Huwezi kusikiliza tena

Kisa na Mkasa na Salim Kikeke

Foleni kiboko

Ndugu zangu wa Nairobi, Dar es salaam na kampala, mnaolalamika foleni ya magari barabarani, sikiliza hii.

Image caption Foleni kiboko ya magari uchina

Foleni ya magari barabarani yenye urefu wa maili sitini nchini Uchina, imefika siku yake ya kumi na moja, na mamlaka za huko zinasema huenda ikaendelea kwa hata wiki tatu.

Foleni hiyo ya magari barabarani imesababishwa na shughuli za ujenzi wa barabara, unaotajwa kuwa wa kujaribu kupunguza foleni ya magari. Foleni hiyo ilianza siku kumi na moja zilizopita katika barabara kuu ya kutoka Beijing kwenda Zhangjiakou katika jimbo la Hebei. Gazeti la Metro la London limeripoti kuwa magari hayo kimsingi yamesimama kabisa.

Image caption Foleni ya magari Uchina

Kituo cha televisheni cha Uchina, siku ya Jumanne wiki hii kilitangaza kuwa baadhi ya magari yamekwama katika foleni hiyo kwa siku tano. Siku ya Jumapili, magari yalisogea kwa nusu maili tu. Kutokana na msongamano huo, madereva wa magari hayo wamekuwa wakipoteza muda kwa kulala, kubishania bei za chakula kutoka kwa wachuuzi wanaouza vyakula barabarani na wengine wakicheza karata.

Bei za vyakula zimepanda, ambapo imeelezwa chupa moja ya maji iliyokuwa ikiuzwa kwa yen 10, hivi sasa bei yake ni mara kumi zaidi. Hakuna vyoo vya kujisaidia, hivyo madereva wamelazimika kujisaidia kando ya barabara, na wengine katika vichaka vilivyo karibu.

Na bado unalalamikia foleni yako ya saa tatu tu kutoka kazini kurudi nyumbani.

Mchezaji kobe

Mchezaji soka mmoja maarufu nchini Iran, amefukuzwa katika klabu yake kwa kuwa kobe.

Image caption Ali Karimi

Mtu anayekula mchana wakati wa mwezi mtukufu wa Ramadhani, bila sababu ya msingi, huitwa kobe.

Hata hivyo mchezaji huyo Ali Karimi ameambiwa anaweza kuendelea kuichezea klabu yake tena iwapo atalipa faini ya dola elfu arobaini za kimarekani. Kwa mujibu wa BBC, Ali Karimi anajulikana kama Maradona wa barani Asia. Ni maarufu sana nchini Iran na ni mmoja wa wachezaji walioichezea zaidi timu ya taifa ya nchi hiyo. Alifungiwa kuichezea klabu yake ya Steel Azin mapema mwezi huu baada ya kuonekana akinywa maji wakati wa mazoezi mchana.

Image caption Ali Karimi

Hata hivyo mashabiki walikasirishwa na hatua ya kumfugia mchezaji huyo na kuandaa migomo, na kumuunga mkono Maradona huyo. Aidha alipata kuungwa mkono na wachezaji wengine wa zamani wa Iran waliokuwa wakiacha kufunga Ramadhani wakati wa mazoezi, hasa katika kipindi hiki cha majira ya joto. Karimi baada ya kurejeshwa, amesema atalipa faini hiyo, lakini amekana kabisa kuibeza dini ya Kiisilam. Wachambuzi wa mambo wanasema hatua ya klabu yake kumsimamisha kazi ni ya kisiasa zaidi kuliko ya kidini. Mchezaji huyo amekuwa akiukosoa utawala wa klabu yake na hata wa chama cha soka cha nchi hiyo.

Mwizi kibogoyo

Mwizi mmoja kibogoyo nchini Uchina amekamatwa baada ya kuiba fedha katika benki moja mjini Beijing kwa kutumia silaha, ili akanunue meno ya bandia. Gazeti la Metro limesema kwa bahati mbaya, au nzuri mwizi huyo Li Han mwenye umri wa miaka arobaini na mitatu, anajulikana sana na polisi.

