa na picha ya Gillard".

Amesema Nigel Palmer, mwangalizi wa mamba huyo kwenye hifadhi ya wanyama ya Darwin. "Tunadhani sasa amemchagua mgombea huyo", mwangalizi huyo ameliambia shirika la habari la AFP.

Image caption Mamba Harry

Bi Gillard hana budi ya kutokuwa na wasiwasi sana na utabiri huu, kwani mamba huyo pia alibashiri kuwa Uhispania itashinda kombe la Dunia, katika mchezo wa fainali dhidi ya Uholanzi mwezi uliopita.

Kwa kuwa Pweza paulo alishastaafu.. Changamoto kwenu wanasiasa.. Kumsaka mamba Harry.. Huenda usihitaji hata kufanya kampeni...

Vuvuzela ndani ya kamusi

Baada ya kuvurumishwa vilivyo katika kombe la dunia mwaka huu Afrika Kusini, neno Vuvuzela limeingia katika kamusi ya Kiingereza ya Oxford.

Image caption Shabiki wa England akipuliza Vuvuzela

Vuvuzela ni moja kati ya maneno yapatayo elfu mbili mapya yaliyoingizwa katika toleo la tatu la kamusi hiyo lililochapishwa juzi alhamisi. Kwa mujibu wa BBC, maneno mapya yaliyotia fora ni yale yanayohusiana na mtikisiko wa kiuchumi na yanayohusu mtandao wa internet. Baadhi ya maneno mapya ni pamoja na Bromance -- yaani uhusiano wa karibu, usio wa kimapenzi kati ya wanaume wawili -- kule kwetu ungeweza kusema Beshte-- au mshkaji --. Jingine ni Chillax -- yaani kutulia tuli... Ama kuchill. Na jingine kati ya mengi ni neno jipya la mtandao, yaani internet-- sasa pia inajulikana kama interweb.

Mwizi kibonge

Mwizi mmoja nchini Uingereza alibaki akininginia kwa saa kadhaa katika dirisha la nyumba nyumba moja, baada ya kunasa wakati akijaribu kupenya kupitia kadirisha kadoogo huku .

Mwivi huyo alikwama kwa kuwa sehemu ya makalio yake ni kubwa kulio dirisha alilokuwa akijaribu kupenya katika nyumba moja Mashariki mwa jiji hili la London. Gazeti la Metro la hapa London limesema mwizi huyo alibaki akininginia, miguu nje mwili ndani kwa muda wa saa takriban sita.

Image caption Mwizi kibonge

Polisi waliitwa baada ya mwenye nyumba kumkuta bwana huyo kiwiliwili nusu kikiwa ndani ya nyumba yake. Hatimaye mwizi huyo aliokolewa na kikosi cha askari wa zima moto, ambao walilazimika kungoa dirisha.

Msemaji wa polisi kikosi cha Scotland Yard amesema mtu huyo mwenye umri wa miaka thelathini na sita amekamatwa kwa tuhuma za kutaka kufanya wizi na uchunguzi unaendelea.

Mwizi zuzu

Mwizi mmoja wa benki nchini Ujerumani, aliwakebehi polisi kwa kushindwa kumkamata kwa kuwaandikia barua pepe yenye kuwakejeli.

Mamlaka katika jiji la Wuerzburg imesema siku ya Jumatano wiki hii mwizi huyo alituma barua pepe kadhaa kwa polisi na magazeti ya mjini humo akiwakebehi polisi kwa kushindwa kumkamata.

Image caption Polisi wa Ujerumani

Shirika la habari la Reuters limesema katika barua pepe hizo, mwizi huyo alikosoa taarifa za kipolisi zilizotolewa kufuatia wizi katika benki ya mji wa Roettingen wiki moja iliyopita. " Polisi wanasema nilitumia gari, mimi sikutumia gari, nilitoka na kutembea tu baada ya kuiba" Mwizi huyo alijitapa kwenye barua pepe yake. Taarifa ya polisi ilitaja kuwa alitoroka kwa kutumia gari. Hata hivyo, kebehi zake zilikita kisiki baada ya polisi kuweza kufuatilia compyuta ambayo barua pepe hiyo iliandikwa, na kuweza kumkamata mwizi huyo mwenye umri wa miaka kumi na tisa. "Mchezo wake wa paka na panya uligonga mwamba" amesema msemaji wa polisi wa jijini Wuerzburg. "Hakuamini kabisa tulipomkamata" ameongeza msemaji huyo.

Mke n'gombe

Kijana mmoja nchini Indonesia alipewa amri na wazee wa kijiji kufunga ndoa na ngombe baada ya kijana huyo kukutwa kasimama nyuma ya ngombe akiwa hajavaa nguo zozote.

Kijana huyo Ngurah Alit alidai kuwa ngombe huyo ni msichana mrembo aliyejigeuza kimiujiza, na alikuwa akimhadaa kwa kumpa sifa kemkem za kumvutia.

Image caption Jamaa alikutwa nyuma ya n'gombe

Taarifa zinasema wazee katika kijiji hicho walimuamuru kijana huyo kufunga pingu za maisha na ngombe huyo, ili kuepusha mapepo mabaya kukumba kijiji hicho cha Yeh Embang, kilichopo katika pwani ya kisiwa cha Bali. Hata hivyo katika sherehe ya harusi bwana harusi huyo alizimia, wakati ngombe huyo akizamishwa ndani ya maji, katika kufuata mila za huko. Mara moja kijana huyo alibakia kuwa mjane, kwani ngombe huyo alikufa kutokana na kuzamishwa. Kwa mujibu wa mila za huko, si kwamba angefungishwa ndoa halisi, bali ni utaratibu wa kumuondosha mnyama huyo, ili kukisafisha kijiji kutokana na mapepo mabaya. Kijana Alit sio wa kwanza kufungishwa ndoa, na wala si wa mwisho, kwani zimekwishawahi kufungwa ndoa kati ya wakazi wa huko, na nyoka, mbuzi, na hata mbwa.

N'gombe azaa nguruwe

Mkulima mmoja nchini Zimbabwe amesema ngombe wake amezaa nguruwe.

Mkulima huyo Tinos Mberi alishitushwa kuona ngombe wake akizaa kiumbe tofauti kabisa na ngombe. "Mwili wote na ukubwa ni kama wa nguruwe" mkulima huyo ameviambia vyombo vya habari. "Pua na mdomo wake ni kama nguruwe kabisa, tofauti ni kuwa hakuwa na manyoya" ameongeza mkulima huyo aliyeshangazwa.

Image caption Kiti moto

Bwana Mberi amesema ngombe wake alikwisha wahi kuzaa ndama wenye afya kabisa katika siku za awali, na kusema kuna mkono wa mtu. Amesema jambo hilo limetokea kwa sababu za kichawi. "Nadhani hii ni kazi ya wachawi" amesema, na kuongeza "Wanataka kunitisha ili niwaachie ardhi yangu nikimbie". Hata hivyo mtaalam wa mifugo wa eneo hilo amesema hakuna uchawi wala nini. Kwa mujibu wa mtandao wa all voices.com, mtaalam huyo amesema ndama huyo aliyefanana na nguruwe, ni ndama halisi ila ana dosari tu ya kimaumbile.

Na kwa taarifa yako...mwezi Agosti unatajwa kuwa na asilimia kubwa ya watoto kuzaliwa.

Tukutane wiki ijayo... Panapo majaaliwa...