Image caption Mwizi alitaka kwena kununua meno

Wafanyakazi wa benki walipokuwa wakitoa maelezo ya mtu aliyefanya wizi huo, na kueleza kuwa mwizi alikuwa kibogoyo, asiye na jino hata moja, moja kwa moja polisi walifahamu mtu wao ni nani.

'Ana muonekano wa kipekee, na watu hupata tabu sana kumuelewa anapozungumza,' amesema afisa mmoja wa polisi, ambaye pia amesema, mwizi huyo, Li Han, anakabiliwa na kifungo cha miaka kumi na tano jela, kwa makosa ya wizi wa kutumia silaha. "Kukosa kwake meno, kunamfanya anabwabwaja maneno, na watu hawaelewi anasema nini" amesema polisi huyo na kuongeza " Yaani ilibidi arudie mara tano kumwabia afisa wa benki kuwa yeye ni mwizi na amekuja kuiba pesa hapo benki" amesema afisa huyo wa polisi ambaye hakutajwa jina lake.

Ugomvi na baisikeli

Bwana mmoja nchini Marekani amekamatwa na polisi baada ya kuanza kugombana na baisikeli yake. Polisi mjini Florida wamesema mtu huyo mwenye umri wa miaka sitini na nane alikuwa akigombana na baisikeli yake wiki hii nje ya kituo kimoja cha mafuta.

Image caption Kiserere

Gazeti la Toronto Sun limekaririwa likisema bwana huyo Richard bailon alikamatwa siku ya Jumanne mchana, mjini Stuart, huko Florida. Afisa wa polisi aliyemkamata bwana huyo amesema alimuona bwana Bailon akipiga kelele na kuitukana baiskeli yake, katika eneo la maehesho ya magari, kwenye kituo cha kujazia mafuta cha Mobil. Kwa mujibu wa faili la maelezo ya kiolisi, wateja waliokuwa wakifika katika kituo hicho kupata huduma ya mafuta, walitatizwa na kelele zilizokuwa zikifanywa na bwana Bailon, akiikaripia baisikeli yake kwa nguvu zote na kutoa matusi. Taarifa zinasema, bwana bailon amekamatwa na kushitakiwa kwa makosa ya ulevi na makosa madogomadogo.

Hakuna taarifa zozote kuhusu hatua gani zimechukuliwa dhidi ya baiskeli -- labda kwa kuwa haikuwa ikisema lolote, itakuwa imeachiwa huru tu.

Paka ndani ya pipa

Mwanamama mmoja hapa Uingereza aliyepigwa picha akimtupa paka aliye hai kwenye pipa la taka, amepewa ulinzi mkali wa polisi, baada ya watu wenye hasira na wapenda wanyama kutoa vitisho vya kumuua. Mwanamama huyo Mary Bale, awali aliliambia gazeti la Sun siku ya Jumatano kuwa haoni kwa nini kila mtu anashitushwa na kitendo chake hicho. " Si ni paka tu" alikaririwa akisema.

Image caption Paka ndani ya pipa?

Mwanamama huyo alionekana kwa kupitia kamera za uchunguzi za CCTV akimtupa paka wa jirani yake.

Picha hizo zilisambazwa kwenye internet na kuzua zogo kubwa kwnye mtandao. Paka huyo hatimaye alipatikana saa kumi na tano baadaye baada ya milio kusikika ikitoka ndani ya pipa la taka.

"yaani sijui mtu anawezaje kufanya hivyo, na akaenda kulala usiku na kupata usingizi mororo" amesema Darryl Mann, mwenye paka huyo, akizungumza na shirika la habari la Reuters. Hata hivyo mwenye paka huyo amesema paka wake anaendelea vizuri, baada ya kukumbana na songombingo hiyo.

Image caption Paka

Usitupe paka ndani ya pipa.....

Na kwa taarifa yako....Paka hana roho tisa kama inayosemwa....

Tukutane wiki ijayo, panapo majaaliwa.....

Taarifa zimekusanywa kutoka vyanzo mbalimbali kutoka kwenye mtandao.